Rozari Takatifu Kumwombea Papa Francisko: Bikira Maria wa Mateso
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican
Waamini katika Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mateso wanayakumbuka mateso ambayo Bikira Maria aliyapitia katika maisha na utume wake. Kristo Yesu alipotolewa Hekaluni, Mzee Simeoni alitabiri kwamba, upanga utaingia moyoni mwa Bikira Maria, ili yafunuliwe mawazo ya mioyo mingi! Bikira Maria, Mtakatifu Yosefu pamoja na Mtoto Yesu, walilazimika kukimbilia ugenini, huko Misri ili kusalimisha maisha ya Mtoto Yesu. Baba MtakatifuFrancisko anasema, Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu waliingiwa na wasi wasi na hofu kubwa, wakaanza kumtafuta Mtoto Yesu kwa muda wa siku tatu bila mafanikio na hatimaye, wakamkuta Yesu akiwa Hekaluni. Katika Njia ya Msalaba, Bikira Maria alikutana na Yesu, akamsindikiza hadi pale Mlimani Kalvari, chini ya Msalaba akashuhudia kifo chake! Wakamteremsha kutoka Msalabani na kumkabidhi Bikira Maria. Baada ya yote haya, Yesu akazikwa kaburini. Kwa karne nyingi, waamini wamejenga na kukuza Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mateso. Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika Sala ya Malaika wa Bwana, Mama Kanisa daima anamkumbuka Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Huyu ni Mama aliyejisadaka na kujitoa kwa ajili ya wengine kama ilivyokuwa kwenye arusi ya Kana ya Galilaya, akakubali kuwa ni Mama wa wote. Bikira Maria katika maisha na utume wake, akawa ni mwanafunzi mwaminifu wa Kristo Yesu, akajifunza kutoka kwake, na kumsindikiza katika maisha na utume wake. Akawasindikiza wanawake wachamungu waliovutwa na huduma ya Kristo Yesu katika maisha yao!
Kuna wakati, Bikira Maria na ndugu zake, walidhani kwamba, “Yesu alikuwa amechanganyikiwa” wakaenda kumwona, lakini hawakupata nafasi! Bikira Maria akamfuata Mwanae wa pekee, hadi kudiriki kusimama chini ya Msalaba na kushuhudia jinsi ambavyo walimnyanyasa na kumdharirisha Kristo Yesu! Lakini, akaendelea kuwa jasiri kama Mama na hatimaye, Kristo Yesu akiwa chini ya Msalaba, akamkabidhi kwa yule Mwanafunzi aliyempenda na tangu wakati huo, akawa ni Mama wa waamini wote. Ni Mama aliyeshirikiana na kushikamana na Mitume wa Yesu katika kusali!Baba Mtakatifu anakaza kusema, Bikira Maria, aliendelea kuwa ni Mama na mwanafunzi hodari wa Kristo Yesu; mwaliko kwa waamini kumtafuta, ili kukimbilia ulinzi na tunza yake ya kimama. Maria ni Mama na Bikira, mfano hai wa utimilifu wa Kanisa. Hata Kanisa, kwa kuutazama utakatifu wa Bikira Maria, kwa kuiga upendo wake na kutimiza mapenzi ya Mungu, linakuwa pia ni Mama. Kwani kwa njia ya mahubiri na Sakramenti ya Ubatizo linazaa watoto waliotungwa kwa uwezo wa Roho Mtakatifu na hivyo kuzaliwa kwa Mungu, kwa uzima mpya usiokufa! Kanisa ni Mama wa wote, watakatifu na wadhambi wanaopaswa kutubu na kumwongokea Mungu. Kumbu kumbu ya Ibada ya Bikira Maria, Mama wa Mateso iwe ni fursa kwa waamini kutafakari Fumbo la mateso katika maisha yao! Waguswe na mateso ya Bikira Maria katika maisha na utume wake, ili hatimaye, waweze kumtolea sifa na heshima kwa kukubali kuwa ni Mama wa Mungu na Kanisa.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Bikira Maria alilia kwa uchungu mkubwa na moyo wake kujeruhiwa vibaya kutokana na mateso na kifo cha Mwanaye Mpendwa Kristo Yesu. Leo hii, Bikira Maria anawaonesha huruma wale wote wanaoendelea kuteseka kutokana na umaskini, magonjwa, njaa, ujinga na umaskini sanjari na kusukumizwa pembezoni mwa jamii na wakuu wa ulimwengu huu. Bikira Maria Mama wa Mateso awe ni faraja kwa wale wanaoteseka; matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo na awe ni chemchemi ya huruma na mapendo kwa wenye huzuni na mahangaiko makubwa! Kumbukumbu ya Bikira Maria Mama wa Mateso anasema Mtakatifu Paulo VI katika Wosia wake wa Kitume “Marialis cultus” yaani “Ibada kwa Bikira Maria”, huu ni mwaliko kwa waamini kutafakari kile kipindi maalum katika historia ya ukombozi wa mwanadamu na hivyo kumheshimu Bikira Maria aliyeshiriki kwa namna ya pekee katika mateso ya Mwanaye mpendwa Kristo Yesu, kiasi hata cha kudiriki kusimama chini ya Msalaba na kupokea maiti ya Mwanaye! Rej. Yn. 19: 25-27. Umama wa Bikira Maria unachukua nafasi ya pekee pale Mlimani Kalvari, chini ya Msalaba. Itakumbukwa kwamba, Ibada ya Kumbukumbu kwa heshima ya Bikira Maria Mama wa Mateso iliandikwa kwenye Kalenda ya Kanisa Katoliki kunako mwaka 1814. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kufafanua kwamba, waamini katika Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mateso wanayakumbuka mateso ambayo Bikira Maria aliyapitia katika maisha na utume wake.
Kwa karne nyingi, waamini wamejenga na kukuza Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mateso. Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika Sala ya Malaika wa Bwana, daima anamkumbuka Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Huyu ni Mama aliyejisadaka na kujitoa kwa ajili ya wengine kama ilivyokuwa kwenye arusi ya Kana ya Galilaya, akakubali kuwa ni Mama wa wote. Bikira Maria katika maisha na utume wake, akawa ni mwanafunzi mwaminifu wa Kristo Yesu, akajifunza kutoka kwake, na kumsindikiza katika maisha na utume wake. Akawasindikiza wanawake wachamungu waliovutwa na huduma ya Kristo Yesu katika maisha yao! Kuna wakati, Bikira Maria na ndugu zake, walidhani kwamba, “Yesu alikuwa amechanganyikiwa” wakaenda kumwona, lakini hawakupata nafasi! Bikira Maria akamfuata Mwanae wa pekee, hadi kudiriki kusimama chini ya Msalaba na kushuhudia jinsi ambavyo walimnyanyasa na kumdharirisha Kristo Yesu! Lakini, akaendelea kuwa jasiri kama Mama na hatimaye, Kristo Yesu akiwa chini ya Msalaba, akamkabidhi kwa yule Mwanafunzi aliyempenda na tangu wakati huo, akawa ni Mama wa waamini wote. Ni Mama aliyeshirikiana na kushikamana na Mitume wa Yesu katika kusali!
Kardinali Víctor Manuel Fernández, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa Ijumaa tarehe 28 Februari 2025 Majira ya Usiku, amewaongoza watu wa Mungu kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko ambaye kwa sasa anasumbuliwa na ugonjwa wa mkamba (Bronchitis) uliopelekea kulazwa tangu Ijumaa tarehe 14 Februari 2025 kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli iliyoko mjini Roma. Ibada hii imehudhuriwa na Makardinali wanaoishi mjini Roma, wafanyakazi wa Sekretarieti kuu ya Vatican pamoja na watu wa Mungu katika ujumla wao! Watu wa Mungu wametafakari mafumbo ya maisha na utume wa Kristo Yesu, kwa kujikita katika “Matendo ya Uchungu” ili kwa maombezi ya Bikira Maria, waamini wajionee uwepo angavu wa upendo wa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Ibada hii imeongozwa na “Sura ya Bikira Maria Mama wa Kanisa” ili kutafakari mafumbo ya Uchungu katika maisha na utume wa Kristo Yesu. Lengo la Sala hii ya Rozari Takatifu ni kumwombea Baba Mtakatifu ili aweze kupona haraka na hatimaye, kurejea tena kwenye maisha na utume wake. Huu ni mwendelezo wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, pamoja na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko, Ibada zinazofanywa sehemu mbalimbali za dunia.
Waamini wanakumbushwa kwamba, wao ni mahujaji wa matumaini na kwamba, Bikira Maria ni chemchemi ya matumaini. Waamini walikusanyika jioni hiyo kusali Rozari Takatifu sanjari na kutafakari mafumbo ya maisha na utume wa Kristo Yesu kwa macho ya Bikira Maria, Mama wa matumaini. Na habari zaidi kutoka kwa Dr Matteo Bruno, Msemaji mkuu wa Vatican zinaonesha kwamba, mapema Ijumaa tarehe 28 Februari 2025 aliendelea kutumia tiba mbadala ya mazoezi ya viungo vya kupumlia; ameshiriki katika Sala kwenye Kikanisa kilichopo Gemelli pamoja na kupokea Ekaristi Takatifu. Baadaye hali ya Baba Mtakatifu ilibadilika ghafla, akaanza kutapika na hivyo kupumua kwa shida. Jopo la madaktari ilimshughulikia kwa haraka kwa kumwezesha kuvuta hewa kwa kutumia mitambo, hali ikatulia na hivyo kuendelea kushirikiana na tiba kwa macho ang’avu. Lakini kwa ujumla hali yake bado ni tete sana. Taarifa kwa vyombo vya habari tarehe Mosi Machi 2025 zinaonesha kwamba, Baba Mtakatifu amepata usingizi mwanana na kwa sasa anaendelea na mapumziko.
Litania ya Bikira Maria Mama wa Mateso.
Bwana utuhurumie Bwana utuhurumie
Kristo utuhurumie Bwana utuhurumie
Bwana utuhurumie Bwana utuhurumie
Kristo utusikie – Kristo utusikilize
Mungu Baba wa Mbinguni, Utuhurumie
Mungu Mwana, Mkombozi wa dunia Utuhurumie
Mungu Roho Mtakatifu Utuhurumie
Utatu Mtakatifu Mungu MMoja Utuhurumie
Maria Mtakatifu Utuombee (iwe kiitikio)
Mama wa Mkombozi wetu,
Mama mwenye mateso,
Malkia wa mashahidi,
Mama wa wenye uchungu,
Mfariji wa wenye taabu,
Msaada wa wenye shida,
Mlinzi wa wenye upweke,
Nguvu ya dhaifu moyoni,
Makimbilio ya wakosefu,
Afya ya wagonjwa,
Matumaini ya wanaozimia,
Kwa ajili ya ufukara wako ulioona pangoni Bethlehemu, – Utusaidie ee Mama wa mateso (iwe kiitikio)
Kwa ajili ya mateso yako uliyoona katika uaguzi wa Simeoni,
Kwa ajili ya taabu zako ulizopata katika safari ya Misri,
Kwa uchungu wako, Mwanao alipopotea,
Kwa ajili ya huzuni yako Mwanao alipodhulumiwa,
Kwa ajili ya hofu yako Yesu alipokamatwa,
Kwa ajili ya uchungu wako ulipokutana na Yesu katika njia ya Msalaba,
Kwa ajili ya mateso ya Moyo wako aliposulibiwa,
Kwa ajili ya mateso yako makali Yesu alipokufa,
Kwa ajili ya kilio chako juu ya Mwanao mpenzi,
Kwa ajili ya uchungu wako penye kaburi la Mwanao,
Kwa ajili ya upweke wako baada ya maziko ya Mwanao,
Kwa ajili ya uvumilivu wako katika shida zote,
Katika uchungu wetu wote,
Katika ugonjwa na mateso,
Katika huzuni na shida,
Katika umaskini na upweke,
Katika mahangaiko na hatari,
Katika vishawisho vyote,
Katika saa ya kifo chetu,
Katika hukumu ya mwisho,
Mwanakondoo wa Mungu, unayeondoa dhambi za dunia, Utusamehe ee Bwana.
Mwanakondoo wa Mungu, unayeondoa dhambi za dunia, Utusikilize ee Bwana.
Mwanakondoo wa Mungu, unayeondoa dhambi za dunia, Utuhurumie.
Kristo utusikie – Kristo utusikilize
Bwana utuhurumie – Kristo utuhurumie
Bwana utuhurumie.
Baba Yetu ….
Utuombee, ee Mama wa Mateso
Tujaliwe kupewa ahadi za Kristo.
TUOMBE: Ee Bwana Yesu Kristo, utusaidie sasa na saa ya kifo chetu msaada wa Bikira Maria Mama yako, ambaye moyo wake mtakatifu ulichomwa na upanga wa mateso ulipoteswa na kufa msalabani. Unayeishi na kutawala milele na milele. Amina.