杏MAP导航

Tafuta

Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine alipokutana na kuzungumza na Papa Francisko tarehe 11 Oktoba 2024. Anamtakia heri, baraka na uponyaji wa haraka ili aendelee na maisha pamoja na utume wake. Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine alipokutana na kuzungumza na Papa Francisko tarehe 11 Oktoba 2024. Anamtakia heri, baraka na uponyaji wa haraka ili aendelee na maisha pamoja na utume wake.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Rais Volodymyr Zelenskyy Amemtakia Heri, Baraka Na Uponyaji wa Haraka Papa Francisko

Rais Volodymyr Zelenskyy amemtakia heri, baraka na uponyaji wa haraka Baba Mtakatifu Francisko ambaye kwa wakati huu amelazwa kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli iliyoko mjini Roma tangu Ijumaa tarehe 14 Februari 2025 na ameambiwa kwamba, hali yake inaendelea kuimarika siku hadi siku, ingawa bado itambidi kuendelea kubaki chini ya uangalizi wa madaktari. Vatican inaendelea kukazia mchakato wa haki, amani na maridhiano!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine, Ijumaa tarehe 14 Machi 2025 alifanya mazungumzo kwa njia ya simu na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, mazungumzo ambayo yamethibitishwa na Dr. Bruno Mattei, Msemaji mkuu wa Vatican, kama yalivyowekwa pia kwenye mitandao ya kijamii na Rais Volodymyr Zelenskyy. Katika mazungumzo haya, Rais Volodymyr Zelenskyy amemtakia heri, baraka na uponyaji wa haraka Baba Mtakatifu Francisko ambaye kwa wakati huu amelazwa kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli iliyoko mjini Roma tangu Ijumaa tarehe 14 Februari 2025 na ameambiwa kwamba, hali yake inaendelea kuimarika siku hadi siku, ingawa bado itambidi kuendelea kubaki chini ya uangalizi wa madaktari.

Afya ya Baba Mtakatifu Francisko inaendelea kuimarika kila siku
Afya ya Baba Mtakatifu Francisko inaendelea kuimarika kila siku   (ANSA)

Rais Volodymyr Zelenskyy anampongeza na kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa sala na mchango wake wa kiroho na kimaadili kwa watu wa Mungu nchini Ukraine, katika kipindi hiki kigumu cha maisha na historia yao katika ujumla sanjari na kuendelea kuhamasisha urejeshwaji wa watoto kutoka Ukraine waliotekwa nyara na kupelekwa Urusi. Hivi karibuni Vatican ilipata orodha ya majina ya wafungwa kutoka Ukraine, wanaoshikiliwa kwenye magereza nchini Urusi. Rais anaipongeza Vatican kwa kuendeleza majadiliano na uongozi wa Urusi, ili hatimaye, wafungwa hao wa kivita, waweze kuachiliwa huru, na wale wafungwa wa kivita kutoka Urusi, waweze pia kuachiwa huru.

Watu wa Mungu nchini Ukraine wanatamani amani ya kudumu
Watu wa Mungu nchini Ukraine wanatamani amani ya kudumu   (AFP or licensors)

Ni matumaini ya Rais Volodymyr Zelenskyy wa Ukraine kwamba, mpango mkakati wa kusitisha vita kati ya Urusi na Ukraine kwa muda wa siku thelathini ni muhimu sana kwani watu wa Mungu kutoka Ukraine wana kiu ya haki, amani na upatanisho wa kweli. Kumbe, mchango wa Vatican ni muhimu sana kuelekea kwenye amani ya kudumu. Kardinali Pietro Parolin, anasema, ni matumaini ya Vatican kuona kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inajikita kwenye majadiliano ya ukweli na uwazi, bila masharti, ili kuweza kupata amani ya kudumu nchini Ukraine.

Ukraine Mazungumzo
18 Machi 2025, 14:39