杏MAP导航

Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko akiwa na baadhi ya familia katika picha iliyopigwa tarehe 25 Novemba 2024. Baba Mtakatifu Francisko akiwa na baadhi ya familia katika picha iliyopigwa tarehe 25 Novemba 2024.  (Vatican Media)

Nia za Baba Mtakatifu Francisko Kwa Mwezi Machi 2025: Familia Zenye Migogoro

Papa Francisko katika nia zake za jumla kwa mwezi Machi 2025, anajikita zaidi katika migogoro inayozikumba familia mbalimbali. Kimsingi watu wengi wanatamani kuwa na familia bora na kamilifu, lakini kwa bahati mbaya hakuna familia kama hiyo kwani kila familia ina matatizo, changamoto na fursa mbalimbali za furaha. Ikumbukwe kwamba, kila mwanafamilia ni muhimu anazo karama na mapungufu yake ya kibinadamu na kwamba, kila mwanafamilia ni wa pekee sana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanazisaidia familia kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Upendo ndani ya familia” umegawanyika katika sura tisa zenye utangulizi mfupi, kwa kuonesha mchango mkubwa uliotolewa na Mababa wa Sinodi ya familia, mchango ambao unapaswa kutunzwa kama amana na hazina ya Kanisa. Baba Mtakatifu anakaza kusema, si majadiliano yote mintarafu Mafundisho tanzu ya Kanisa, maadili au shughuli za kichungaji yanapaswa kujadiliwa na Khalifa wa Mtakatifu Petro, bali mambo mengine yanahitaji kupatiwa ufumbuzi makini kadiri ya mila, tamaduni na changamoto mahalia. Hii inatokana na ukweli kwamba, mila na tamaduni za watu zinatofautiana, kumbe, hapa kuna haja ya kutamadunisha changamoto hizi ili ziweze kupatiwa ufumbuzi wa kudumu kadiri ya mwanga na tunu za kweli za Kiinjili. Wosia huu wa Kitume ni matunda ya mwanga wa Neno la Mungu unaozingatia ukweli na changamoto za maisha ya ndoa na familia katika ulimwengu mamboleo.

Familia ni Kanisa dogo la nyumbani. Picha ya tarehe 22 Aprili 2023
Familia ni Kanisa dogo la nyumbani. Picha ya tarehe 22 Aprili 2023   (Vatican Media)

Wosia huu wa Kitume unatoa mwelekeo wa Yesu katika kukuza tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, ili kuzijengea familia uwezo wa kutangaza na kushuhudia Injili ya familia. Ni waraka unaokazia upendo thabiti ndani ya familia; upendo unaogeuka na kuwa ni chemchemi na asili ya maisha. Baba Mtakatifu Francisko anatoa mapendekezo yanayopaswa kufanyiwa kazi katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji mintarafu utume wa maisha ya ndoa na familia. Anawataka wazazi na walezi kuimarisha elimu na makuzi ya watoto wao, ili waweze kuwajibika kikamilifu katika maisha yao. Ni wajibu wa Kanisa kuwasindikiza, kung’amua na kuwasaidia wanafamilia wanaolegalega katika maisha na wito wao. Baba Mtakatifu anachambua kwa kina na mapana tasaufi ya maisha ya ndoa na familia! Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni alikutana na kuzungumza na washiriki wa kozi maalum kuhusu: Utunzaji wa ndoa na huduma ya kichungaji kwa wanandoa waliojeruhiwa katika maisha na utume wao. Katika kozi hii, washiriki walipata nafasi ya kupembua kwa kina na mapana taalimungu ya maisha ya ndoa na familia; sheria, taratibu na kanuni za maisha ya ndoa na famlia sanjari na maisha ya Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Baba Mtakatifu anasema, mbele ya wanandoa wanaoteseka kutokana na madonda ya maisha ya ndoa na familia, Kanisa kama ilivyokuwa katika historia yake, halina budi kuonesha moyo wa upendo na mshikamano; kwa kuonja shida na magumu wanayokabiliana nayo, ili hatimaye, kuwawezesha kuzima kiu ya amani, utulivu na furaha ya kweli kama mtu binafsi na kama wanandoa katika ujumla wao. Mipasuko na majeraha ya maisha ya ndoa na familia ni matokeo ya sababu mbalimbali katika maisha kwa mfano haya ni masuala: kisaikolojia, kimwili, kimazingira na kitamaduni na wakati mwingine ni matokeo ya binadamu kujifungia katika uchoyo na ubinafsi wake na kushindwa kupokea zawadi ya upendo.

Watoto ni waathirika wakuu wa migogoro ya kifamilia
Watoto ni waathirika wakuu wa migogoro ya kifamilia

Katika muktadha huu unaowaonesha wanandoa wakichuruzika damu kutokana na madonda ya ndoa na familia, si rahisi kwa Kanisa kuweza kuwageuzia kisogo na kujifanya kana kwamba hakuna kinachoendelea. Mama Kanisa anapaswa kuonesha mshikamano wa dhati na wale wote wanaoteseka na kuomboleza kutokana na majeraha ya ndoa na familia zao. Katika mazingira kama haya, Kanisa litafute ukweli wa upendo wao kwa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za Kanisa, daima likitafuta mafao ya watu wa ndoa. Hii ni zawadi ambayo Mwenyezi Mungu anapenda kuwakirimia watoto wake. Katika ushuhuda wa kesi za watu wa ndoa zinazoendeshwa na Mama Kanisa, mashuhuda wanapaswa kwanza kabisa kujiaminisha chini ya ulinzi na maongozi ya Roho Mtakatifu, ili wasikilize kwa umakini sana, wapate vigezo muhimu, wafanye mang’amuzi na hatimaye, kutoa hukumu ya haki. Baba Mtakatifu anakiri kwamba, mchakato huu ni tete na wala si “maji kwa glasi.” Kanisa linapaswa kuwa makini ili kuwasaidia wanandoa kudumisha maisha yao ya ndoa mintarafu Mafundisho ya Kanisa kama ambavyo Mtakatifu Paulo anavyofafanua uhusiano kati ya Kristo Yesu na mchumba wake Kanisa, ambaye amejisadaka hata kufa kwa ajili yake pale Msalabani. Kwa njia hii, mapenzi ya Mungu kwa ajili ya familia nzima ya binadamu yakatendeka. Maisha ya ndoa na familia ndani ya Kanisa yanapaswa kuwa ni chemchemi ya furaha, imani na matumaini. Huu ni mwaliko wa kutembea kwa pamoja na Kanisa ndani ya Kanisa kwa kujikita na kuambata njia ya utakatifu wa maisha. Ndoa kadiri ya Agano Jipya ni safari ya imani. Kumbe, familia ya Kikristo inapata chimbuko lake katika maisha ya ndoa ambayo ni ushirikiano wa agano la upendo kati ya Kristo Yesu na Kanisa lake. Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika hija hii ya maisha ya kiroho kuna haja kuwa na wachungaji watakaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwasaidia wanandoa kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao.

Ndoa nyingi zinavunjika kutokana na mizengwe ya uhamisho kazini
Ndoa nyingi zinavunjika kutokana na mizengwe ya uhamisho kazini   (AFP or licensors)

Ndoa na familia ni utume unaobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ndoa; unapaswa kukita mizizi yake katika ari na mwamko wa kimisionari; ili kuwawezesha wanandoa kuwa wakarimu, tayari kupokea maisha mapya kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ili wanandoa waweze kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao, wanapaswa kupata maandalizi makini yanayogusa masuala ya kisaikolojia, upendo wa dhati, mahusiano na mafungamano yao katika maisha ya unyumba ili kuwasaidia kupata ukomavu na hatimaye, udumifu katika maisha yao. Wanandoa na familia wanapaswa kukuza na kudumisha ndani mwao wito wa ndoa, ili hatimaye, kusimama kidete, kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya Injili ya ndoa na familia katika mazingira ya kifamilia, maeneo ya kazi na katika jamii kwa ujumla wake. Wanandoa wanapaswa kutangaza na kushuhudua uzuri, utakatifu na ukuu wa maisha ya ndoa na familia kama kielelezo chenye mvuto na mashiko. Maisha ya ndoa na familia ni ushuhuda wa ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa mwanadamu. Mababa wa Mtaguso wa Pili wa Vatican wanabainisha umuhimu wa Neno la Mungu katika maisha ya ndoa na familia, kwa kuwa na mwelekeo, ari na mwamko wa kimisionari. Ni katika muktadha huu, wanandoa wanapaswa kujizatiti katika sala, kwa kushiriki kikamilifu maadhimisho ya Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Upatanisho; kwa kuendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa wenzi wao wa ndoa katika ukweli, uwazi na uaminifu, ili kweli familia yao iweze kuwa ni shule ya utakatifu, haki na amani; kitovu cha uinjilishaji, maadili na utu wema. Parokia hazina budi kuwasaidia wanandoa kuishi vyema wito na utume wao ndani ya Kanisa. Mchakato huu wa maisha na utume wa wanandoa ni tete lakini unawezekana kutekelezwa. Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime wakleri kujizatiti kuwasaidia, kuwaunga mkono na kuwasindikiza wanandoa ili kulisaidia Kanisa kupyaisha maisha na utume wake, kwa kujenga na kudumisha mtandao wa jumuiya na familia ambazo ni mashuhuda na wamisionari wa Injili ya familia.

Wanandoa wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya familia
Wanandoa wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya familia

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika nia zake za jumla kwa mwezi Machi 2025, anajikita zaidi katika migogoro inayozikumba familia mbalimbali. Kimsingi watu wengi wanatamani kuwa na familia bora na kamilifu, lakini kwa bahati mbaya hakuna familia bora na kamilifu, kwani kila familia ina matatizo, changamoto na fursa mbalimbali za furaha. Ikumbukwe kwamba, kila mwanafamilia ni muhimu anazo karama na mapungufu yake ya kibinadamu na kwamba, kila mwanafamilia ni wa pekee kabisa. Tofauti hizi zinaweza kuwa ni chanzo cha migogoro na madonda ya kifamilia. Dawa mchunguti ya uponyaji wa madonda haya ni msamaha wa kweli, maana yake, ni kumpatia mwenzi nafasi ya kutubu na kumwongokea Mungu ambaye ni mvumilivu, mwingi wa huruma na upendo, anayesamehe bila ya kuchoka. Huyu ni Mungu anayewasimamisha waja wake wanapoteleza na kuanguka, ili kuweza tena kupyaisha maisha yao katika matumaini. Hata pale matumaini yanapogonga mwamba, neema ya Mungu inawakirimia nguvu ya kusamehe na hivyo kuwakirimia amani ya ndani kwa kuwaondolea machungu moyoni na hasa zaidi chuki. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini na watu wenye mapenzi mema, kusali na kuziombea familia zenye matatizo na changamoto zaisha, watambue madonda yao kwa njia ya msamaha, kwa kugundua karama za wenzi wao wa ndoa bila kusahau tofauti zao msingi.

Nia za Papa Francisko
04 Machi 2025, 16:15