杏MAP导航

Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea vyema na tiba, sala, mazoezi na mapumziko. Anafuatilia mafungo ya kiroho kwa Sakretarieti kuu ya Vatican kwa njia ya video. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea vyema na tiba, sala, mazoezi na mapumziko. Anafuatilia mafungo ya kiroho kwa Sakretarieti kuu ya Vatican kwa njia ya video.  (ANSA)

Mafungo Sekretarieti Kuu ya Vatican: "Mauti ya Pili"

Maboresho ya afya yamemletea nafuu Baba Mtakatifu kiasi cha kufuatilia mahubiri ya Padre Pasolini, kwa njia ya video kuanzia Dominika Jioni tarehe 9 Machi 2025. Na kwa njia hii, Baba Mtakatifu anaendelea kuungana kiroho na wajumbe wa Sekretarieti kuu ya Vatican katika mafungo haya. Papa amepokea Ekaristi Takatifu, akasali na hatimaye, akaendelea na mapumziko yake. Jumanne, tarehe 11 Machi 2025 amepata usingizi mwanana na kuamka saa 2: 00 Asubuhi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sekretarieti kuu ya Vatican kuanzia tarehe 9 hadi 14 Machi 2025 “inapanda kwenda jangwani” kwa ajili ya mafungo ya maisha ya kiroho, kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Pasaka ya Bwana, sanjari na Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo. Mafungo haya yanaongozwa na Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa. Kiini cha mafungo haya ni “Tumaini la Maisha na Uzima wa Milele” kama Mama Kanisa anavyofundisha na kuungama katika Kanuni ya Imani ya Nicea: “Nangojea na ufufuko wa wafu, na uzima wa milele ijayo. Amina.”  Padre Roberto Pasolini anasema, Imani ya Kanisa inasimikwa katika: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, chemchemi ya matumaini kwa waamini, changamoto na mwaliko kwa waamini kugundua tunu na uzuri wa maisha ya uzima wa milele, hasa wakati huu, Mama Kanisa anapoadhimisha Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo na  Baba Mtakatifu Francisko anapokabiliana na changamoto ya afya. Taarifa rasmi iliyotolewa na Dr. Matteo Bruno, Msemaji mkuu wa Vatican inaonesha kwamba, hali ya afya ya Baba Mtakatifu Francisko inaendelea kuimarika na kwamba, anaendelea vyema na tiba yake. Maboresho haya ya afya yamemletea nafuu Baba Mtakatifu kiasi cha kufuatilia mahubiri ya Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., kwa njia ya video kuanzia Dominika Jioni tarehe 9 Machi 2025. Na kwa njia hii, Baba Mtakatifu anaendelea kuungana kiroho na wajumbe wa Sekretarieti kuu ya Vatican katika mafungo haya. Baba Mtakatifu amepokea Ekaristi Takatifu, akaenda kwenye Kikanisa kusali na hatimaye, akaendelea na mapumziko yake. Jumanne, tarehe 11 Machi 2025 amepata usingizi mwanana na kuamka saa 2: 00 Asubuhi kwa saa za Ulaya. Bado umati mkubwa wa waamini unaendelea kumwombea Baba Mtakatifu Francisko kwa njia ya Rozari Takatifu, kutoka katika Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican.

Tumaini la maisha ya uzima wa milele
Tumaini la maisha ya uzima wa milele   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., katika tafakari yake, Jumanne, tarehe 11 Machi 2025, amekita mawazo yake kuhusu “Mauti ya Pili.” Maandiko Matakatifu yanasimulia historia ya maisha ya wanadamu inayosimikwa kati mvutano mkubwa kati ya ahadi ya maisha na uzima wa milele pamoja na ukweli wa kifo. Israeli katika uaminifu na kukengeuka kwake, ameendelea daima kuitafuta nchi ya ahadi. Mtakatifu Paulo, Mtume anasema: “kama wasiojulikana, bali wajulikanao sana; kama wanaokufa, kumbe tu hai; kama wanaorudiwa, bali wasiouawa.” (2Kor 6:9), akionesha kitendawili cha uwapo! Ezekieli ni miongoni mwa Manabii katika Agano la Kale anayeonesha hali hii katika maono ya bonde la mifupa mikavu. Rej Eze 37. Israeli alionekana kama kaburi lililo wazi, lisilo na uhai wala matumaini. Mwenyezi Mungu amamwamuru Nabii azungumze na mifupa, ambayo inarudi na kuchukua nyama, lakini inabaki bila uhai mpaka Roho yake ipumue juu yake, kielelezo cha Israeli kurejea tena kutoka uhamishoni, lakini inaonesha hali halisi ya binadamu, ambaye mara nyingi anaishi bila ukweli. Mifupa iliyokaushwa inaashiria “Kifo cha kwanza” cha ndani ya mwanadamu, ambacho kinadhihirishwa kwa: hofu, hali ya kutojali sanjari na binadamu kupoteza matumaini. Hivi ndivyo ilivyotokea kwa Adamu na Hawa baada ya kuanguka dhambini; mwili wao ulikuwa hai, lakini umetengwa na uwepo wa Mungu. Roho wa Mungu pekee ndiye anayeweza kurejesha uzima wa kweli. Walakini, pia kuna "Kifo cha pili," ambacho mara nyingi hueleweka kama laana ya milele, lakini ambayo inaweza pia kuonekana kama kifo cha kibaolojia. Wale ambao tayari wameshinda kifo cha kwanza - yaani, hofu, ubinafsi na udanganyifu wa uthabiti wanakabiliwa na kifo cha pili bila hofu.

Padre Roberto Pasolini: Mauti ya Pili
Padre Roberto Pasolini: Mauti ya Pili

Mtakatifu Francisko wa Assisi anaeleza hayo katika Utenzi wake wa “Ndugu jua” akiwasifu wale wanaokikaribisha kifo katika Mungu Mwenyezi. Mwinjili Yohane katika Kitabu cha Ufunuo anasema: “Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa. Yeye ashindaye hatapatikana na madhara ya mauti ya pili.” Ufu 2:11. Watu wanaoishi kwa imani na matumaini thabiti wanaweza kupitia hali hiyo bila ya kupondwa nayo. Maono ya Nabii Ezekieli yanafundisha kwamba, ufufuo na uzima wa milele unaanza sasa, ikiwa kama waamini watakaribisha Roho wake. Jambo la msingi kwa waamini ni kujiuliza, Je, wanataka kubaki mifupa mikavu au wanajiruhusu kuhuishwa na maisha halisi? Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., anaendelea kusema, changamoto hali ya hija ya maisha ya binadamu sio tu kupitia Fumbo la kifo, lakini ni kutambua kwamba uzima wa milele tayari unaanzia hapa. Mwanadamu daima anajidanganya kwamba, kuna aina mbili tu za watu: walio hai na wafu. Injili ya Yohane pamoja na ufufuo wa Lazaro unapinga maono haya, kwani wafu wa kweli si tu wale ambao wamekata pumzi, bali hata wale ambao wamemezwa na hofu pamoja na aibu. Lazaro aliyekuwa kaburini amefungwa sanda anawawakilisha wale wote wanao jiruhusu kutawalia pamoja na kuwa na mifumo migumu, kiasi cha kupoteza mawasiliano na uhuru wao wa ndani.  Martha na Mariamu, walikabiliwa na kifo cha ndugu yao, wanaonesha imani yenye masharti: “Kama ungalikuwa hapa, ndugu yangu hangalikufa” (Yn 11:21). Mtazamo huu unaonesha wazo la Mwenyezi Mungu ambaye anapaswa kuingilia kati kila wakati ili kuwaepusha watu kupata maumivu. Lakini  Kristo Yesu hakuja kuondoa mateso, bali kuyabadilisha na kuyapatia maana mpya: “Mimi ndimi huo ufufuo na uzima” (Yn 11:25). Kwa hiyo, swali la kweli si iwapo binadamu atakufa, bali ikiwa kama binadamu tayari anaishi ukweli huu, akiendelea kumtumainia Kristo Yesu na Neno lake.

Mafungo ya kiroho kwa Sekretarieti kuu ya Vatican
Mafungo ya kiroho kwa Sekretarieti kuu ya Vatican   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., anakaza kusema, changamoto hii pia inajitokeza katika tukio la mwanamke mwenye kuvuja damu, mwanamke ambaye amekuwa mgonjwa kwa muda wa miaka kumi na miwili ambaye, licha ya kila kitu, anathubutu kugusa vazi la Kristo Yesu kutafuta uponyaji (Mk 5:25-34). Hali yake inawakilisha ubinadamu wote: binadamu anayetafuta tiba na uzima, lakini mara nyingi, mwanadamu anategemea sanamu za uongo, ambazo humwachana mtu tupu pasi na kitu. Kristo Yesu ndiye mponyaji wa kweli, changamoto na mwaliko kwa waamini kujenga mahusiano na mafungamano ya dhati na Kristo Yesu, ili awakirimie uponyaji wa ndani na hivyo kuwajalia uwezo wa kuamini na kujisikia kupendwa na kukaribishwa. Kristo Yesu anamwambia hivi: “Binti, imani yako imekuokoa” (Mk 5:34), akionesha kwamba wokovu si mwingilio wa nje wa Mungu, bali unaoneshwa katika uwezo wa kujifungua kwa kuwapo kwake. Vivyo hivyo kwa kuungama na kwa kila uzoefu wa upatanisho: tendo rasmi halitoshi, mioyo ya mwanadamu inahitaji kugundua tena imani katika Mungu ambaye anamkirimia mwanadamu uhai. Ishara ya Lazaro na uponyaji wa mwanamke mwenye kutokwa na damu hutuuliza swali ngumu: Je, tunakufa na kusubiri mwisho au kuishi maisha ambao tayari wameanza kupata ufufuo? Uzima wa milele sio tu thawabu ya baadaye, lakini ni ukweli ambao mwanadamu anaweza kuuchagua kuanzia sasa, kuendelea kuishi kwa uhuru, tumaini pamoja na  kuchagua kuanzia sasa, kuishi kwa uhuru, tumaini na kumwamini Mungu anayemwita mwanadamu katika utimilifu wake.

Tafakari Kuhusu Kifo
11 Machi 2025, 15:29