Sekretarieti Kuu ya Vatican Yaanza Mafungo ya Kiroho: Matumaini Na Uzima wa Milele
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mafungo ya maisha ya kiroho ni msaada kwa waamini kukuza na kudumisha: Moyo wa Sala, Ibada na Majitoleo kwa Mwenyezi Mungu pamoja na Kanisa lake. Ni wakati wa kufanya tafakari ya kina ya Neno la Mungu, tayari kulimwilisha katika uhalisia wa maisha na wito wa kila mmoja wao. Ni wajibu wa waamini kutambua uwepo wa Mungu katika kazi ya uumbaji, bila ya kumwogopa. Itakumbukwa kwamba, wakati fulani katika maisha yao, Mitume walishikwa na woga, kwa sababu hawakuwa na imani thabiti kiasi cha kumwomba Kristo Yesu awaongezee imani. Hali hii inaweza kumkuta mwamini ikiwa kama hawezi kuzamisha mahusiano na mafungamano yake ya dhati na Kristo Yesu na kusahau kwamba, Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma, upendo na msamaha kwa wale wote wanaomkimbilia kwa moyo wa toba na wongofu wa ndani. Huu ni muda muafaka wa kuingia katika jangwa la maisha ya kiroho. “Jangwa” au "Upweke mtakatifu" ni muhimu sana katika maisha na utume wa waamini ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Ni baada ya Yesu kubatizwa na Roho kutua kama njiwa juu yake. Roho huyo huyo aliyetua juu ya Yesu, anamtoa na kumpeleka jangwani. Huko anakaa siku 40 akijaribiwa na Shetani, Ibilisi. Hizi ni alama zenye maana kubwa sana katika utume wa Yesu. Baba Mtakatifu Francisko anasema jangwa ni mahali ambapo Mwenyezi Mungu anazungumza kutoka katika undani wa mtu mwenyewe, yaani dhamiri nyofu. Hii ni chemchemi ya majibu ya Mungu katika sala. Ni mahali pa majaribu na kishwawishi kikubwa! Kumbe, jangwa, katika Biblia, ni mahala ambapo mtu anajitambua “ni nani” mbele ya watu na mbele ya Mungu. Kwa kuzingatia historia ya Waisraeli waliosafiri jangwani kwa miaka 40 kuelekea nchi ya ahadi, jangwa lilikuwa ni mahala pa kujaribiwa uaminifu, mahala pa kutakaswa na mahala pia pa kuonja wema, upendo na huruma ya Mungu. Wakiwa jangwani Mungu aliwaonesha upendo wake mkuu kwa kuwalinda, kuwaongoza, kuwapatia chakula na hatimaye kuwaokoa!
Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2025 unanogeshwa na kauli mbiu “Tutembee kwa pamoja katika matumaini.” Kwaresima ni kipindi cha imani na matumaini; toba na wongofu wa ndani, ili kukumbatia na kuambata huruma na upendo wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa mtu mmoja mmoja na kama Jumuiya ya waamini. Kwaresima ni kipindi cha kuimarisha na kuboresha imani, matumaini na mapendo kwa: kufunga na kusali; kwa kufanya toba na malipizi ya dhambi; kwa kushiriki kikamilifu katika Sakramenti za Kanisa; Kwa kusoma, kutafakari na hatimaye, kumwilisha Neno la Mungu katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo makini cha imani tendaji. Lengo ni kujitakasa na hatimaye, kuambata utakatifu wa maisha, ili kushiriki furaha ya Kristo Mfufuka wakati wa Sherehe ya Pasaka ya Bwana, huku waamini wakiwa wamepyaishwa kwa neema ya Roho Mtakatifu. Waamini watambue kwamba, wanaitwa kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao kwa watu wanaowazunguka na wale wote ambao Mwenyezi Mungu anawajalia fursa ya kukutana nao katika hija ya maisha yao, ili waweze kujaliwa mwanga na furaha ya Injili katika maisha. Mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani, kiwe ni kikolezo cha toba na wongofu wa ndani kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa.
Ni katika muktadha huu, Sekretarieti kuu ya Vatican kuanzia tarehe 9 hadi 14 Machi 2025 “inapanda kwenda jangwani” kwa ajili ya mafungo ya maisha ya kiroho, kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Pasaka ya Bwana, sanjari na Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo. Mafungo haya yanaongozwa na Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., mwenye umri wa miaka 53, Mtaalamu wa Sayansi ya Maandiko Matakatifu, ambaye, Mwezi Novemba 2024 aliteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa na hivyo kuchukua nafasi ya Kardinali Raniero Cantalamessa ambaye aling’atuka baada ya kuhubiri kwa muda mrefu. Kutokana na hali ya afya ya Baba Mtakatifu Francisko kuwa tete alilazimika kulazwa kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli iliyoko mjini Roma tangu Ijumaa tarehe 14 Februari 2025; kwa hakika anasema anaonja: umakini wa huduma na huruma kutoka kwa madaktari na wafanyakazi katika sekta ya afya hospitalini hapo. Baba Mtakatifu ametumia fursa ya tafakari ya Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 9 Machi 2025 kuwatakia heri na baraka wafanyakazi wote wa Sekretarieti kuu ya Vatican wanapofanya mafungo ya mwaka na kwamba, anaungana nao kiroho. Taarifa rasmi kutoka kwa Dr. Matteo Bruno, Msemaji mkuu wa Vatican inaonesha kwamba, hali ya afya ya Baba Mtakatifu Francisko inaendelea kuimarika zaidi kwa kupumua kama kawaida pamoja na kuendelea na mazoezi ya kupumua kwa viungo bila mashine. Kuanzia Jumamosi, hadi Jumatatu tarehe 10 Machi 2025, Baba Mtakatifu Francisko ameendelea kupata tiba, kufanya mazoezi ya viungo, kusali, kutafakari pamoja na kufanya kazi ndogo ndogo pamoja na kujipatia mapumziko marefu nwa kwamba, Jumatatu tarehe 10 Machi 2025, Baba Mtakatifu alipata usingizi mwanana na anaendelea na mapumziko yake kama kawaida.
Kiini cha mafungo haya ni “Tumaini la Maisha na Uzima wa Milele” kama Mama Kanisa anavyofundisha na kuungama katika Kanuni ya Imani ya Nicea: “Nangojea na ufufuko wa wafu, na uzima wa milele ijayo. Amina.” Makanisa na Madhehebu mbalimbali ya Kikristo yanajiandaa kuadhimisha Jubilei ya Miaka 1, 700 tangu Mtaguso wa Kwanza Nicea ulipoadhimishwa kunako mwaka 325 na kilele cha maadhimisho haya ni mwaka 2025, tukio la pekee na muhimu sana. Mwaka huu wa 2025 wakristo wote wanaadhimisha Pasaka ya Bwana siku moja, matendo makuu ya Mungu kwa waja wake. Kanuni ya Imani ya Nicea-Constantinopoli ni formula rasmi ambayo ilipitishwa na Mababa wa Mtaguso wa Kwanza wa Nicea (325) ikakamilishwa na Mtaguso wa kwanza wa Konstantinopoli (381) ili kubainisha imani sahihi ya Kanisa Katoliki dhidi ya uzushi, hasa wa Ario na wafuasi wake. Katika mazingira hayo, lengo kuu lilikuwa kwanza kabisa ni kumkiri Kristo Yesu “Mungu kweli kwa Mungu kweli” yaani Mungu kweli sawa na Baba, halafu kwamba Roho Mtakatifu anastahili kuabudiwa pamoja na Baba na Mwana (Utatu Mtakatifu). Wakristo wanataka kutembea pamoja na Kristo ambaye ni njia, ukweli na uzima.
Mababa wa Kanisa wanasema, maana ya Kikristo ya kifo imefunuliwa katika mwanga wa Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo ambaye ndani yake mna tumaini la Wakristo. Mkristo anayekufa katika Kristo Yesu huuacha mwili ili kwenda kukaa pamoja na Mwenyezi Mungu, milele yote! Kwa Mkristo, siku ya kifo huanzisha, mwishoni mwa maisha yake ya Kisakramenti, utimilifu wa kuzaliwa kwake upya kulikoanzishwa na Sakramenti ya Ubatizo, kufanana kamili na sura ya Mwana, kulikotolewa kwa Mpako wa Roho Mtakatifu na ushirika katika karamu ya Ufalme, uliotangulizwa katika Ekaristi, hata kama ana lazima bado kutakaswa zaidi ili kuvikwa vazi la arusi! Waamini wanahamasishwa kulitafakari Fumbo la kifo, kama sehemu ya matumaini ya Kikristo kwani, Kristo Yesu mwenyewe anasema, ndiye ufufuo na uzima na kwamba, yeyote anayemwamini ajapokufa atakuwa anaishi na kwamba, heri yao wale wote wanaokufa katika Kristo Yesu. Matumaini ya Kikristo yawasaidie waamini kukabiliana na Fumbo la kifo kwa imani na matumaini na kwamba, hata ustaarabu wa watu wa kale umepitia katika fumbo hili na kwa hakika, ibada ya kifo ni sehemu ya vinasaba vya maisha ya binadamu.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, kifo ni sehemu ya matukio ya maisha ya mwanadamu, ni urithi na kumbukumbu. Tangu pale mwanadamu anapozaliwa, anaanza safari ya kuelekea katika Fumbo la kifo, changamoto na mwaliko kwa waamini kumwomba Mwenyezi Mungu ili aweze kuwakirimia kufa kifo chema badala ya kujifungia katika muda na ubinafsi wao! Mama Kanisa anawataka watoto wake kujiandaa vyema ili kukabiliana na Fumbo la kifo katika maisha yao. Kifo ni urithi unaofumbatwa katika ushuhuda ambao unapaswa kutolewa kwa wale wanaobaki. Baba Mtakatifu anawataka Wakristo kujiuliza swali la msingi, Je, wewe leo ukifa utaacha ushuhuda gani nyuma yako? Swali hili liwasaidie waamini kujiandaa kufa vyema. Lakini, kabla ya kuitupa mkono duniani Je, kuna jambo gani ambalo ningependa kulifanya leo hii? Fumbo la kifo liwasaidie waamini kufikiri na kutenda kila siku wakitambua kwamba, daima wako safarini kuelekea kufani! Maswali haya ni muhimu kwa waamini wote, ili kuweza kujiandaa vyema ili kukabiliana na Fumbo la kifo! Mafungo haya yanachota amana na utajiri wake kutoka katika Katekisimu ya Kanisa Katoliki, Maandiko Matakatifu pamoja na Mapokeo hai ya Kanisa.