Tafakari ya Baba Mtakatifu Francisko Dominika 2 Machi 2025: Kutazama Na Haki!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican
Haki ni fadhila ya kibinadamu na Mababa wa Kanisa wanasema, haki ni fadhila adilifu iliyo na utashi wa kudumu na thabiti wa kumpa Mungu na jirani iliyo haki yao. Haki kwa Mungu huitwa “Fadhila ya Kimungu.” Haki kwa watu yaelekeza kuheshimu haki za kila mmoja, huanzisha mapatano katika mahusiano ya kibinadamu yanayoendeleza usawa kuhusu watu, mali ya Jumuiya. Mtu mwenye haki, anayetajwa mara nyingi katika Maandiko Matakatifu hutofautishwa kwa kawaida ya mawazo yake, unyofu wa mwenendo wake kwa jamii. “Usimpendelee mtu maskini, wala kumstaajabia mwenye nguvu; bali utamhukumu jirani yako kwa haki. Ninyi akina bwana, wapeni watumwa wenu yaliyo haki na adili, mkijua kuwa ninyi nanyi mna Bwana mbinguni.” KKK 1807. Fadhila ya haki inajulikana pia kwa lugha ya Kilatini kama “Unicuique suum.” Ni katika muktadha wa tafakari ya Neno la Mungu, kama ilivyoandaliwa na Baba Mtakatifu Francisko ambaye kwa sasa anasumbuliwa na ugonjwa wa mkamba (Bronchitis) uliopelekea kulazwa tangu Ijumaa tarehe 14 Februari 2025 kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli iliyoko mjini Roma anawaalika waamini kuzama katika kutazama na haki. Baba Mtakatifu katika tafakari yake ya Injili ya Dominika ya Nane ya Kipindi cha Mwaka C wa Kanisa, Dominika tarehe 2 Machi 2025 anajikita zaidi katika maneno makuu mawili: Kutazama na Haki.
Katika muktadha wa kutazama, Baba Mtakatifu anawaalika waamini kupanua wigo wao wa kuangalia mambo ya dunia na kumhukumu kwa haki na upendo jirani aliyeko mbele yao. “Mnafiki wewe, itoe kwanza ile boriti katika jicho lako mwenyewe, ndipo utakapoona vema kukitoa kile kibanzi kilichomo katika jicho la ndugu yako. Kwa maana hakuna mti mzuri uzaao matunda mabaya, wala mti mbaya uzaao matunda mazuri; kwa kuwa kila mti hutambulikana kwa matunda yake; maana, katika miiba hawachumi tini, wala katika michongoma hawachumi zabibu.” Lk 6:41- 45.Baba Mtakatifu anakaza kusema, lengo ni kumrekebisha mtu kwa upendo na udugu wa kibinadamu na wala si kulaani na kuhukumu. Kwa kuwa kila mti hutambulikana kwa matunda yake, yaani kwa njia ya maneno yanayotoka kinywani mwa mtu kwani “Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake.” Lk 6:44. Matunda maovu ni kama vile: maneno ya vurugu, uongo; pamoja na maneno machafu. Lakini maneno mazuri ni maneno sahihi ya uaminifu yanayotoa ladha nzuri katika mazungumzo. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujiuliza, Je, wanamwangaliaje jirani yake ambaye ni ndugu yake, Je, anajisikia namna gani kutazamwa na wao? Je! maneno yao yana ladha nzuri, au yamejaa uchungu na ubatili?
Baba Mtakatifu Francisko anasema, anawaandikia ujumbe huu, akiwa bado amelazwa kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli iliyoko mjini Roma tangu tarehe 14 Februari 2025. Taarifa kutoka Hospitalini Gemelli zinaonesha kwamba, Usiku wa kuamkia Dominika tarehe 2 Machi 2025, Baba Mtakatifu amepata usingizi mwanana na anaendelea na mapumziko. Baba Mtakatifu anasema, hospitalini hapo anasindikizwa na madaktari pamoja na wafanyakazi kutoka katika sekta afya na kwamba, kutoka katika sakafu ya moyo wake, anapenda kuwapongeza na kuwashukuru wale wote wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya maboresho ya afya yake. Anapenda kuwapatia baraka zake zinazobubujika kutoka katika sakafu ya moyo wake, kwani ni katika hali ya unyonge na udhaifu, mwanadamu anajifunza kujiaminisha mbele ya Mungu na kwamba, anamshukuru Mungu anayemwezesha kushiriki katika mateso ya wagonjwa wengi na wale wote wanao teseka: kiroho na kimwili.Baba Mtakatifu anapenda kuchukua fursa hii kuwashukuru watu wote wa Mungu na wenye mapenzi mema kutoka sehemu mbalimbali za dunia, wanao sali na kumwombea afya njema, kiasi kwamba, “anajisikia” kubebwa na kuenziwa na watu wa Mungu. Baba Mtakatifu anasema, hata yeye kwa upande wake anasali na kuwaombea, lakini zaidi anaombea amani. Hata leo hii, vita bado inaendelea kurindima sehemu mbalimbali za dunia. Vita inaendelea kuonekana kuwa ni kero. Baba Mtakatifu anasali na kuwaombea wote wanaoteseka nchini Palestina, Israeli, Lebanon, Myanmar, Sudan pamoja na Kivu nchini DRC. Baba Mtakatifu amehitimisha ujumbe wake kwa kujiaminisha na kujikabidhi, kwa Bikira Maria Mama wa Kanisa na hatimaye, akawatakia Dominika njema.