杏MAP导航

Tafuta

Sanda Takatifu ni kielelezo cha upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na kifani kwa waja wake na kwa njia hii, waamini pia wanaweza kuona sura ya ndugu zao wanaoteseka: kiroho na kimwili sehemu mbalimbali za dunia! Sanda Takatifu ni kielelezo cha upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na kifani kwa waja wake na kwa njia hii, waamini pia wanaweza kuona sura ya ndugu zao wanaoteseka: kiroho na kimwili sehemu mbalimbali za dunia!  

Sanda Takatifu ya Torino Ni Injili Hai, Kielelezo cha Upendo Na Huruma ya Mungu

Sanda Takatifu inaweza kufananishwa kama kioo cha Injili. Hii ni sura ya mwanadamu anayeendelea kuteseka, kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba yaani mateso, kifo na ufufuko. Hii ni ishala ya ukimya unaowachangamotisha waamini kulitafakari kwa kina Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu na kwamba, kifo si hatima ya maisha ya mwanadamu, kwani baada ya kifo, kuna maisha ya uzima wa milele.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Mwaka 2025 ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani “Mahujaji wa matumaini.” Matumaini ya waamini yako katika Msalaba, yaani katika Kristo Yesu, chemchemi ya wokovu wa mwanadamu aliyezaliwa katika Familia Takatifu iliyopata baraka ya kuwa na Mungu yaani Emanueli kati yake.  Huu ni muda muafaka wa kukimbilia na kuambata huruma na upendo wa Mungu; kwa kuweka kando mizigo ya zamani, na kupyaisha msukumo kuelekea siku zijazo; ili kusherehekea uwezekano wa mabadiliko katika maisha, kwa kujitahidi kupyaisha utambulisho wa waamini na kuwa jinsi walivyo, kwa njia ya imani, tayari kushuhudia ubora wao katika maisha ya kila siku. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kupita katikati ya Mlango wa Imani kwani Kristo Yesu anasema “Mimi ndimi mlango; mtu akiingia kwa mimi, ataokoka; ataingia na kutoka, naye atapata malisho.” Rej. Yn 10: 1-18. Ni katika muktadha huu, Jimbo kuu la Torino, lililoko Kaskazini mwa Italia kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Mwaka 2025 ya Ukristo, limeandaa “Tamasha la Vijana linaloanza kutimua vumbi tarehe 28 Aprili hadi tarehe 5 Mei 2025 na hivyo kuhitimisha Mzunguko wa Katekesi ulioanza mwaka 2024 hadi mwaka 2025, kwa mwaliko kwa vijana kutafakari: Sanda iliyoviringishwa, Matumaini sanjari na Maadhimisho ya Jubilei.

Taji la Miiba
Taji la Miiba

 

Katekesi ya vijana, ilizinduliwa rasmi tarehe 8 Novemba 2024 kwa kuwahusisha vijana wenye umri kati ya miaka 18 hadi 30. Jimbo kuu la Torino, linamshukuru Mungu kwa maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya kidijitali ambayo inaliwezesha sasa Jimbo hilo kuweza kuonesha “Sanda Takatifu ya Torino” sehemu mbalimbali za dunia. Kumbe, mahujaji wa matumaini mahali popote pale walipo wanaweza kutembelea na hatimaye kujionea maajabu ya Sanda Takatifu ya Torino kuanzia tarehe 28 Aprili hadi tarehe 5 Mei 2025. Kardinali Roberto Repole, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Torino anasema, Sanda Takatifu ya Torino ni ushuhuda wa mtu aliyeshindwa na historia, aliyeteswa na kufa kifo cha aibu, kielelezo cha matukio ya vita, magonjwa, umaskini, dhuluma na nyanyaso. Sanda Takatifu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kupyaisha maisha yao na hivyo kuyakita katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu uletao maisha na uzima wa milele. Sanda Takatifu ya Torino, haitaweza kuoneshwa hadharani kwa macho maputu, bali kwa njia ya mawasiliano ya kidijitali na hivyo waamini wanaweza kujionea: Sura, Shada la Miiba pamoja na Alama za Misumari katika Mwili wa Kristo Yesu. Onesho hili la kidijitali limebuniwa hasa zaidi kwa ajili ya vijana wa kizazi kipya, kama sehemu ya Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo na kama Tamasha la Vijana. Inaweza kufuatilia onesho hili kwa anuani ifuatayo:   www.sindone.org

Mijeledi iliyotumika wakati wa mateso ya Kristo Yesu
Mijeledi iliyotumika wakati wa mateso ya Kristo Yesu

Itakumbukwa kwamba, kuna mamillioni ya watu ambao wamekuwa wakifanya hija ya kiroho, ili kutembelea na kutafakari mateso na mahangaiko ya mwanadamu yanayojionesha kwenye Sanda Takatifu ya Torino. Kunako mwaka 1973, Mtakatifu Paulo VI, katika ujumbe wake wakati wa Onesho la kwanza alisikika akisema kwamba, pamoja na tafiti na mahitimisho mbalimbali yaliyofanywa na wanasayansi kuhusiana na Sanda Takatifu ya Torino, lakini hapa kuna sura ya “Mungu kweli na Mtu kweli”, inayoonesha mateso ya mwanadamu. Kunako mwaka 1998, Mtakatifu Yohane Paulo II alitambua na kuthamini mchango uliokuwa umetolewa na wanasayansi kwa kutumia vipimo vya kisasa ili kutambua uhalisia wa Sanda Takatifu ya Torino na kukiri kwamba, Sanda Takatifu ni changamoto kubwa kwa akili ya mwanadamu. Papa Yohane Paulo wa Pili aliwataka wanasayansi kuendelea na uchunguzi wao, lakini wakiheshimu imani ya waamini, kwani Sanda Takatifu inaweza kufananishwa kama kioo cha Injili. Hii ni sura ya mwanadamu anayeendelea kuteseka, kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu unaofumbatwa katika Fumbo la Msalaba. Sanda Takatifu ni ishala ya ukimya unaowachangamotisha waamini kulitafakari kwa kina Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu na kwamba, kifo si hatima ya maisha ya mwanadamu, kwani baada ya kifo, kuna maisha ya uzima wa milele.

Misumari iliyotumika kumtundikia Yesu Msalabani
Misumari iliyotumika kumtundikia Yesu Msalabani

Baba Mtakatifu Benedikto XVI kunako mwaka 2010 alitembelea Jimbo kuu la Torino, ili kutoa heshima yake kwa Sanda Takatifu na hatimaye kusema kwamba, Sanda Takatifu ni kielelezo cha Jumamosi kuu, inayoonesha kimya kikuu na mwendelezo wa mchakato wa mbegu iliyozikwa ardhini, iweze kuchipua na kuzaa matunda ya matumaini. Sanda Takatifu inagusa giza la imani lakini pia ni mwanga wa matumaini yasiyokuwa na mwisho. Kwa upande wake Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2013, mara tu baada ya kuchaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, alisema, Sanda Takatifu inaonesha macho yaliyofumbwa, na mwili wa maiti, lakini bado unaendelea kuwaangalia watu na katika ukimya wake, maiti hii, inazungumza na kuwahoji watu kutoka katika undani wa maisha yao. Hii ni sura inayoangalia kwa upendo na hakuna cha zaidi kinachotafutwa na sura hii. Katika kitabu cha kumbukumbu ya mahujaji waliotembelea na kusali mbele ya Sanda Takatifu, hakuna hata mtu mmoja aliyeomba kufanyiwa muujiza, maneno ya mshangao na shukrani ndiyo yanayoonekana kwa wingi. Sanda Takatifu inazungumza kuhusu Kristo Yesu, lakini kwa namna ya pekee, inagusa mateso na mahangaiko ya watu wengi wanaoteseka sehemu mbalimbali za dunia. Hawa ni watu wenye madonda makubwa katika maisha yao; watu ambao utu na heshima yao vimewekwa rehani kutokana na vita, magonjwa, umaskini, dhuluma na nyanyaso. Sanda Takatifu inaonesha michirizi ya damu, kielelezo cha Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu aliyetwaa mwili na kukaa kati ya watu wake, ili kuwashirikisha huruma na upendo wa Mungu.

Sanda Takatifu ni kielelezo cha Ijumaa kuu
Sanda Takatifu ni kielelezo cha Ijumaa kuu

Sanda ya Yesu ni Injili Hai; Kielelezo cha Upendo na Huruma ya Mungu; Taabu na mateso ya mwanadamu. Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili kunako tarehe 23 hadi 24 Mei, 1998, alifanya hija ya kichungaji Jimbo kuu la Torino, akapata nafasi ya kuabudu Ekaristi Takatifu, kiini cha maisha na utume wa Kanisa. Baadaye alitembelea Sanda ya Yesu, inayoweza kuwa ni msaada mkubwa wa kiimani kwa waamini kuweza kuonja upendo na huruma ya Kristo Yesu, Neno lwa Mungu aliyefanyika mwili, kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu. Sanda ya Yesu ni kielelezo cha taabu na mahangaiko ya mwanadamu, licha ya maendeleo ya sayansi na teknolojia. Ni ushuhuda wa hekima inayofumbatwa katika Mti wa Msalaba wa Kristo. Ni mateso kama haya yanayoendelea kujidhihirisha katika uso wa dunia kwa mamillioni ya watu wanaokufa kwa njaa, vita, unyonyaji na unyanyasaji wa wanawake na watoto; watu wanaoendelea kusukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na umaskini na magonjwa; watu ambao haki na utu wao kama binadamu havithaminiwi kutokana na dhuluma na mashambulizi ya kigaidi. Sanda ya Yesu ni mwaliko kwa waamini na watu wenye mapenzi mema, kuvua utu wao wa kale unaogubikwa na ubinafsi na uchoyo na hivyo kuanza hija ya maisha mapya, kwa kutembea katika Mwanga wa Kristo Mfufuka, kwa kutafuta utakatifu na wongofu wa ndani, kwa ajili ya wokovu wa binadamu. Ni kielelezo cha upendo wa Mungu, licha ya dhambi za binadamu. Upendo wa Mungu ni hazina kubwa ambayo Mwenyezi Mungu ameweza kuwakirimia watu wake. Sanda hii inamwalika mwamini pia kulifikiria Fumbo la Umwilisho, Neno wa Mungu alipoutwaa mwili na kukaa kati ya watu wake, katika mambo yote akawa sawa na binadamu, isipokuwa Yeye hakutenda dhambi. Hiki ni kielelezo cha hija ya maisha ya Kristo Yesu, baada ya mateso na kifo chake Msalabani, kuelekea utukufu na ufufuko wake kutoka katika wafu, matumaini ya wote wanaoteseka na kuhangaika katika maisha yao huku Bondeni kwenye machozi.

Sanda Takatifu itaangaliwa kwa mfumo wa kidijitali: vijana wa kizazi kipya
Sanda Takatifu itaangaliwa kwa mfumo wa kidijitali: vijana wa kizazi kipya   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Baba Mtakatifu Francisko anasema kwamba, Sanda Takatifu ni kielelezo cha upendo mkuu wa Yesu Kristo kwa binadamu; upendo ambao hata kwa wakati huu, umekuwa na mvuto kwa watu wengi waliofika kutembelea mji wa Torino. Sura na mwili wa Yesu unaooneshwa kwenye Sanda Takatifu ni ushuhuda wa kila mtu anayeteseka kwa kutotendewa haki pamoja na kudhulumiwa, mwaliko wa kuambata upendo wa Mungu kwa binadamu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Mtakatifu Giuseppe Benedetto Cottolengo kwa kusukumwa na upendo wa Mungu, akaamua kauli mbiu yake iwe ni yale maneno ya Mtakatifu Paulo “Caritas Christi urges nos” “Upendo wa Kristo unatuwajibisha.” Sanda Takatifu inayohifadhiwa Jimbo Kuu la Torino, Kaskazini mwa Italia ni Kisakramenti kinachowasaidia waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuona sura ya Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wakfu kadiri ya Maandiko Matakatifu. Sanda Takatifu ni kielelezo cha upendo na huruma ya Mungu isiyokuwa na kifani kwa waja wake na kwa njia hii, waamini pia wanaweza kuona sura ya ndugu zao wanaoteseka: kiroho na kimwili sehemu mbalimbali za dunia! Katika shida na mahangaiko ya binadamu kwa wakati huu kutokana na majanga mbalimbali yanayomwandama, Mama Kanisa anawaalika watoto wake kuwa na imani, matumaini na mapendo thabiti, kwani nguvu ya Kristo Mfufuka imeshinda dhambi na mauti! Sanda Takatifu ni ufunuo wa Mtumishi wa Bwana aliyedharauliwa na kukataliwa na watu, mtu wa huzuni nyingi, ajuaye sikitiko! Hakika ameyachukua masikitiko ya mwanadamu, akajitwika huzuni yake, akadhaniwa kuwa amepigwa, tena amepigwa na Mungu na kuteswa! Alichubuliwa na kuteswa kwa maovu ya binadamu. Adhabu ya amani ya binadamu ilikuwa juu yake na kwa kupigwa kwake, binadamu amepona! Rej. Isa. 53: 3. 4-5.

Sanda Takatifu ni kielelezo cha mateso na mahangaiko ya binadamu.
Sanda Takatifu ni kielelezo cha mateso na mahangaiko ya binadamu.   (AFP or licensors)

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, sura iliyoko kwenye Sanda Takatifu ni kielelezo na ufunuo wa sura za: maskini, wagonjwa na watu wanaoishi katika upweke hasi; wagonjwa ambao hawana uwezo wa kupatiwa tiba muafaka kutokana na maradhi yanayowasibu. Hii ni sura ya watu wanaoteseka kutokana na vita pamoja na ghasia sehemu mbali mbali za dunia; watu wanaotumbukizwa katika biashara ya binadamu na viungo vyake, utumwa mamboleo; nyanyaso na dhuluma mbalimbali. Kama Wakristo katika mwanga wa Maandiko Matakatifu, wanatafakari Sura ya Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Wakristo wana imani na matumaini kwa Kristo Yesu kwa sababu daima anasikiliza sauti na kilio cha waja wake wanaomlilia usiku na mchana naye anawaokoa! Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kujiunga na mateso ya Kristo Yesu, ili hatimaye, waweze kuonja neema na baraka ya ufufuko na uzima wa milele.

Sanda Takatifu
17 Machi 2025, 10:44