Mafungo Sekretarieti Kuu ya Vatican: Pumziko, Maisha Na Uzima Wa Milele
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Sekretarieti kuu ya Vatican kuanzia Dominika jioni tarehe 9 hadi Ijumaa tarehe14 Machi 2025 “iko Mlimani” kwa ajili ya mafungo ya maisha ya kiroho, kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Pasaka ya Bwana, sanjari na Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo. Mafungo haya yanaongozwa na Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., Mtaalamu wa Sayansi ya Maandiko Matakatifu na Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa. Tema inayoongoza mafungo haya ni: “Tumaini la Maisha na Uzima wa Milele” kama Mama Kanisa anavyofundisha na kuungama katika Kanuni ya Imani ya Nicea: “Nangojea na ufufuko wa wafu, na uzima wa milele ijayo. Amina.” Padre Roberto Pasolini anasema, Imani ya Kanisa inasimikwa katika: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, chemchemi ya matumaini kwa waamini, changamoto na mwaliko kwa waamini kugundua tena na tena tunu na uzuri wa maisha ya uzima wa milele, hasa wakati huu, Mama Kanisa anapoadhimisha Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo na wakati huo huo, Baba Mtakatifu Francisko anapokabiliana na changamoto ya afya. Kifo ni tokeo la dhambi na kwamba, utii wa Kristo Yesu uligeuza laana ya kifo kuwa baraka. Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., katika tafakari yake, Alhamisi tarehe 13 Machi 2025 amekazia umuhimu wa kuishi zaidi, umuhimu wa maisha ya milele, jambo ambalo waamini wanapaswa kuliwekea malengo ya maisha. Baba Mtakatifu anasema, swali la kijana tajiri “nifanye nini nipate kuurithi uzima wa milele ni kielelezo cha maisha ya kiroho kinachofumbatwa katika dhana ya biashara na Mwenyezi Mungu. Kijana tajiri alitekeleza Amri za Mungu tangu ujana wake, ili aweze kupatiwa kile alichohitaji. Ni falsafa potofu ya kufanya na kupata matokeo yake na kusahau kwamba, maisha ya kiroho yanasimikwa katika uhuru na upendo wa kweli. Wokovu ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu na wala si haki ya mtu au bidhaa inayoweza kununuliwa sokoni!
Huu ni mwaliko kwa waamini kuondokana na imani inayokita mizizi yake katika biashara, kiasi hata cha kutaka kumdhibiti Mwenyezi Mungu na hivyo kusahau kwamba, Mwenyezi Mungu ni Baba mwenye huruma na mapendo!Mwinjili Marko anasema, Kristo Yesu alimkazia macho, akampenda, hii ni chemchemi ya kweli katika imani, mtazamo wa upendo unaopaswa kupokelewa. Huu ndio uzuri wa maisha ya Kikristo unaofumbatwa katika mtazamo wa Mungu, unaopyaisha tena imani. Huu ni mtazamo unaobubujika kutoka katika Ibada ya Kuabudu; msamaha kutoka katika Sakramenti ya upatanisho, amani na utulivu wa ndani kutoka kwa Kristo Yesu, chini ya Msalaba, ili kuweza kujiachilia kupendwa na Mwenyezi Mungu. Kristo Yesu anatoa mkazo akisema, “Umepungukiwa na neno moja. Enenda ukauze ulivyo navyo vyote, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni.” Mk 10:21 Hiki ni kielelezo cha zawadi na sadaka, mwaliko kutoka kwa Kristo Yesu, kufanya yale yanayowezekana. Katika Injili Kristo Yesu anakazia umuhimu wa sadaka kwa kukumbushia kuhusu Amri za Mungu na mwishoni anampatia wazo la mwisho, auze vyote kisha amfuate! Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., anasema, ilikuwa ni vigumu sana kwa kijana kujitenga na utajiri wake, ndiyo maana akaondoka kwa huzuni kwani alikuwa na mali nyingi. Mtume Petro akamuuliza Kristo Yesu, tazama sisi tumeacha yote na kuitikia wito wa kukufuata tutapata nini? Yesu akajibu kwamba, watapata uzima wa milele. Rej. Mk 10: 28-32. Hapa jambo la msingi ni kwa wafuasi wa Kristo Yesu kujikabidhi kwa Yesu. Si rahisi sana kwa mwanadamu kujitenga na umiliki wa mali, lakini kuna mifano hai ya waamini waliothubutu kuishi kikamifu maisha ya uzima wa milele kama ilivyokuwa kwa mfano wa Chiara Corbella Petrillo ambaye alikabili mateso na mahangaiko ya ugonjwa wake kwa uaminifu bila ya kukata tamaa, akaishi kwa bidii katika kweli na haki.
Kristo Yesu katika Injili ya Yohane anatangaza kwamba, Yeye ndiye mchungaji mwema na kwamba, bado anaendelea kujitaabisha kuwatafuta kondoo wake waliopotea na kutokomea kwenye majangwa ya dunia. Kwa njia ya alama ya mateso na madonda yake yenye huruma anawavuta waja wake kwenye njia na maisha yake; anawabeba mabegani mwake wale wote waliokandamizwa na ubaya wa dhambi katika mifumo yake mbalimbali. Kristo Mfufuka anaendelea kuwatafuta wale wote waliomezwa katika upweke hasi; wanaotengwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii; anakutana na wote hawa kwa njia ya jirani zao wanaowakaribia kwa heshima, wema na huruma, ili kuwawezesha watu hawa kuisikia sauti ya Kristo ambayo kamwe haiwezi kusahaulika kwani ni mwaliko wa kujenga urafiki na Mwenyezi Mungu. Rej. Yn 10:11-15. Yesu anaendelea kubeba mzigo wa wahanga wa utumwa wa kale na ule mamboleo; kazi za suluba zisizo na staha kwa heshima na utu wa binadamu; biashara haramu ya binadamu na silaha; unyonyaji na uhalifu; matumizi haramu ya dawa za kulevya na ulevi wa kupindukia. Yesu anajitwika mzigo wa watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi; watoto wanaonyanyaswa na kupokwa utu, heshima na haki zao msingi; Yesu anajitwika mzigo wa watu waliojeruhiwa moyoni mwao kutokana na ubaya unaotendeka katika kuta za nyumba zao wenyewe!
Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., anasema, Kristo Yesu anawaalika wafuasi wake kujisadaka bila ya kujibakiza, kwa kuondoa hofu katika maisha kama inavyojidhihirisha kwa ishara ya kuzidisha mikate, kwani kile kinachoonekana kutokutosheleza kinaongezeka maradufu mikononi mwa Kristo Yesu. Ule umati ukashikwa na shauku ya kutafuta zaidi mkate wa kushibisha njaa ya miili yao, bila kufahamu kwamba, ishara ile ililenga njaa ya maisha ya kiroho inayoshibishwa kwa Ekaristi Takatifu. Waamini waelimishwe katika Neno la Mungu; walishwe katika karamu ya Mwili na Damu ya Bwana; wamtolee Mungu shukrani; wakitolea hostia isiyo na doa, siyo kwa mikono ya Padre tu, bali pia pamoja naye, wajifunze kujitolea wenyewe. Tena, siku kwa siku, kwa njia ya Kristo mshenga, wakamilishwe katika umoja na Mungu na kati yao ili hatimaye, Mungu awe yote katika wote. Rej. SC. 47-49. Ekaristi Takatifu ni Sakramenti ya Mwili na Damu yake Azizi inayotolewa kwa ajili ya kurutubisha maisha ya walimwengu. Kwa kumpokea Kristo Yesu kwa imani, mwamini anakuwa sawa na Yesu na hivyo kufanyika kuwa mwana katika Mwana. Kwa njia ya Ekaristi Takatifu, Kristo Yesu anaandamana na wafuasi wake kama ilivyokuwa kwa wale Wafuasi wa Emau! Anasafiri na waja wake katika historia ili kuwakirimia imani, matumaini na mapendo; kwa kuwafariji wakati wa majaribu na magumu ya maisha. Ibada ya Ekaristi Takatifu inawaunganisha waamini na Kristo Yesu. Mwinjili Yohane, katika simulizi lake, anakita zaidi ujumbe wake katika huduma ya upendo na kwamba, Ibada ya kweli inasimikwa katika huduma. Kristo Yesu amejinyenyekesha kiasi hata cha kujifanya kuwa mtumwa wa wote, ili kuwakomboa wote wanaogelea katika utumwa wa dhambi na mauti! Kristo Yesu anampenda kila mtu jinsi alivyo!
Baada ya kuwaosha Mitume wake miguu, Yesu aliweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu kwa kuwapatia wafuasi wake: Mkate kuwa ni kielelezo cha mwili wake na Divai, kielelezo cha Damu yake azizi. Hivi ndivyo upendo wa Mungu unavyojidhihirisha katika maisha ya wafuasi wake kwa kuhudumiana. Maisha ya milele ni ukweli unaowafikia waamini katika maisha yao kwa kujifunza kutoa kwa ujasiri hata kile kidogo walicho nacho. Machoni pa Mwenyezi Mungu, kila ishara ya upendo ina thamani isiyokuwa na kikomo na kwamba, kila kitu kinaweza kuwa ni cha milele.Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., anasema, Sala ya kuwaombea wafu: “Raha ya milele uwape, ee Bwana, na mwanga wa milele uwaangazie. Wapumzike kwa amani. Amina” imezoeleka na kwamba, hapa Kanisa linaonesha umuhimu wa mapumziko, kama kielelezo cha utimilifu wa maisha ya mwanadamu kadiri ya Maandiko Matakatifu. Mwenyezi Mungu alijipumzisha na Kristo Yesu alipotundikwa Msalabani na hatimaye, akazikwa kaburini, changamoto na mwaliko kwa waamini kukumbatia muda kwa ujasiri “bila kupelekwa puta.” Hapa changamoto kwa jamii ni kujiwekea muda wa mapaumziko, kwa mwanadamu kukubali na kupokea mipaka katika maisha yake, ili kujitafutia muda kwa ajili ya mapumziko katika utulivu na amani. Pumziko la kweli linajikita katika uhuru wa ndani, ili kuweza kukumbatiwa na upendo wa Mungu. Hii ni amani na utulivu wa ndani, unaomwezesha mwamini kusema: “Kwa maana yeye aliyeingia katika raha yake amestarehe mwenyewe katika kazi yake, kama vile Mungu alivyostarehe katika kazi zake.” Ebr 4:10. Mapumziko na mwanadamu kuishi vyema ni sehemu ya mchakato wa maisha ya uzima wa milele. Huu ni mwaliko wa kuishi bila woga na kuendelea kuamini kwamba, Mwenyezi Mungu anatenda kazi ndani ya waja wake. Mapumziko ya kweli ni amani ya ndani, ni njia ya kuishi kwa bidii zaidi bila hofu, wasiwasi wala woga. Hiki ni kielelezo cha imani hai inayowafanya waamini kuwa huru kupenda. “Katika pendo hamna hofu; lakini pendo lililo kamili huitupa nje hofu, kwa maana hofu ina adhabu; na mwenye hofu hakukamilishwa katika pendo.” 1Yn 4:18. Kumbe, maisha ya uzima wa milele sio lengo ambalo liko mbali na mwanadamu, lakini ni ukweli ambao tayari unakua ndani ya waamini na kwamba, tayari wanaendelea kuuishi.