杏MAP导航

Tafuta

Padre Roberto Pasolini anasema, Imani ya Kanisa inasimikwa katika: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, chemchemi ya matumaini kwa waamini. Padre Roberto Pasolini anasema, Imani ya Kanisa inasimikwa katika: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, chemchemi ya matumaini kwa waamini.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Mafungo ya Sekretarieti Kuu ya Vatican: Tumaini la Maisha na Uzima wa Milele

Padre Roberto Pasolini anasema, Imani ya Kanisa inasimikwa katika: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu chemchemi ya matumaini, changamoto na mwaliko kwa waamini kugundua tunu na uzuri wa maisha ya uzima wa milele, hasa wakati huu, Mama Kanisa anapoadhimisha Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo na wakati huu, Papa Francisko anapokabiliana na changamoto ya afya. Kifo ni tokeo la dhambi na kwamba, utii wa Kristo Yesu uligeuza laana ya kifo kuwa baraka.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sekretarieti kuu ya Vatican kuanzia tarehe 9 hadi 14 Machi 2025 “inapanda kwenda jangwani” kwa ajili ya mafungo ya maisha ya kiroho, kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Pasaka ya Bwana, sanjari na Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo. Mafungo haya yanaongozwa na Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., mwenye umri wa miaka 53, Mtaalamu wa Sayansi ya Maandiko Matakatifu, ambaye, Mwezi Novemba 2024 aliteuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kuwa Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa. Kiini cha mafungo haya ni “Tumaini la Maisha na Uzima wa Milele” kama Mama Kanisa anavyofundisha na kuungama katika Kanuni ya Imani ya Nicea: “Nangojea na ufufuko wa wafu, na uzima wa milele ijayo. Amina.”  Padre Roberto Pasolini anasema, Imani ya Kanisa inasimikwa katika: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, chemchemi ya matumaini kwa waamini, changamoto na mwaliko kwa waamini kugundua tunu na uzuri wa maisha ya uzima wa milele, hasa wakati huu, Mama Kanisa anapoadhimisha Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo na wakati huu, Baba Mtakatifu Francisko anapokabiliana na changamoto ya afya. Kifo ni tokeo la dhambi na kwamba, utii wa Kristo Yesu uligeuza laana ya kifo kuwa baraka.

Imani ya Kanisa inasimikwa katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu
Imani ya Kanisa inasimikwa katika mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu

Katika kifo, Mwenyezi Mungu humwita mtu kwake na kwamba, kifo ni mwisho wa safari ya mwanadamu hapa duniani, ni wakati wa kupata neema ya huruma, ambayo Mwenyezi Mungu anampatia kuratibisha maisha yake ya duniani, mintarafu mpango wa Mungu kwa ajili ya kuamua hatima yake ya mwisho. Kristo Yesu kwa kifo chake ameshinda mauti, na hivyo kuwafungulia watu wote uwezekano wa wokovu. Kila mtu toka saa ya kufa kwake hupokea katika roho yake isiyokufa tuzo la milele katika hukumu ya pekee kuhusiana na maisha yake na Kristo Yesu au kwa kupitia: Utakaso, au kwa kuingia moja kwa moja katika heri ya mbingu au kulaaniwa moja kwa moja kwa milele. Jioni ya maisha ya mwanadamu atahukumiwa juu ya upendo, kama anavyokaza kusema, Mtakatifu Yohane wa Msalaba. Kwa mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu amewafungulia waja wake uzima wenye heri ambao umo katika utimilifu wa matunda ya ukombozi uliofanywa na Kristo Yesu aliyewaunganisha katika utukufu wake wa mbinguni wale waliomsadiki; na wale waliobaki na waaminifu kwa mapenzi yake.

Wajumbe wa Sekretarieti kuu ya Vatican wakihudhuria mafungo ya kiroho
Wajumbe wa Sekretarieti kuu ya Vatican wakihudhuria mafungo ya kiroho   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Mbingu ni jumuiya ya wenye heri, wote wale ambao wameingizwa kikamilifu ndani ya Kristo Yesu. Mama Kanisa huita “Purgatorio” au “Toharani” mahali pa utakaso. Jahanamu ni hali ya mtu kujitenga mwenyewe kabisa na ushirika pamoja na Mwenyezi Mungu pamoja na wenyeheri, hapa kuna moto usiozimika. Roho za wale wafao katika hali ya dhambi ya mauti hushuka mara moja baada ya kifo chao ndani ya Jahanum na huko wanapata teso kuu la kutengana na Mungu. Hukumu ya mwisho itafunua kwamba haki ya Mungu inashinda maonevu yote yaliyotendwa na viumbe vyake, na kwamba, upendo wake una nguvu kuliko mauti. Kumbe, waamini wana tumaini la mbingu mpya na dunia mpya. Uzima, halisi na kweli ni Baba wa milele ambaye kwa njia ya Mwanawe na katika Roho Mtakatifu, anamimina zawadi zake za mbinguni juu ya vitu vyote bila tofauti. Kwa huruma yake mwanadamu pia hupokea ahadi isyoondosheka ya uzima wa milele. Kadiri ya mafundisho ya Injili udhaifu mkubwa wa binadamu ni ukosefu wa upendo. Huu ni mwaliko kwa waamini kujenga na kudumisha upendo, umoja na mshikamano na Kristo Yesu, chemchemi ya matumaini ya waamini wake. Kifo ni sehemu ya mchakato unaomwezesha mwanadamu kugundua Uso wa huruma ya Mungu.

Kifo ni tokeo la dhambi
Kifo ni tokeo la dhambi   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., amegusia kuhusu hukumu ya mwisho na kwamba, kipimo ni matendo ya huruma, yaani upendo; Marafiki wa kweli wa Kristo Yesu ni wale waliojipambanua kwa huduma kwa maskini na kwamba, upendo umwilishwe katika huduma. Mwinjili Mathayo anaweka mbele ya macho ya waamini siku ile ya hukumu ya mwisho, Mataifa yote yatakapokusanyika mbele zake na hapo wale marafiki wa Mfalme watajipambanua kwa matendo yao ya huruma yaliyomwilishwa katika upendo unaojikita katika uhalisia wa maisha ya kila siku. Hili ndilo tumaini la mbingu mpya na dunia mpya. Rej. KKK 1042-1044. Upendo upewe kipaumbele cha kwanza. Kristo Yesu anasema, “Amin, amin, nawaambia, Yeye alisikiaye neno langu na kumwamini yeye aliyenipeleka yuna uzima wa milele; wala haingii hukumuni, bali amepita kutoka mautini kuingia uzimani.” Yn 5:24. Injili ya Kristo Yesu inatoa mwaliko wa kutambua kwamba, uzima wa milele umekwisha anza: unajidhihirisha katika jinsi watu wanavyoishi na kupendana na hivyo kuwafungulia uwepo wa Mungu unaobadilisha mambo; mshangao wa kweli wa hukumu ya mwisho utakuwa ni kugundua kwamba, Mwenyezi Mungu hakuwa na matazamio yoyote kwa binadamu, zaidi ya yale ya kututambua kikamilifu sisi kama watoto wake, tayari tumezama katika umilele wake.

Kwaresima ni kipindi cha toba, wongofu na utakatifu wa maisha
Kwaresima ni kipindi cha toba, wongofu na utakatifu wa maisha   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Waamini wanahimizwa kukuza tumaini lao la maisha na uzima wa milele, mara baada ya mtu wa kwanza kuanguka katika dhambi ya asili na huo ukawa ni mwanzo wa kifo. Mwanadamu badala ya kukaribisha maisha kama zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, akajaribu kuidhibiti na kwenda kinyume cha ukomo uliowekwa na Mwenyezi Mungu. Huo ukawa ni mwanzo wa “kifo cha ndani cha mwanadamu.” Hata hivyo Mwenyezi Mungu katika huruma na upendo wake, akaendelea kumtafuta mwanadamu. “BWANA Mungu akamwita Adamu, akamwambia, Uko wapi? Akasema, Nalisikia sauti yako bustanini, nikaogopa kwa kuwa mimi ni uchi; nikajificha.” Mwa 3:9. Katika nafasi ya kwanza, swali hili anaulizwa mtu aliyepotea, mtu ambaye yuko katika eneo lisilojulikana. Adamu baada ya anguko lake alitoka eneo la uwepo wa Mungu, akaenda nje, mbali na neema ya Mungu. Mwenyezi Mungu ndiye aliyekuwa wa kwanza kutaka kuanzisha tena mahusiano na mafungamano na Adamu aliyekuwa amepotea kutoka katika eneo la neema, akataka kurejesha tena mahusiano haya. Mungu ndiye anayechukua nafasi ya kwanza. Hii inaonesha kwamba kifo cha ndani si mwisho wa maisha na kwamba, hii inaweza kuwa ni hatua ya kwanza ya wokovu. Katika simulizi la Kaini na Abeli, Mwenyezi Mungu haingilii kati kuzuia mauaji bali anamlinda Kaini kutokana na hisia zake za hatia, fursa ya kugundua tena maisha na uzima wa milele, tayari kutubu na kumwongokea Mungu. Lk 13: 4-5. Mwenyezi Mungu anakiangalia kifo cha ndani kama fursa ya toba, wongofu wa ndani na mwanzo mpya wa maisha, tayari kuambata maisha na uzima wa milele, kwa uaminifu na uwazi wa Mwenyezi Mungu.

Maisha na uzima wa milele
10 Machi 2025, 15:29