杏MAP导航

Tafuta

Kuzaliwa kutoka Juu: "Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu. Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee?” Yn 3:1-3. Kuzaliwa kutoka Juu: "Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu. Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee?” Yn 3:1-3.  

Papa Francisko: Katekesi Kuhusu Yesu Tumaini Letu: Nikodemo! Kuzaliwa Upya!

Baba Mtakatifu katika mzunguko huu mpya, anapenda kuonesha mikutano kati ya Kristo Yesu na watu mbalimbali ili kuwakirimia matumaini, kama ilivyokuwa kwa Nikodemo, mwenye historia ya pekee katika maisha yake, anayeonesha kwamba, kuna uwezekano mkubwa wa kutoka gizani na hatimaye, kupata ujasiri wa kumfuasa Kristo Yesu. Nikodemo alimwendea Kristo Yesu usiku, kadiri ya Mwinjili Yohane, hiki ni kielelezo cha giza, wasiwasi na mashaka katika maisha!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Kanisa wanasema, Mwana wa Mungu, katika hali ya kibinadamu aliyofungamana nayo, aliposhinda mauti kwa kifo chake na ufufuko wake, alimkomboa mwanadamu, akamgeuza kuwa kiumbe kipya (taz. Gal 6:15; 2Kor 5:17). Maana kwa kuwashirikisha Roho wake, anawafanya ndugu zake waitwao kutoka katika mataifa yote kuwa mwili wake katika fumbo. Ndani ya mwili huo uhai wa Kristo hutiwa katika waamini, ambao kwa njia ya Sakramenti wanaunganishwa, kwa jinsi ya siri na ya kweli, na Kristo Yesu aliyeteswa na kutukuzwa. Maana kwa ubatizo tumefananishwa na Kristo: “Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja” (1Kor 12:13). Katika ibada hii takatifu ushirikiano wetu na kifo cha Kristo Yesu na ufufuko wake huonyeshwa kwa ishara na kutekelezwa: “Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake”; na “kama tulivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika tutaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake” (Rum 6:4-5). Kwa kushiriki kweli mwili wa Bwana katika kumega mkate wa Ekaristi, twainuliwa hadi tuufikie ushirikiano naye na kati yetu, “Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja” (1Kor 10:17). Hivyo sisi sote tumekuwa viungo vya mwili ule (taz. 1Kor 12:27), “na sisi tu viungo, kila mmoja kwa mwenzake” (Rum 12:5). Rej. LG 7. Sakramenti ya Ubatizo ni mlango wa imani na msingi wa maisha yote ya Kikristo. Hili ni lango la kuingilia uzima katika Roho “Vitae spiritualis ianua”. Ni mlango unaomwezesha mwamini kuzipata Sakramenti nyingine zote. Kwa njia ya Ubatizo, mwamini anafanywa huru toka dhambi na kuzaliwa upya kama mtoto wa Mungu, anakuwa ni kiungo cha Kristo Yesu na kuingizwa katika Kanisa na hivyo kufanywa washiriki katika utume wake. Kimsingi Ubatizo ni Sakramenti ya kuzaliwa upya kwa maji katika Neno!

Mshumaa wa Pasaka ni kielelezo cha Kristo Mfufuka
Mshumaa wa Pasaka ni kielelezo cha Kristo Mfufuka   (Vatican Media)

Katekesi iliyoandaliwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 5 Machi 2025 ilikita mizizi yake katika: “Utoto wa Yesu.” Jinsi ambavyo Bikira Maria na Mtakatifu Yosefu walivyotaabika kumtafuta Mtoto Yesu hatimaye, wakamkuta akiwa ameketi katikati ya waalimu, wakimsikiliza na kumuuliza maswali. Huu ni mwaliko kwa waamini kutafakari hija ya Bikira Maria, ambayo kimsingi ilisheheni magumu na changamoto za maisha hadi pale aliposimama Mlimani Kalvari akashuhudia kifo cha Mwanaye mpendwa Kristo Yesu. Huu ni mwendelezo wa Katekesi kuhusu: “Roho Mtakatifu na Bibi Arusi. Roho Mtakatifu anawaongoza watu wa Mungu kuelekea kwa Yesu, tumaini letu” kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. “Basi palikuwa na mtu mmoja wa Mafarisayo, jina lake Nikodemo, mkuu wa Wayahudi. Huyo alimjia usiku, akamwambia, Rabi, twajua ya kuwa u mwalimu, umetoka kwa Mungu; kwa maana hakuna mtu awezaye kuzifanya ishara hizi uzifanyazo wewe, isipokuwa Mungu yu pamoja naye. Yesu akajibu, akamwambia, Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa mara ya pili, hawezi kuuona ufalme wa Mungu. Nikodemo akamwambia, Awezaje mtu kuzaliwa, akiwa mzee?” Yn 3:1-3. Hii ni sehemu ya Maandiko Matakatifu iliyoongoza Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano tarehe 19 Machi 2025 na kunogeshwa na kauli mbiu “Hamna budi kuzaliwa mara ya pili.”

Roho Mtakatifu anawaongoza watu kwa Kristo Yesu
Roho Mtakatifu anawaongoza watu kwa Kristo Yesu

Baba Mtakatifu katika mzunguko huu mpya, anapenda kuonesha mikutano kati ya Kristo Yesu na watu mbalimbali ili kuwakirimia matumaini, kama ilivyokuwa kwa Nikodemo, mwenye historia ya pekee katika maisha yake, anayeonesha kwamba, kuna uwezekano mkubwa wa kutoka gizani na hatimaye, kupata ujasiri wa kumfuasa Kristo Yesu. Nikodemo alimwendea Kristo Yesu usiku, kadiri ya Mwinjili Yohane, hiki ni kielelezo cha giza na mashaka katika maisha, kiasi cha kutokuona njia ya kufuata, ndiyo maana Nikodemo anajibidiisha kuutafuta mwanga wa maisha. Mwinjili Yohane anasema, “Kulikuwako Nuru halisi, amtiaye nuru kila mtu, akija katika ulimwengu.” Yn 1:9. Nikodemo alimtafuta Kristo Yesu, Mwanga wa Mataifa ili aweze kuliangazia giza la moyo wake, lakini hakuweza kuutambua mara moja mwanga huu kutoka kwa Kristo Yesu kama inavyojidhihirisha katika mahojiano yake na Yesu.Nikodemo alikuwa ni mtu mwenye utambulisho maalum na nafasi kubwa katika jamii, lakini alihisi kutaka kufanya mabadiliko katika maisha yake, bila kufahamu mahali pa kuanzia, bila kukubali kupokea mabadiliko katika maisha, mwamini anaishia kujifungia katika ubinafsi wake na hivyo kushindwa kupata mwelekeo mpya wa kupenda, yaani kwa kuzaliwa upya “anōthen (?νωθεν) kwa lugha ya Kigiriki kunaweza kumaanisha “Kuzaliwa upya au kuzaliwa kutoka juu.” Huu ni mwaliko kwa waamini kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kuwapatia maisha mapya, kwa kuzaliwa mara ya pili, ili kupyaisha tena maisha yaliyokuwa yanaanza kuzimika. Nikodemo kadiri ya maisha yake, anaonesha kwamba, kuna uwezekano wa kufanya mabadiliko katika maisha na kwa hakika huyu ni kati ya wanafunzi wa Kristo Yesu waliomwendea Pilato ili wakauzike mwili wake “Hata baada ya hayo Yusufu wa Arimathaya, naye ni mwanafunzi wa Yesu, lakini kwa siri, kwa hofu ya Wayahudi, alimwomba Pilato ruhusa ili auondoe mwili wake Yesu. Na Pilato akampya ruhusa. Basi akaenda akauondoa mwili wake. Akaenda Nikodemo naye, yule aliyemwendea usiku hapo kwanza, akaleta mchanganyiko wa manemane na uudi yapata ratli moja.” Yn 19: 38-39.

Nikodemo akagundua mwanga mpya na hivyo kuondokana na giza la maisha
Nikodemo akagundua mwanga mpya na hivyo kuondokana na giza la maisha

Hatimaye, Nikodemo akafanikiwa kuuona mwanga, akazaliwa tena mara ya pili na kuanza kutembea katika mwanga kwani hakuwa na haja tena ya kutembea gizani. Baba Mtakatifu Francisko anasema, wakati mwingine mageuzi ya maisha yanaleta mshtuko, yana mvuto na wakati mwingine ni sehemu ya tamaa ya mtu. Lakini yataka moyo ili kuweza kubadilika, kumbe, waamini hawana budi kumwomba Roho Mtakatifu ili awakirimie ujasiri wa kupambana na changamoto hizi na hatimaye, kuweza kuzishinda. Yesu anamtambua Nikodemo kuwa ni Mwalimu wa Israeli lakini kumbe haya mambo hakuyafahamu, hata Waisraeli waliogopa kutembea katika jangwa la maisha, kiasi kwamba, ilimbidi Musa kutengeneza nyoka wa shaba akaiweka juu ya mti; hata ikiwa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba akaishi. Rej. Hes 21: 4-9. Nyoka aliwakilisha hofu, woga na wasiwasi waliokuwa nao Waisraeli. Ikuweza kukombolewa kutokana na woga huu, iliwabidi kumwangalia nyoka wa shaba. Kama ilivyo kwa Nikodemo, hata waamini wanaalikwa kuuangalia Msalaba wa Kristo Yesu, aliyeshinda dhambi na kifo, chemchemi ya woga na wasiwasi wa mwanadamu. Waamini wamwangalie Kristo Yesu aliyetobolewa kwa mkuki ubavuni, ili kukutana naye, chemchemi ya matumaini tayari kukabiliana na mabadiliko katika maisha na hivyo kuzaliwa upya.  

Nikodemo

 

19 Machi 2025, 14:30