杏MAP导航

Tafuta

Papa Francisko akiwa katika kikanisa cha kibinafsi kwenye ghorofa ya 10 ya Hospitali ya Gemelli, Roma. Papa Francisko akiwa katika kikanisa cha kibinafsi kwenye ghorofa ya 10 ya Hospitali ya Gemelli, Roma.  (ANSA)

Papa Francisko aadhimisha Misa katika kikanisa cha kibinafsi cha Hospitali ya Gemelli

Ofisi ya Waandishi wa Habari ya Vatican imetoa picha ya Papa Francisko akiwa katika sala baada ya kuadhimisha Misa,siku ya Dominika asubuhi.Hii ni picha ya kwanza tangu kulazwa hospitalini tarehe 14 Februari.Hali ya kiafya ya Papa Francisko bado inaendelea vizuri na matibabu yake ya kupumua na mazoezi ya viungo yanaendelea.

Na Salvatore Cernuzio - Vatican.

Katika picha ya Papa Francisko iliyopigwa kutokea nyuma yake, anaonekana ameketi kwenye kiti cha magurudumu, amevaa casock na stola baada ya kuadhimisha Misa. Picha hiyo inamuonesha akitazama msalaba kwenye madhabahu ya kikanisa hicho kwenye ghorofa ya kumi ya hospitali ya Gemelli ambako amekuwa akienda kusali kila siku kwa kuwa hali yake ya kiafya imeonesha kuimarika kidogo. Hii ni picha ya kwanza ya Papa Francisko tangu alipolazwa katika Hospitali ya Gemelli,  Roma tarehe 14 Februari 2025. Ofisi ya Vyombo vya habari Vatican, ilisambaza picha hiyo Dominika jioni tarehe 16 Machi 2025.

Matumaini ya kumuona Papa

Kwa siku kadhaa sasa, waandishi wa habari na umma kwa ujumla walikuwa wakiomba picha ya Papa. Picha ya mwisho kuonekana ilikuja zaidi ya mwezi mmoja uliopita wakati katika makazi yake ya  Mtakatifu  Marta mjini Vatican, kabla ya kulazwa hospitalini Papa alipokea wanachama wa Mfuko wa Gaudium et Spes wa Hispania. Tangu wakati huo, hakuna mtu, mbali na madaktari wanaomtibu na washirika wake wa karibu aliyeweza kumuona Papa. Sauti yake ilisikika, hata hivyo, katika klipu ya sauti iliyochezwa tarehe 6 Machi 2025 wakati wa  sala ya Rozari katika Uwanja wa Mtakatifu Petro, ambapo aliwabariki waamini na kuwashukuru wale ambao wamemuombea wakati huu wa ugonjwa.

Watoto wa UNICEF

Leo asubuhi (Dominika 16 Machi) karibu watoto 200 kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto (UNICEF) na makundi mbalimbali kutoka Italia walikusanyika katika Uwanja mbele ya Hospitali ya Gemelli wakiwa wamebeba maua, maputo, na "kumbatio la ishara" kwa Papa. Walitazama juu kwenye madirisha ya orofa ya kumi ya hospitali ambapo Papa anapokea uangalizi wakitumaini kuona labda kumuona au salamu na baraka zinazowezekana.

Watoto 200 wakusanyika uwanja wa Gemelli kumsalimia Papa

Maombi, kupumzika, mazoezi ya viungo

Dominika jioni tarehe 16 Machi 2025, ishara mpya ya "uwepo" wa Papa Francisko ilifika wakati wa maombi yake. Sala ni sehemu ya utaratibu wake wa kila siku, pamoja na kupumzika na tiba: matibabu ya dawa, kupumua, na mazoezi ya viungo(physiotherapy,) ambayo yanaendelea. Kulingana na  taharifa za Ofisi ya Vyombo vya Habari Vatican, Papa amefaidika hasa na tiba ya viungo. Hakupokea wageni siku ya Dominika na aliendelea na shughuli fulani. Hali ya kiafya ya Papa bado ni thabiti, kama ilivyothibitishwa katika siku zilizopita, lakini bado ndani ya muktadha wa kiafya ambao wahudumu wa afya - kama ilivyoripotiwa katika taarifa za hivi karibuni - wanafafanua kuwa "tata." Taarifa za matibabu hazitolewi mara kwa mara, kwa kuzingatia hali ya afya ya Papa. Wakati huo huo, Ofisi ya Vyombo vya habari Vatican, inaendelea kuwasasisha wanahabari kila siku kuhusu afya ya Papa.

Waandishi wa Habari  wameongoezeka hadi 700 walioidhinishwa

Kwa sasa kuna waandishi wa habari 700 walioidhinishwa, idadi ambayo imeongezeka tangu Papa amelazwa hospitalini. Wakati huo huo, Papa anaendelea na shughuli zake za kila siku katika hospitali hiyo ambayo imekuwa makazi yake kwa zaidi ya mwezi mmoja. "Kipindi cha majaribu," kama alivyoandika katika tafakari yake ya Dominika ya Sala ya Malaika wa Bwana  tarehe 16 Machi 2025, ambapo ameunganisha sala zake na kaka na dada wengine wengi wagonjwa, "walio dhaifu, kwa wakati huu, kama mimi."

16 Machi 2025, 20:00