Papa Francisko Akutana na Kuzungumza na Kardinali Parolin
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Watu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia wanaendelea kumwombea Baba Mtakatifu Francisko ambaye kwa sasa anasumbuliwa na ugonjwa wa mkamba (Bronchitis) uliopelekea kulazwa tangu Ijumaa tarehe 14 Februari 2025 kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli iliyoko mjini Roma. Taarifa rasmi iliyotolewa na Dr Matteo Bruni, Msemaji mkuu wa Vatican inaeleza kwamba, Baba Mtakatifu Francisko Dominika tarehe 2 Machi 2025, alikutana na kuzungumza na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameambatana na Askofu mkuu Edgar Peña Parra, Katibu mkuu msaidizi wa Vatican. Baba Mtakatifu aliweza kupata kifungua kinywa, akajisomea magazeti na baadaye ameshiriki Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa Hospitalini hapo na kusali peke yake kwa takribani dakika ishirini kwenye Kikanisa kilichoko hospitalini hapo. Taarifa zaidi zinabainisha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko usiku wa kuamkia tarehe 3 Machi 2025 amelala usingizi mwanana na kwamba, anaendelea na tiba pamoja na mapumziko.
Kardinali Claudio Gugerotti, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Makanisa ya Mashariki, Jumamosi, tarehe Mosi, Machi 2025 usiku, amewaongoza watu wa Mungu kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko, kwa kutafakari mafumbo ya maisha na utume wa Kristo Yesu, mintarafu Matendo ya furaha huku macho yao yakiwa yanaelekezwa kwa Kristo Yesu. Waamini wamejikabidhi kwa ulinzi na tunza ya Bikira Maria “Mama wa Mungu na Kanisa” kwa ajili ya kumwombea afya njema, Baba Mtakatifu Francisko. Haya ni maombezi yanayoangaza njia ya waamini kama ishara ya faraja na chemchemi ya matumaini. Bikira Maria anamtembelea binadamu yake Elizabeti, tukio la kwanza kabisa kusimuliwa kwenye Maandiko Matakatifu.
Toka huko, baadaye atakwenda mjini Galilaya, na Bethlehemu, mahali atakapozaliwa Yesu, Mwana wa Mungu; Itawapasa kuokoa maisha ya Mtoto Yesu kutoka kwenye mkono katili wa Herode kwa kukimbilia Misri. Hizi ni safari ambazo zilihitaji ujasiri na uvumilivu mkubwa, kwani hata leo hii, Bikira Maria anatambua magumu na changamoto zinazowakabili wafuasi wa Kristo katika hija ya maisha yao huku bondeni kwenye machozi. Katika changamoto hizi, Bikira Maria anakuwa ni dada katika safari na mwenza, anayetoa mkono kuwasaidia wale wanaoelemewa na ugumu wa safari. Kama Mama, Bikira Maria anafahamu fika kwamba, upendo unamwilishwa katika mambo ya kawaida katika maisha. Ni Bikira Maria aliyethubutu kubadilisha Pango la kulishia wanyama, kuwa ni makazi ya Yesu, akamvika mtoto wake nguo za kimaskini, lakini akamwonesha wingi wa upendo! Kwa kumtafakari Bikira Maria, waamini wanaweza kuona nyuso za wanawake na wasichana wengi duniani! Hawa ni wanawake ambao kwa sadaka na majitoleo yao wanaweza kuandika historia ya maisha ya leo na kuanza kusuka ndoto ya kesho. Ni watu wanaojisadaka katika hali ya ukimya, uvumilivu na unyenyekevu mkuu, kiasi hata cha kuthubutu kujitwika mizigo mizito inayowaelemea watoto na familia zao katika ujumla wake. Hawa ni wanawake wanao amini kwa kutarajia yale yasioweza kutarajiwa.
Wakati huo huo, Dominika tarehe 2 Machi 2025, Kardinali Konrad Krajewski, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Upendo, amewaongoza waamini kusali Rozari Takatifu, kwa kutafakari mafumbo ya maisha ya Kristo Yesu kwa macho ya Bikira Maria, kwa ajili ya afya ya Baba Mtakatifu Francisko. Bikira Maria, Mama wa Kanisa, amsaidie wakati huu anapoendelea kukabiliana na changamoto ya afya. Lengo la Sala hii ya Rozari Takatifu ni kumwombea Baba Mtakatifu ili aweze kupona haraka na hatimaye, kurejea tena kwenye maisha na utume wake. Huu ni mwendelezo wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, pamoja na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko, Ibada zinazofanywa sehemu mbalimbali za dunia.