Ujumbe wa Papa Francisko Kwa Mkutano Mkuu wa Taasisi ya Kipapa ya Maisha
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Taasisi ya Kipapa ya Maisha ilianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II, mnamo tarehe 11 Februari 1994, kwa Motu Proprio, yaani Barua binafsi ya “Vitae mysterium, Fumbo la maisha.” Lengo la taasisi hii ni kusimama kidete kulinda na kutetea thamani ya maisha na utu wa binadamu mintarafu Mafundisho Jamii ya Kanisa. Taasisi hii ina dhamana ya kutafiti, kuunda utamaduni wa maisha dhidi ya utamaduni wa kifo na kuhabarisha wadau mbalimbali changamoto zinazojitokeza katika mchakato wa kulinda na kudumisha Injili ya uhai duniani! Ni wajibu wa taasisi hii kutenda katika hali ya uwazi na kwa haraka na kwamba, inapaswa kuwajulisha viongozi wa Kanisa, taasisi za elimu maumbile na sayansi ya biolojia ya binadamu; taasisi za kiafya; vyombo vya mawasiliano ya jamii na jumuiya za kiraia kuhusu shughuli na tafiti zake kama sehemu ya mchakato wa kulinda na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Taasisi ya Kipapa ya Maisha, inawajibika kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha uhai wa binadamu, utu na heshima yake, tangu pale mtoto anapotungwa mimba tumboni mwa mama yake hadi mauti ya kawaida inapomfika kadiri ya mpango wa Mungu pamoja na kudumisha heshima kati ya vizazi. Ni wajibu wa taasisi hii kusaidia mchakato wa maboresho ya maisha ya binadamu; kwa kuendeleza tunu msingi za maisha: kiroho na kimwili, ili kudumisha Ikolojia ya binadamu kwa kumpatia mwanadamu nafasi yake katika Kazi ya Uumbaji.
Taasisi hii inapaswa kushirikiana kwa karibu zaidi na Sekretarieti kuu ya Vatican, Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kwa kuheshimu na kuzingatia dhamana na wajibu wa kila taasisi katika ari na moyo wa kushirikiana, ili kujenga na kudumisha utamaduni wa maisha. Taasisi pia inashirikiana pia na vyuo vikuu pamoja na taasisi za elimu ya juu zinazojihusisha na tafiti kuhusiana na maisha ya binadamu!Ni katika muktadha wa kutekeleza dhamana na majukumu yake, Taasisi ya Kipapa ya Maisha, kuanzia tarehe 3 hadi tarehe 5 Machi 2025 inaadhimisha Mkutano wake mkuu wa mwaka unaonogeshwa na kauli mbiu mbiu “Mwisho wa Dunia? Migogoro, Majukumu na Matumaini.” Mkutano huu unaadhimishwa katika Kituo cha Waagustino, kilichoko mjini Roma. Hii ni tema inayobeba uzito wa tafiti zilizofanywa mintarafu maisha ya binadamu, afya na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, katika hali na mazingira ya vita, athari za mabadiliko ya tabianchi, mgogoro wa nishati, magonjwa ya mlipuko, changamoto na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji sanjari na teknolojia rafiki. Mambo yote haya yangusa kwa namna ya pekee maisha ya binadamu, changamoto na mwaliko kwa mwanadamu kujiuliza kuhusu hatima ya ulimwengu na ufahamu wa mwanadamu.
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa washiriki wa mkutano huu, anakazia umuhimu wa kuchukua hatua ya kwanza kwa kufanya uchunguzi makini juu ya uwakilishi wa mwanadamu katika ulimwengu wa anga; hatua nyingine muhimu ni kuepukana kubaki bila kusonga mbele, kushikamana na uhakika, tabia na hofu za mwanadamu, bali kusikiliza kwa makini mchango unaotolewa na ujuzi wa kisayansi, ili kupata maarifa mapya kwa kujikita katika majadiliano na sayansi; kwa kutambua kwamba, vitu vyote vinategemeana na kukamilishana, kwa kumweka mwanadamu “homo sapiens” na mfumo mzima wa viumbe hai.Baba Mtakatifu anasema, katika ujumbe aliouandika akiwa Hospitali ya Gemelli tarehe 26 Februari 2025 anakaza kusema, njia hizi za kufasiri ulimwengu na mageuzi yake pamoja na njia mpya za uhusiano zinazolingana nazo, zinaweza kutoa ishara za matumaini, kama ilivyo katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, kwani tumaini linapyaishwa na kuwa na muungano wa kuwepo na watu na linaweza kufikiwa kwa kila mtu ndani ya watu hawa. Hii ni pamoja na mbinu mkakati wa kupambana na: Ujinga, baa la njaa na umaskini duniani kwa kuendelea kujikita katika katika mchakato wa kulinda na kudumisha utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili kukuza hali bora zaidi ya kisiasa; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hii ni kazi ya dharura inayowagusa binadamu wote na kwamba, hii ni sababu msingi ya kuanzishwa kwa Taasisi ya Kipapa ya Maisha. Baba Mtakatifu Francisko aliwaweka wajumbe wa mkutano mkuu wa Taasisi ya Kipapa ya Maisha chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Kikao cha hekima na Mama wa Matumaini wakati huu mwanadamu anaposafiri kuiendea “mbingu mpya na dunia mpya.” Ufu 21:1.