Papa Francisko: Majaribu ya Kristo Yesu Kwa Siku Arobaini Jangwani!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2025 unanogeshwa na kauli mbiu “Tutembee kwa pamoja katika matumaini.” Kwaresima ni kipindi cha imani na matumaini; toba na wongofu wa ndani, ili kukumbatia na kuambata huruma na upendo wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa mtu mmoja mmoja na kama Jumuiya ya waamini. Kwaresima ni kipindi cha kuimarisha na kuboresha imani, matumaini na mapendo kwa: kufunga na kusali; kwa kufanya toba na malipizi ya dhambi; kwa kushiriki kikamilifu katika Sakramenti za Kanisa; Kwa kusoma, kutafakari na hatimaye, kumwilisha Neno la Mungu katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo makini cha imani tendaji. Lengo ni kujitakasa na hatimaye, kuambata utakatifu wa maisha, ili kushiriki furaha ya Kristo Mfufuka wakati wa Sherehe ya Pasaka ya Bwana, huku waamini wakiwa wamepyaishwa kwa neema ya Roho Mtakatifu. Waamini watambue kwamba, wanaitwa kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao kwa watu wanaowazunguka na wale wote ambao Mwenyezi Mungu anawajalia fursa ya kukutana nao katika hija ya maisha yao, ili waweze kujaliwa mwanga na furaha ya Injili katika maisha. Mateso na kifo cha Kristo Yesu Msalabani, kiwe ni kikolezo cha toba na wongofu wa ndani kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa anayesema: “Lakini sikujulikana uso wangu na makanisa ya Uyahudi yaliyokuwa katika Kristo; ila wamesikia tu ya kwamba huyo aliyetuudhi hapo kwanza, sasa anaihubiri imani ile aliyoiharibu zamani. Wakamtukuza Mungu kwa ajili yangu.” Gal 1: 22-24. Waamini wajitahidi kuwa na kumbukumbu hai ya kukutana na Kristo Yesu katika maisha na utume wao. Ni wakati wa kuuvua utu wa kale na kuanza kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka.
Kipindi cha Kwaresima kinasimikwa katika nguzo kuu nne: yaani; Sala, Kufunga, Neno la Mungu na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha imani tendaji. Ibada ya Jumatano ya Majivu, inawaingiza Wakristo katika Kipindi cha Kwaresima, hija ya imani, matumaini na mapendo inayodumu kwa takribani siku arobaini, za toba na wongofu wa ndani. Ni wakati uliokubalika kwa waamini kumfungulia Mwenyezi Mungu na jirani zao, mioyo ya upendo na huruma. Binadamu kwa kupakwa majivu, anakumbushwa kwamba, yeye ni kiumbe cha Mungu aliyetolewa kutoka mavumbini na mavumbini atarudi tena! Hapa Mwenyezi Mungu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na pili ni kumheshimu binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Majivu ni alama inayomwingiza mwamini katika Fumbo kuu la huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake; kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Majivu ni alama ya unyenyekevu, mwanzo mpya na kwamba, hapa duniani mwanadamu ni msafiri na wala hana makazi ya kudumu! Kwaresima ni mwaliko kwa waamini kujikita katika toba na wongofu wa ndani; kujitakasa na kuendelea kupyaisha maisha yao ya kiroho; kama sehemu ya mchakato wa ukuaji katika fadhila ya mapendo, imani na matumaini.
Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Watu wa Kujitolea kuanzia tarehe 8 Machi na kufikia kilele chake Dominika tarehe 9 Machi 2025, Baba Mtakatifu Francisko amemteuwa Kardinali Michael Czerny, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu kuwa ni mwakilishi wake katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri aliyoyaandaa kwa ajili ya Ibada hii ya Misa Takatifu na kusomwa kwa niaba yake na Kardinali Michael Czerny, amekazia kuhusu majaribu ya Kristo Yesu Jangwani kwa muda wa Siku Arobaini, kwa kujikita katika sifa kuu tatu: Mwanzo, Namna na Matokeo, changamoto na mwaliko kwa waamini kujikita katika hija ya toba na wongofu wa ndani. Baba Mtakatifu Francisko anasema, hija ya maisha na utume wa Kristo Yesu inaanza kwa kujikita katika utii kwa kuongozwa na Roho Mtakatifu kwa muda wa siku arobaini nyikani. Jangwani mwanadamu anakabiliana na mapambano ya maisha ya kiroho na kimwili; anaonja uhitaji wa chakula na faraja ya Neno. Kristo Yesu, Mungu kweli na mtu kweli, aliona njaa na kujaribiwa na Shetani, Ibilisi. Hata waamini wanaonja majaribu katika hija ya maisha yao, lakini wakumbuke kwamba, Kristo Yesu yuko pamoja nao; ndiye anayewafugulia lango la jangwa na kuwakirimia nguvu ya kushinda vishawishi na hivyo, kuendelea kudumu katika safari ya maisha ya kiroho. Baba Mtakatifu anakaza kusema, mwanzoni kabisa majaribu ya Kristo Yesu ni ya makusudi, kielelezo makini cha uwajibikaji wake kwa Roho Mtakatifu na kwa Baba yake wa milele, ambaye kwa maongozi yake anajibu mara moja.
Katika majaribu, mwanadamu anateseka, kwani uovu hutangulia uhuru wake, uharibu na hivyo kuwa ni tishio la ndani la kudumu. Waamini wanapomwomba Mungu Baba Mwenyezi asiwaache majaribuni, Rej Mt 6:13 wakumbuke kwamba, Mwenyezi Mungu amekwisha kujibu maombi yao kupitia kwa Kristo Yesu, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili na kukaa kati yao daima. Mwenyezi Mungu yu karibu na waja wake daima na huwatunza hasa wakati wa majaribu na mashaka, pale Shetani, Ibilisi anapoinua sauti yake. Shetani, Ibilisi ni baba wa uwongo, Rej Yn 8:44, mwovu na mpotoshaji, kwa sababu analijua Neno la Mungu lakini halifahamu kwa undani wake na matokeo yake anaishia kulipotosha kama vile ilivyokuwa kwenye Agano la Kale kwa Adamu, Bustanini Eden, (Mwa 3:1-5) na kama anavyofanya sasa Jangwani dhidi ya Adamu mpya, yaani Kristo Yesu. Baba Mtakatifu anasema, majaribio ya Kristo Yesu yaliendeshwa mintarafu umoja, uhusiano na mafungamano yake na Baba yake wa milele. Shetani, Ibilisi ndiye anayetenganisha, anayesababisha migawanyiko na mipasuko, wakati Kristo Yesu anamuunganisha mwanadamu na Muumba wake na hivyo anakuwa ni mpatanishi. Katika upotovu wake, Shetani, Ibilisi anataka kuharibu kifungo hiki cha umoja na kumfanya Kristo Yesu kuwa na upendeleo wa pekee kabisa akisema: “Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, liambie jiwe hili liwe mkate, ... Nitakupa enzi hii yote na fahari... ukisujudu mbele yangu... Ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, jitupe chini...” Lk 4: 1-10.
Kristo Yesu katika majaribu haya yote aliibuka kidedea kwa kuonesha kwamba, kwa hakika alikuwa ni Mwana wa Mungu, akaongozwa na Roho Mtakatifu, kutangaza na kushuhudia uhusiano wake wa kimwana na Baba yake wa Milele, kwa kuonesha kwamba, Kristo Yesu alikuwa ni Mwana wa pekee wa Baba na kwamba, uhusiano na mafungamano haya ni kwa ajili ya kushiriki wokovu wa Ulimwengu na wala si hazina ya wivu (Rej Flp 2: 6), hali ya kujivunia, ili kupata mafanikio ya chapu chapu na hivyo kuwavuta wafuasi wengi. Baba Mtakatifu anawakumbusha waamini kwamba, hata wao wanajaribiwa mintarafu mahusiano na mafungamano yao na Mwenyezi Mungu, kwa kuonesha kwamba, kwa hakika Mwenyezi Mungu amewaacha; anataka kumwonesha jeuri yake na kwamba, Mwenyezi Mungu alikuwa yuko mbali nao na matokeo yake ni vita inayoendelea sehemu mbalimbali za dunia pamoja na watu kukata tamaa na kuvunjika moyo. Lakini Mwenyezi Mungu katika huruma na upendo wake, bado anamwendea na kuonesha ukaribu wake na mwanadamu, huku akiyamimina maisha yake kwa ajili ya ukombozi wa Ulimwengu.Kristo Yesu, Mwana wa Mungu aliye hai anashinda vishawishi, lakini, Shetani, Ibilisi akamwacha akaenda zake kwa muda na atarejea tena pale juu Msalabani, akiambiwa: “Ewe mwenye kulivunja hekalu na kulijenga kwa siku tatu, jiokoe nafsi yako; ukiwa ndiwe Mwana wa Mungu, shuka Msalabani.” Mt 27:40; Rej. Lk 23:25.
Ushindi mkamilifu wa Kristo Yesu unafumbatwa katika Fumbo la Pasaka, yaani: Mateso, Kifo na Ufufuko wa wafu, kiini cha imani ya Kanisa. Waamini wajitambue kwamba, wao ni wadhambi na wanaweza kuteleza na kuanguka wakati wowote, lakini Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo, ataweza kuwainua tena, kwa upendo, huruma na msamaha wake wa daima, kwani Kristo Yesu amekuja kuwakomboa watu kutoka katika lindi la dhambi na mauti na kwa njia ya imani, waamini wanakuwa kweli ni mahujaji wa matumaini.Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuanza kipindi cha Kwaresima, kwa kujiaminisha chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuwatakia heri na baraka watu wa kujitolea katika maadhimisho ya Jubilei yao, kwani kwa hakika, wao ni mfano bora wa kuigwa kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu kwa ajili ya huduma ya upendo kwa jirani zao. Hawa ni watu ambao wameendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa wasafiri, faraja kwa wagonjwa na maskini; huduma kwa wafungwa, vijana na wazee. Kwa hakika, anasema Baba Mtakatifu Francisko watu wa kujitolea ni mahujaji wa Injili ya Matumaini kwa watu waliovunjika na kupondeka moyo. Ni faraja kwa watu wanaotembea katika jangwa la umaskini na upweke hasi na kwa njia matendo na huduma zao, wanaweza kuanzisha Bustani ya ubinadamu mpya, ndoto ambayo Mwenyezi Mungu anaendelea kumwotea mwanadamu.