Mafungo Sekretarieti Kuu ya Vatican: Kuzaliwa Upya Katika Roho
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mababa wa Kanisa wanasema, Mwana wa Mungu, katika hali ya kibinadamu aliyofungamana nayo, aliposhinda mauti kwa kifo chake na ufufuko wake, alimkomboa mwanadamu, akamgeuza kuwa kiumbe kipya (taz. Gal 6:15; 2Kor 5:17). Maana kwa kuwashirikisha Roho wake, anawafanya ndugu zake waitwao kutoka katika mataifa yote kuwa mwili wake katika fumbo. Ndani ya mwili huo uhai wa Kristo hutiwa katika waamini, ambao kwa njia ya Sakramenti wanaunganishwa, kwa jinsi ya siri na ya kweli, na Kristo Yesu aliyeteswa na kutukuzwa. Maana kwa ubatizo tumefananishwa na Kristo: “Kwa maana katika Roho mmoja sisi sote tulibatizwa kuwa mwili mmoja” (1Kor 12:13). Katika ibada hii takatifu ushirikiano wetu na kifo cha Kristo Yesu na ufufuko wake huonyeshwa kwa ishara na kutekelezwa: “Basi tulizikwa pamoja naye kwa njia ya ubatizo katika mauti yake”; na “kama tulivyounganika naye katika mfano wa mauti yake, kadhalika tutaunganika kwa mfano wa kufufuka kwake” (Rum 6:4-5). Kwa kushiriki kweli mwili wa Bwana katika kumega mkate wa Ekaristi, twainuliwa hadi tuufikie ushirikiano naye na kati yetu, “Kwa kuwa mkate ni mmoja, sisi tulio wengi tu mwili mmoja; kwa maana sisi sote twapokea sehemu ya ule mkate mmoja” (1Kor 10:17). Hivyo sisi sote tumekuwa viungo vya mwili ule (taz. 1Kor 12:27), “na sisi tu viungo, kila mmoja kwa mwenzake” (Rum 12:5). Rej. LG 7. Sakramenti ya Ubatizo ni mlango wa imani na msingi wa maisha yote ya Kikristo. Hili ni lango la kuingilia uzima katika Roho “Vitae spiritualis ianua”. Ni mlango unaomwezesha mwamini kuzipata Sakramenti nyingine zote. Kwa njia ya Ubatizo, mwamini anafanywa huru toka dhambi na kuzaliwa upya kama mtoto wa Mungu, anakuwa ni kiungo cha Kristo Yesu na kuingizwa katika Kanisa na hivyo kufanywa washiriki katika utume wake. Kimsingi Ubatizo ni Sakramenti ya kuzaliwa upya kwa maji katika Neno!
Ni katika muktadha huu, Sekretarieti kuu ya Vatican kuanzia tarehe 9 hadi 14 Machi 2025 “inapanda kwenda Mlimani” kwa ajili ya mafungo ya maisha ya kiroho, kama sehemu ya maandalizi ya Maadhimisho ya Pasaka ya Bwana, sanjari na Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo. Mafungo haya yanaongozwa na Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., Mtaalamu wa Sayansi ya Maandiko Matakatifu na Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa. Kiini cha mafungo haya ni “Tumaini la Maisha na Uzima wa Milele” kama Mama Kanisa anavyofundisha na kukiri katika Kanuni ya Imani ya Nicea: “Nangojea na ufufuko wa wafu, na uzima wa milele ijayo. Amina.” Padre Roberto Pasolini anasema, Imani ya Kanisa inasimikwa katika: Mateso, Kifo na Ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, chemchemi ya matumaini kwa waamini, changamoto na mwaliko kwa waamini kugundua tunu na uzuri wa maisha ya uzima wa milele, hasa wakati huu, Mama Kanisa anapoadhimisha Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo na wakati huu, Baba Mtakatifu Francisko anapokabiliana na changamoto ya afya. Kifo ni tokeo la dhambi na kwamba, utii wa Kristo Yesu uligeuza laana ya kifo kuwa baraka. Taarifa rasmi kutoka kwa Dr. Matteo Bruno, Msemaji mkuu wa Vatican inaonesha kwamba, hali ya afya ya Baba Mtakatifu Francisko inaendelea kuimarika zaidi kwa kupumua kama kawaida pamoja na kuendelea na mazoezi ya kupumua kwa viungo bila mashine. Baba Mtakatifu anaendelea na matibabu, anapata muda wa sala na tafakari; anashiriki katika mafungo ya kiroho yanayotolewa na Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., kwa njia ya video na kwamba, anaendelea kuonesha ucheshi na uchangamfu, lakini madaktari bado wanaendelea kumwangalia kwa karibu sana. Jumatano tarehe 12 Machi 2025 ameshiriki pia katika mafungo ya maisha ya kiroho kwa njia ya video.
Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., katika tafakari yake, Jumatano tarehe 12 Machi 2025, amegusia kuhusu umuhimu wa kuzaliwa upya katika Maji na Roho Mtakatifu yaani kuzaliwa upya katika maisha ya kiroho kama Kristo Yesu anavyofafanua kwenye Injili ya Yohane, wakati Kristo Yesu akijadiliana na Nikodemo: “Amin, amin, nakuambia, Mtu asipozaliwa kwa maji na kwa Roho, hawezi kuuingia ufalme wa Mungu.” Yn 3:5. Kristo Yesu anakazia umuhimu wa kuzaliwa kutoka juu, hali inayohitaji toba, wongofu wa ndani na mabadiliko ya kweli, kwa kuondokana na miundo ya zamani ambayo kwa sasa imepitwa na wakati. Huku ni kuzaliwa kwa maji na Roho Mtakatifu, mwanzo mpya wa maisha mintarafu kazi ya Roho Mtakatifu. Huu ni mwaliko kwa waamini kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu, kwa kuyaacha mazoea na mang’amuzi yao ya zamani; kwa kumtegemea na kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu, ili aweze kumwongoza katika upeo mpya ambao haujagunduliwa. Ni katika muktadha huu, Waisraeli wanakumbukumbu ya maisha na safari yao Jangwani kwa muda wa miaka arobaini na kwamba wakiwa safarini Waisraeli waliogopa kifo, lakini wakabahatika kupata wokovu kwa kutazamia Ishara iliyotolewa na Mwenyezi Mungu. Leo hii ishara ya wokovu ni Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Ubatizo ni ishara ya maisha haya mapya, lakini huu ni mwanzo wa safari ya mabadiliko. Hata hivyo katika historia yote; ufanisi wa Sakramenti ya Ubatizo umedhohofika, mara nyingi zinafanywa kuwa ni desturi ya kitamaduni badala ya kutoa upendelea wa pekee katika imani. Hali hii imepelekea kuzuka kwa migogoro ndani ya Kanisa, ambapo maisha ya Kikristo yanaonekana kuwa ni ya kufikirika na hivyo kuelea kwenye ombwe katika maisha ya watu wengi.
Kristo Yesu anawaalika wafuasi wake kufanya uchaguzi kwa kutoa kipaumbele cha pekee katika ujenzi wa mahusiano na mafungamano na Kristo Yesu, kwa kutambua kwamba, uzima wa milele unapatikana kwa Mungu mwenyewe. Hii ni changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, “wanapoteza maisha” katika maana ya kibayolojia na kiakili, ili kuupata tena mwelekeo wa milele. Hatimaye, Kristo Yesu anatumia sitiari ya kuzaa mtoto kuelezea kwamba, kuzaliwa upya katika maji na Roho Mtakatifu, yaani kuzaliwa upya kiroho ni hatua inayobeba uchungu ndani mwake, lakini ni ya lazima. Kila mtu anaitwa kuacha “mimba” yake ya asili ili kukaribisha utimilifu wa maisha na uzima wa milele. Mtakatifu Francisko wa Assisi ni kielelezo cha mtu ambaye aliacha uhakika na usalama wote ili kukumbatia na kuambata kikamilifu maisha mapya katika Kristo Yesu! Kwa hakika kuzaliwa upya kwa maji na Roho Mtakatifu si wazo la kufikirika bali ni ukweli unaotoa nafasi kwa Roho Mtakatifu kufanya mabadiliko, kwa kuishi ahadi za maisha ya uzima wa milele. Padre Roberto Pasolini, OFM Cap., anasema, maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia yamezalisha dhana ya kutokufa, hali inayowaongoza watu kupuuza mipaka ya hali ya ubinadamu. Hofu ya kifo inaendelea kupungua na hivyo kuondoa mila na desturi njema zilizomsaidia mwanadamu kukabiliana kikamilifu na kwa ujasiri na Fumbo la kifo. Leo hii kifo ni habari inayoshika uzito wa chini kabisa katika vyombo vya mawasilino ya jamii na kwamba kifo ni changamoto ya kufundisha maendeleo ya sayansi na teknolojia ya tiba ya mwanadamu. Lakini kwa Wakristo wanapaswa kufahamu maana ya ndani kabisa ya kifo na tumaini la maisha na uzima wa milele. Mtakatifu Francisko wa Assisi anakiita kifo kuwa ni “dada kifo” kama njia mbadala ya kukubali ukomo wa kibinadamu kma sehemu inayoongoza kwenda kwenye umilele.
Mtakatifu Yohane, Mwinjili anasema, “Sisi tunajua kwamba tumekwisha pita kutoka katika kifo na kuingia katika uhai kwa sababu tunawapenda ndugu zetu. Mtu asiye na upendo hubaki katika kifo.” 1Yn 3:14. Kupenda hadi mwisho maana yake ni kukubali ukomo wa maisha ya mwanadamu na hivyo kuubadilisha kuwa ni fursa ya kujisadaka bila ya kujibakiza. Kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake, Kristo Yesu, amekipatia kifo maana mpya kabisa na kwamba, Fumbo la Umwilisho ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Mungu kwa binadamu. Mwinjili Marko anaelezea kuhusu Fumbo la Pasaka kuwa ni ufunuo wa ukombozi wa mwanadamu, mwaliko wa kutoogopa kurejea tena kwa Mwenyezi Mungu anayeokoa kwa njia ya Fumbo la Msalaba. Fumbo la Umwilisho linawataka waamini wabaki imara katika kuamini ukweli huu kwamba upendo hadi mwisho kamwe hauzeeki na kwamba, umeshuhudiwa na vizazi kwa vizazi, mwaliko kwa waamini kuendelea kuimba wimbo huu wa upendo.