杏MAP导航

Tafuta

Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini limetoa Ujumbe wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na Sikukuu ya ‘Id al-Fitr 1446 h. / 2025 A.D. Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini limetoa Ujumbe wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na Sikukuu ya ‘Id al-Fitr 1446 h. / 2025 A.D.   (AFP or licensors)

Ujumbe wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na Sikukuu ya Eid Al-Fitr

Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini limetoa Ujumbe wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na Sikukuu ya ‘Id al-Fitr 1446 h. / 2025 A.D. Nguzo kuu tano ambazo ni muhimu katika imani yao, nazo ni: Shahada (kukiri Imani), Sala, Zakat, Sawm, na Hija. Kalenda ya dini ya Kiislamu inaanza baaada ya Hija ya Mtume Muhammad (Salah Allah alaghi wa salaam – amani iwe kwake) kutoka Mecca kwenda Medina mwaka 622 AD na kuanzisha Jumuiya ya kwanza ya Kiislamu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu analihamasisha Kanisa kuhakikisha kwamba, linakuza na kuendeleza majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbalimbali duniani kwani huruma ya Mungu inavuka mipaka ya Kanisa na kumwambata kila mwamini. Waamini wa dini ya Kiislam wanamtambua Mungu kuwa ni Muumbaji, mwingi wa huruma na mpole. Hizi ni sifa za Mwenyezi Mungu zinazowasindikiza na kuwategemeza waamini wa dini ya Kiislam katika udhaifu wao wa kibinadamu. Waamini wa dini ya Kiislam wanaamini kwamba huruma ya Mungu haina mipaka kwani malango ya huruma ya Mungu yako wazi kwa kila mtu anayetaka kuikimbilia na kuiambata katika maisha yake. Maadhimisho ya Mwaka wa Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu anasema Baba Mtakatifu iwe ni fursa ya kumwilisha huruma ya Mungu katika maisha ya waamini wa dini mbalimbali, ili kujenga msingi wa majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa lengo la kutaka kufahamiana na kuelewana zaidi. Majadiliano ya kidini yasaidie kufuta kiburi na jeuri; udhalilishaji, ukatili na ubaguzi, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki na amani na maridhiano kati ya watu! Baba Mtakatifu anapenda kukazia kwa namna ya pekee majadiliano ya kidini yanayolenga kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Waamini wa dini mbali mbali wajitahidi kujenga madaraja ya watu kukutana na kuheshimiana ili kujenga umoja, urafiki na udugu wa kibinadamu licha ya tofauti zao za kidini, ambazo zinapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa kama amana na utajiri mkubwa katika maisha ya watu.

Nyumba ya Mungu
Nyumba ya Mungu

Hapa mwaliko ni kushirikiana kwa dhati kabisa ili kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazomwandama mwanadamu katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia. Lengo ni kudumisha misingi ya amani na utulivu, kikolezo kikuu cha: Utu, ustawi na maendeleo ya wengi. Kuna dhuluma, nyanyaso na ubaguzi kwa misingi ya kidini, mambo ambayo yanadhalilisha utu na heshima ya binadamu. Kumbe, waamini wa dini mbalimbali wanahamasishwa na Baba Mtakatifu Francisko kusimama kidete kulinda, kutetea, kudumisha na kujenga familia ya binadamu inayojikita katika umoja, upendo, msamaha na upatanisho unaobubujika kutoka katika undani wa maisha ya mwanadamu.Majadiliano ya kidini katika ukweli na uwazi, yanawasaidia waamini kushuhudia imani na utambulisho wao, ili kwa pamoja waweze kusimama kidete kutetea mafao ya wengi, udugu wa kibinadamu na mshikamano ili kujenga dunia iliyo bora zaidi. Majadiliano ya kidini yanapania kukuza amani, utulivu na usalama, changamoto na mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kujifunga kibwebwe ili kuhakikisha kwamba, inasaidia kumaliza vita na mipasuko ya kidini, ili kujenga haki na amani sehemu mbalimbali za dunia. Hapa waamini wanapaswa kuangaliana kwa jicho la huruma na upendo; kwa kuheshimiana na kuthaminiana hata katika tofauti zao za kidini, lakini kwa kutambua kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na kwamba, ni watoto wa Baba mwenye huruma.

Kufunga, Kusali na Matendo ya Huruma ni Muhimu wakati wa Ramadhani
Kufunga, Kusali na Matendo ya Huruma ni Muhimu wakati wa Ramadhani   (AFP or licensors)

Majadiliano ya kidini si dhana inayoelea katika ombwe, bali ni sehemu ya mchakato wa maisha ya kila siku; katika maisha ya kijamii kwa kuthamini na kuheshimu taratibu, kanuni na miiko ya waamini wa dini nyingine. Kutambua utu na heshima ya binadamu na haki zake msingi kwa kujenga madaraja ya watu kukutana na kusaidiana. Viongozi wa kidini wawe na ujasiri wa kuzuia, kukemea na kulaani vitendo vinavyofanywa na waamini wa dini zao kinyume cha utu, heshima na utakatifu wa maisha ya binadamu.Baba Mtakatifu Francisko anahimiza majadiliano ya kidini ili kujenga jamii inayowakumbatia na kuwaambata watu wote pasi na ubaguzi kwani ubaguzi ndio chanzo kikuu cha chokochoko, uhasama na mipasuko ya kijamii. Waamini washirikiane na kushikamana dhidi ya utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya watu wengine. Mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko mintarafu majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbalimbali duniani ni mwendelezo wa Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican pamoja na viongozi wengine waliofuatia. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican katika Waraka wao kuhusu majadiliano ya kidini: “Nostra aetate” wanaonesha umuhimu wa majadiliano ya kidini kama mbegu na chemchemi ya amani na utulivu katika ya Jumuiya ya kimataifa. Mtakatifu Paulo VI alikazia majadiliano ya kidini; Yohane Paulo II akaanzisha utamaduni wa amani kati ya waamini kwa kuitisha mkutano wa Assisi uliofanyika kunako mwaka 1986; Baba Mtakatifu Benedikto XVI akalitaka Kanisa kufanya majadiliano ya kidini katika ukweli na upendo kwa kuheshimu tofauti ili kujenga umoja na udugu wa kweli!

Sikukuu ya Eid El Fitr iwe ni chemchemi ya amani, matumaini na udugu
Sikukuu ya Eid El Fitr iwe ni chemchemi ya amani, matumaini na udugu

Ni katika muktadha wa kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini, Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini limetoa Ujumbe wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na Sikukuu ya ‘Id al-Fitr 1446 h. / 2025 A.D. Itakumbukwa kwamba, katika dini ya Kiislamu, kuna nguzo kuu tano ambazo ni muhimu katika imani yao, nazo ni: Shahada (kukiri Imani), Sala, Zakat, Sawm, na Hija. Kalenda ya dini ya Kiislamu inaanza baaada ya Hija ya Mtume Muhammad (Salah Allah alaghi wa salaam – amani iwe kwake) kutoka Mecca kwenda Medina mwaka 622 AD na kuanzisha Jumuiya ya kwanza ya Kiislamu (Ummah). Huo ndio mwaka mpya wa Kiislamu 622 (Anno Hegirae AH). Kwa hiyo kalenda ya dini ya Kiislamu inajulikana kama Hijri au Lunar kwa vile inafuata mwandamo wa Mwezi. Hii ndiyo inayotumika katika matukio ya imani na tamaduni zao, kama Sikukuu na mfungo. Ramadhani inatokana na neno la Kiarabu “???, Ramida au ar-ramad” likimaanisha, ukavu. Ramadhani ni kati ya miezi muhimu sana katika dini ya Kiislamu. Ramadhani ni mwezi mtukufu kwa waamini wa dini ya Kiislam kwa sababu ni katika mwezi huu Mungu (Allah) alimpa Mtume Muhammad (Salah Allah alaghi wa salaam) sura ya kwanza ya Kuruani Tukufu kunako mwaka 610. Sura hiyo al fatihah yaani ufunguzi, inasomwa yote katika kila sala kwa mwamini wa dini ya Kiislam. Hivyo ni maarufu kama Mama wa Kitabu au Mama wa Kuruani (Umm al Kitabu au umm al kuruani). Hii ni Sura inayomwalika mwamini wa dini ya Kiislam kutambua Ukuu wa Mungu muweza wa yote, kuomba ulinzi na huruma yake na kuendelea kumsifu. Ramadhani ni mwezi wa tisa katika Kalenda ya dini ya Kiislamu, ambapo Waislamu wanaalikwa kufunga, kuacha anasa na kusali zaidi ili kuwa karibu na Mwenyezi Mungu (Allah). Japo Waislamu wanasali kila siku tena mara tano inaaminika sala katika kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani inabeba uzito zaidi, kwa kuwa ni katika mwezi huu Mtume alikutana na Allah.

Waamini wa dini ya Kiislam wakisherehekea Eid El Fitri
Waamini wa dini ya Kiislam wakisherehekea Eid El Fitri   (ANSA)

Mwezi huu mtukufu kimsingi ni mfano wa nidhamu ya kibinafsi ambapo watu sio tu kwamba wanakata tamaa ya maji na chakula lakini pia hutumia wakati huu kuzama zaidi katika sala, matendo mema, hisani na huduma za jamii ambazo kimsingi huwasogeza waamini karibu zaidi na Mwenyezi Mungu. Mwezi mtukufu wa Ramadhan ukizingatiwa kuwa nguzo ya nne ya dini ya Kiislam umejengwa juu ya kanuni kama vile kujirekebisha, utakaso wa mawazo, kuwasaidia wenye shida na kupyaisha imani. Kwa mujibu wa Quran tukufu, huu ni mwezi wa maana sana kwani Mtume Mohammad alipokea aya za kwanza za Maandiko Matukufu. Kwa hiyo, mwezi huu unatajwa kuwa wakati muafaka wa kufunga na kusali kwa bidii na shauku kubwa. Kwa mujibu wa dini ya Kiislam, matendo mema yanayotekelezwa katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani huleta ustawi na mafanikio. Pia, inaaminika kuwa katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani, milango ya mbinguni hufunguliwa na mashetani hufungwa minyororo. Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni muda muafaka kwa waamini wa dini ya Kiislam kujikita katika tunu msingi za maisha na imani yao, kama ilivyo kwa Wakristo katika Kipindi cha Kwaresima kwa: Kufunga, Kusali, Kutafakari Neno la Mungu na kulimwilisha katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili pamoja na kujikita katika ushiriki mkamilifu wa Sakramenti za Kanisa. Kumbe, Mwezi Mtukufu wa Ramadhani umewawezesha waamini wa dini hizi mbili kutembea bega kwa bega katika mchakato wa pamoja wa utakaso, sala na upendo, kwa kutambua kwamba, waamini wote ni mahujaji wa matumaini na kwamba, wote wanatafuta kuishi maisha bora, kwa kuendelea kujikita katika ujenzi wa ulimwengu ulio bora zaidi, kwa kushuhudia urafiki wa Mungu pamoja na binadamu.

Sikukuu ya Eid El Fitr ni muda wa kumshukuru Mungu
Sikukuu ya Eid El Fitr ni muda wa kumshukuru Mungu   (ANSA)

Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa Wakristo ni kama shule ya mabadiliko ya ndani; toba na wongofu; kwa kujinyima, kutoa sadaka kama sehemu muhimu sana ya kuimarisha nidhamu ya mapambano ya maisha ya kiroho na kwamba, imani inapaswa kumwilishwa katika matendo mema, adili na matakatifu, kama sehemu ya mchakato wa wongofu wa ndani. Ulimwengu mamboleo una kiu ya udugu wa kibinadamu na majadiliano katika ukweli na uwazi, kwa kutangaza na kushuhudia urafiki wa Mwenyezi Mungu na binadamu. Matumaini ni sifa njema inayokita mizizi yake kwa imani katika Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema na Muumba wa vyote vinavyoonekana na visivyoonekana. Haya ni matumaini yanayosamehe na kuongoza na kwamba, upendo wa Mungu una nguvu zaidi kuliko majaribu na vikwazo katika hija ya maisha ya mwanadamu. Huu ni mwaliko kwa waamini wa dini hizi mbili kujibidiisha kujenga utamaduni wa kukutana, ili kudumisha udugu wa kibinadamu, kwa kuishi kwa pamoja katika haki na amani; kwa kuheshimiana na kushirikiana sanjari na kuendelea kujikita katika kanuni maadili na utu wema kama vile huruma, utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; kwa kujenga madaraja yanayowakutananisha waamini; kwa kusimama kidete kulinda, kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu; kwa kutangaza na kuenzi uzuri wa utofauti katika maisha ya binadamu. Kimsingi waamini wa dini hizi mbili wanataka kujikita katika mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu kwa kuheshimiana na kuthaminiana; kwa kuenzi na kudumisha uhai wa binadamu sanjari na utakatifu wa maisha kwa kutambua kwamba, imani ni chachu ya mabadiliko ya watu na jamii katika ujumla wake na kwamba, hii kimsingi ni nguvu ya umoja na upatanisho.

Ujenzi wa udugu wa kibinadamu katika utu, heshima na haki msingi
Ujenzi wa udugu wa kibinadamu katika utu, heshima na haki msingi   (Vatican Media)

Waamini wa Kanisa Katoliki wanayo furaha ya kushiriki katika Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na hatimaye kusherehekea kwa pamoja Sikukuu ya Eid El-Fitri ambayo imeadhimishwa tarehe 31 Machi 2025. Mchakato wa kutafuta na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano, iwe ni fursa kwa waamini wa dini hizi mbili kukutana na kusherehekea kidugu wema na utukufu wa Mwenyezi Mungu na hivyo kuendelea kushirikishana mbegu za matumaini zinazoweza kuleta mabadiliko katika jumuiya na ulimwengu katika ujumla wake, ili hatimaye, kuzima kiu ya amani na udugu wa kibinadamu. Sikukuu ya Eid El-Fitri iwe ni chemchemi ya amani, matumaini, udugu wa kibinadamu na furaha kwa wote.

Eid El Fitri 2025
31 Machi 2025, 14:56