杏MAP导航

Tafuta

Papa Francisko anajibu barua ya aliyesalitiwa. Papa Francisko anajibu barua ya aliyesalitiwa.  (Vatican Media)

Papa amjibu Mke aliyesalitiwa:"Msamaha huleta nguvu kutoka katika neema ya Mungu!

Katika gazeti la kila mwezi "Piazza San Pietro,"kuna jibu la Papa Francisko kwa Catia,mwanamke ambaye aliuliza jinsi gani ya kusamehe usaliti wa mumewe."Msamaha ni tendo la bure,la kibinafsi,ambalo huchota nguvu kutoka katika roho,neema na upendo wa Mungu,"anaandika Papa katika barua iliyoandikwa kabla ya kulazwa hospitalini.

Vatican News

“Si rahisi kusamehe, hasa unaposalitiwa kwa upendo, kwa maneno, kwa uaminifu. Upendo katika ndoa lazima uimarishwe daima kwa kumwangalia Yesu, kwa Maria, kwa utenzi wa upendo wa Mtakatifu Paulo. Ikiwa kuna upendo, upendo unaweza kuwa na subira, kushona na kurekebisha.

Baba Mtakatifu Francisko anaandika haya katika kurasa za “Piazza San Pietro” yaani Uwanja wa Mtakatifu Petro, gazeti la kila mwezi linaloongozwa na Padre Enzo Fortunato(OFMConv) linalopembua mada za imani, kiroho na maisha ya kila siku. Papa, kama kila mwezi, anajibu mojawapo ya barua alizoandikiwa. Wakati huu ni barua ya mwanamke aliyesalitiwa na mumewe na ambaye anajiuliza ikiwa amsamehe, huku akiomba ishara ya kuelewa kuliko kusamehe "wasiosamehewa" ni jambo sahihi kulifanya.

Neema ya msamaha

Kabla ya kulazwa hospitalini, Papa alitilia maanani kesi ya Catia, ambaye anawakilisha hali ya wanandoa na familia nyingi za leo hii. "Kila historia, hata hivyo, daima ni maalum, tofauti, na ya kipekee. Msamaha ni tendo la bure, la kibinafsi, ambalo huchota nguvu kutoka katika roho, neema na upendo wa Mungu,” anaandika Papa ambaye anahimiza msamaha, akipendekeza njia iliyoainishwa vyema kuwa:"Katika utafutaji huu wa upendo wa kweli kwa uvumilivu, wema, ukarimu, usawa, Catia, unaweza kumwomba mume wako kuanza safari ya kusindikizana pamoja, kwa mfano baadhi ya mikutano na wanandoa Wakristo waliojitolea kusaidia wanandoa waliojeruhiwa, kubadilishana uzoefu wa maisha, shida, msamaha, upatanisho."

Michango mingine katika gazeti

Mbali na barua ya Papa, toleo la mwezi Machi la “Piazza San Pietro” kuna ripoti ya kina kuhusu Mkutano wa Kimataifa wa Haki za Watoto wenye kichwa: "Tuwapende na Kuwalinda," uliofanyika Vatican Februari 3, uliohudhuriwa na Papa Francisko na viongozi zaidi ya hamsini duniani. Kisha miaka kumi na miwili ya upapa wa Baba Mtakatifu ikiwa na picha za nyakati muhimu zaidi na chaguzi ambazo zilileta mapinduzi makubwa katika Kanisa. "Papa ambaye anaweka historia" ni jina la mchango wa mwandishi wa habari wa Marekani Norah O'Donnel, uso wa mtandao wa Habari wa CBS, kati ya waandishi waliofanya mahojiano na Papa. Na kisha ‘The Abraham wa karne ya 21’ na mtaalamu wa Vatican Piero Schiavazzi. Jarida hili pia linaandaa "Sauti za Wanawake", kwa Kanisa kuelekea usawa, pamoja na tafakari za Liliana Segre katika "Wajibu wa  kutobaki na sintofahamu." Hapakosekani maarifa ya kisanii na kiutamaduni katika Basilika ya Mtakatifu Petro na uzoefu wa mahujaji katika Mwaka huu wa Jubilei.

13 Machi 2025, 10:52