Ujumbe wa Papa kwa wanahija Jimbo la Rieti:kuweni mashuhuda kwa kila hali ya maisha!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika fursa ya Hija ya Matumaini kwa mwaka 2025, waamini mbali mbali kutoka pande za dunia na ndani ya Nchi ya Italia wanafika mjini Vatican ili kupita Mlango mtakatifu. Ni katika fursa ya Hija ya kijubilei ya Jimbo Katoliki la Rieti nchini Italia, Jumamosi tarehe 29 Machi 2025, mjini Vatican ambapo Baba Mtakatifu Francisko amewatumia ujumbe wake, ambao akianza na salamu zake kwa Askofu wao, Vito Piccinonna na pamoja naye kwa wote: mapadre, mashemasi, watu waliowekwa wakfu, wale wenye majukumu ya kiraia, waamini wote, hasa wale wagonjwa na wazee, wanatoa sala na mateso kwa ajili ya wema wa Kanisa.
Katika ujumbe huo ni matashi ya Papa kuwa, ziara yao katika makaburi ya mitume na kupitia Mlango Mtakatifu, iwaongezee nguvu ya imani yao na kuwasaidia kuelewa na kupokea daima upendo zaidi wa Mungu, chemichemi na sababu ya furaha ya kweli. Baba Mtakatifu Francisko anabainisha kuwa hasa watu walio wadhaifu zaidi na wenye kuhitaji, sisi sote tunaalikwa kuwa mashuhuda wa upendo huo ambao kama mwali wa moto unatoa guvu ya kutembea katika maisha.
Kwa hisia hizo, “Papa Francisko anawatia moyo kuwa, kila siku wawe mashuhuda wa matumaini katika mazingira mbali mbali ya kikanisa na ya kuishi mahali wanapoishi, kwa kutoa mchango wa ujenzi wa ulimwengu wa kidugu zaidi na mshikamano, na wakati akiwaomba kuendelea kusali kwa ajili yake, Papa Francisko ameomba juu yao, ulinzi wa kimama wa Bikira Maria na Mtakatifu Barbara,(Msimamizi wa Mji wa Rieti) na kwa moyo amewapa baraka za Kitume na kuzisambaza kwa Jumuiya nzima ya Jimbo la Rieti.