Mafungo ya Sekretarieti Kuu ya Vatican: Mabadiliko Katika Maisha
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Maandiko Matakatifu yanamweka Kristo Yesu kuwa ni njia, ukweli na uzima. Ndiye mchungaji mwema anayewaongoza waja wake kwa mfano bora wa maisha, unyenyekevu, upendo na sadaka iliyofikia kilele chake pale juu Msalabani anapoinamisha kichwa na kutoa roho, kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti! Yesu katika maisha yake alijitosa kuhakikisha kwamba, watu wa Mungu wanapata huduma yao: kiroho na kimwili. Kwa kuwaondolea dhambi zao, kuwaponya magonjwa kwa kuwalisha na kuwanywesha wakati wa njaa na kiu! Kwa miaka mitatu aliwafundisha Mitume wake tunu msingi za Kiinjili zinazofumbatwa katika Heri za Mlimani na Sala ya Baba Yetu. Akawarekebisha pale walipokosea njia na kutopea katika uchoyo na ubinafsi. Akajitahidi kuwalinda na kuwaelekeza katika ukweli, haki na upendo. Akayafunga madonda na majeraha yao kwa imani, matumaini na mapendo, kiasi cha kuwanyanyua wale waliopondeka na kuvunjika moyo, kiasi cha kujikatia tamaa, ili kuanza hija mpya ya maisha. “Jangwa” au "Upweke mtakatifu" ni muhimu sana katika maisha na utume wa waamini ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake. Ni baada ya Yesu kubatizwa na Roho kutua kama njiwa juu yake. Roho huyo huyo aliyetua juu ya Yesu, anamtoa Kristo Yesu na kumpeleka jangwani. Huko anakaa siku 40 akijaribiwa na Shetani, Ibilisi. Hizi ni alama zenye maana kubwa sana katika utume wa Yesu. Baba Mtakatifu Francisko anasema jangwa ni mahali ambapo Mwenyezi Mungu anazungumza kutoka katika undani wa mtu mwenyewe, yaani dhamiri nyofu. Hii ni chemchemi ya majibu ya Mungu katika sala. Ni mahali pa majaribu na kishwawishi kikubwa! Kumbe, jangwa, katika Biblia, ni mahala ambapo mtu anajitambua “ni nani” mbele ya watu na mbele ya Mwenyezi Mungu.
Kwa kuzingatia historia ya Waisraeli waliosafiri jangwani kwa kipindi cha miaka 40 kuelekea nchi ya ahadi, jangwa lilikuwa ni mahala pa kujaribiwa uaminifu, mahala pa kutakaswa na mahala pia pa kuonja wema, upendo, ukarimu na huruma ya Mungu. Wakiwa jangwani Mungu aliwaonesha upendo wake mkuu kwa kuwalinda, kuwaongoza na kuwapatia mahitaji yao msingi. Kwaresima ni hija ya maisha ya kiroho inayofumbatwa kwa namna ya pekee katika toba na wongofu wa ndani ili kufanana zaidi na Mwenyezi Mungu; Kwa kusali na kufunga; kwa kuishi kikamilifu Sakramenti za Kanisa; kwa kusoma, kutafakari na kumwilisha tunu za Injili katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili! Ni katika muktadha huu, Sekretarieti kuu ya Vatican kuanzia tarehe 9 hadi 14 Machi 2025 “imepanda kwenda Mlimani” kwa ajili ya mafungo ya maisha ya kiroho, kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Pasaka ya Bwana, sanjari na Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo. Katika maadhimisho ya kumbukizi ya miaka 12 tangu Baba Mtakatifu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki tarehe 13 Machi 2013, Baba Mtakatifu amepokea salam na matashi mema kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Ameendelea na tiba, sala na tafakari, kwa kushiriki kwa njia ya video mafungo ya maisha ya kiroho yaliyokuwa yanatolewa kwa Sekretarieti kuu ya Vatican. Taarifa rasmi iliyotolewa na Dr Matteo Bruno, Msemaji mkuu wa Vatican zinaonesha kwamba Baba Mtakatifu Francisko usiku wa kuamkia Ijumaa tarehe 14 Machi 2025 amepata usingizi mnono na kwamba, amefuatilia tafakari ya kufunga mafungo kwa Sekretarieti ku ya Vatican kwa njia ya video.
Itakumbukwa kwamba, Mafungo ya maisha ya kiroho kwa ajili ya Sekretarieti kuu ya Vatican yameongozwa na Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., Mtaalamu wa Sayansi ya Maandiko Matakatifu na Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa. Kiini cha mafungo haya ni “Tumaini la Maisha na Uzima wa Milele” kama Mama Kanisa anavyofundisha na kukiri katika Kanuni ya Imani ya Nicea: “Nangojea na ufufuko wa wafu, na uzima wa milele ijayo. Amina.” Padre Roberto Pasolini anasema, Imani ya Kanisa inasimikwa katika: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, chemchemi ya matumaini kwa waamini, changamoto na mwaliko kwa waamini kugundua tunu na uzuri wa maisha ya uzima wa milele, hasa wakati huu, Mama Kanisa anapoadhimisha Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo! Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., katika tafakari yake iliyokunja jamvi la safari ya jangwani kwa Baba Mtakatifu Francisko pamoja na wasaidizi wake, Ijumaa tarehe 14 Machi 2025 ametoa mwaliko kwa watu wa Mungu kuruhusu neema ya Mungu kuleta mabadiliko katika maisha yao, ili hatimaye, waweze kupata tumaini na maisha ya uzima wa milele. Huu ni mwaliko wa kuondokana na wasi wasi na tabia ya kujikatia tamaa. Mtakatifu Paulo, Mwalimu na Mtume wa Mataifa anapendekeza watu kuweka macho yao juu ya vitu visivyoonekana, vitu ambavyo ni vya milele. Maisha ya mwanadamu hupyaishwa kila kukicha na kwamba, hatima ya mwanadamu ni tumaini la maisha ya uzima wa milele. Baada kifo, kuna ufufuko wa wafu na maisha ya uzima wa milele; hatima na ukamilifu wa maisha ya mwanadamu.
Katika Fumbo la Msalaba, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kwa wafu, Mwenyezi Mungu alikamilisha mpango wa upendo wake kwa mwanadamu kwa kumfunulia huruma ya Mungu isiyokuwa na kifani, ili mwanadamu aweze kutambua kwamba, kwa hakika yeye ni mwana mpendwa wa Mungu, jambo ambalo limekusudiwa na Mwenyezi Mungu tangu milele yote. Kumbe, maisha ya mwanadamu yanasimikwa katika furaha, mateso, uchungu, mafanikio na hata pengine kushindwa kwake, lakini yote haya ni sehemu ya mchakato wa mabadiliko yanayoendelea kutendeka katika maisha ya mwanadamu. Mabadiliko haya ni sawa na mbegu inayokufa, ili kuchipua maisha mapya. Hata mwanadamu baada ya kuvuka kizingiti cha kifo, amekusudiwa kuwa na maisha mapya na yenye utukufu. Mchakato wa mabadiliko haya tayari umekwisha kuanza. Kristo Yesu, Usiku ule alipotolewa, aliweka Sadaka ya Ekaristi Takatifu yaani Mwili na Damu yake Azizi. Alifanya hivyo ili kuendeleza Sadaka ya Msalaba siku zote mpaka atakaporudi, kusudi amwachie Bibi Arusi mpendwa, yaani Kanisa, ukumbusho wa mateso, kifo na ufufuko wake. Hii ndiyo Sakramenti ya upendo, umoja, karamu ya Pasaka ambamo Kristo Yesu, huliwa, na roho hujazwa neema, na ambamo waamini wanapewa amana ya uzima wa milele. Ekaristi Takatifu ni chemchemi na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Ni Sakramenti ya sadaka, shukrani, kumbukumbu na uwepo endelevu na angavu wa Kristo Yesu kati ya waja wake kwa nguvu ya Neno na Roho wake Mtakatifu. Hii ni Karamu ya Pasaka na amana ya utukufu ujao. Rej. KKK 1322 – 1419.
Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., anasema, maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, mwamini anatoa maisha yake kwa Mungu na hivyo kumpokea Kristo Yesu anayewabadilisha katika upendo wake usiokuwa na kifani na hivyo, maisha kubadilishwa katika Kristo Yesu, kwa kuwaleta pamoja mbele za Baba yake wa milele. Ekaristi Takatifu ni sehemu ya mchakato wa mabadiliko halisi yanayomfanya mwamini kushiriki katika maisha na uzima wa milele, kuanzia sasa. Hakika ya mambo yajayo ni sehemu ya matumaini ya kazi iliyochapwa na kuratibiwa na Mwenyezi Mungu mwenyewe, anayemwalika mwanadamu kutembea kwa ujasiri huku akiyaelekea maisha na uzima wa milele. Binadamu wote ni watoto wateule wa Mungu. Yale yajayo ni sehemu ya mpango wa Mungu uliofichuliwa kwa kiasi, kielelezo cha maajabu ya Mungu. Waamini wakumbuke kwamba, wao ni watoto wapendwa wa Mungu, raia wa mbinguni na wanaoishi kwa ajili ya Mungu pamoja na kuendelea kuwa na matumaini ya maisha na uzima wa milele.