杏MAP导航

Tafuta

Msamaha kama chemchemi ya matumaini ndiyo kauli mbiu ambayo imeongoza maadhimisho ya Jubilei ya Wamisionari wa Huruma ya Mungu kuanzia tarehe 28-30 Machi 2025. Msamaha kama chemchemi ya matumaini ndiyo kauli mbiu ambayo imeongoza maadhimisho ya Jubilei ya Wamisionari wa Huruma ya Mungu kuanzia tarehe 28-30 Machi 2025.   (Vatican Media)

Maadhimisho ya Jubilei ya Wamisionari wa Huruma ya Mungu: Msamaha Na Matumaini

Msamaha kama chemchemi ya matumaini ndiyo kauli mbiu ambayo imeongoza maadhimisho ya Jubilei ya Wamisionari wa Huruma ya Mungu kuanzia tarehe 28-30 Machi 2025. Papa Francisko anapenda kuwashukuru na kuwapongeza Wamisionari wa Huruma ya Mungu kwa kuendelea kuwa ni mashuhuda wa ufunuo wa Uso wa Baba mwenye huruma, kielelezo cha upendo usiokuwa na kikomo, anayewaita waja wake kujikita katika toba, wongofu na utakatifu wa maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu yalifunguliwa rasmi tarehe 8 Desemba 2015, Kumbukizi ya Miaka 50 tangu Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ulipoadhimishwa na mwaka huu ukafungwa tarehe 20 Novemba 20216. Hii ilikuwa ni fursa makini kwa huruma ya Mungu kuwa ni kiini cha tafakari ya maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Hii ni tafakari ambayo inapaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu kwa njia ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Hii inatokana na ukweli kwamba, huruma ya Mungu ni kiini cha Injili na njia muafaka ya uinjilishaji mpya unaojikita katika mchakato wa ushuhuda wenye mvuto na mashiko, kielelezo cha imani tendaji! Imekuwa ni nafasi kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuchunguza dhamiri zao, ili kuangalia ikiwa kama maisha yao yanaendana na utu wema sanjari na kweli za Kiinjili zinazotangazwa na kushuhudiwa na Mama Kanisa. Kimsingi hili ndilo lililokuwa lengo kuu la maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Misericordia et misera” yaani “Huruma na haki” anasema, huruma ya Mungu inapaswa kuendelezwa katika medani mbali mbali za maisha ya watu kama utimilifu wa huruma, upendo na msamaha wa Mungu unaobubujika kutoka katika Fumbo la Umwilisho linalopata utimilifu wake katika Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo kutoka kwa wafu! Huruma ya Mungu inajionesha katika maadhimisho ya Sakramenti mbali mbali za Kanisa, lakini kwa namna ya pekee kabisa, Sakrameti ya Ekaristi Takatifu, Upatanisho na Mpako wa Wagonjwa. Huruma ya Mungu inaendelea kujifunua katika historia na maisha ya watu kwa njia ya Neno la Mungu, ikikumbukwa kwamba, Biblia ni muhtasari wa ufunuo wa huruma ya Mungu kwa binadamu!

Wamisionari wa huruma ya Mungu ni mashuhuda wa huruma ya Mungu
Wamisionari wa huruma ya Mungu ni mashuhuda wa huruma ya Mungu   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Uso wa huruma “Misericordia vultus” na “Misericordia et misera” yaani “Huruma na haki” ni nyaraka zinazoweza kuwasaidia waamini kutambua na kuthamini ukuu wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, changamoto anasema Baba Mtakatifu ni kwa Jumuiya za Kikristo kuhakikisha kwamba, zinaendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma ya Mungu, kama kielelezo makini cha imani tendaji. Kwa njia hii, Kanisa litaendelea kuwa kweli ni shuhuda wa huruma ya Mungu na utambulisho wa Kanisa. Maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu ilikuwa ni fursa kwa waamini kurejea tena katika mambo msingi ya imani, maisha ya kiroho, sala, tafakari na hija za maisha ya kiroho. Katika maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu Francisko aliwateuwa Wamisionari wa huruma, ili waweze kuwa ni ishara ya hamasa ya kimama ya Kanisa kwa Taifa la Mungu, wakiwezeshwa kuingia kwa undani katika utajiri wa fumbo la msingi la imani. Hawa ni mapadre waliopewa dhamana na wajibu wa kuwaondolea watu hata dhambi ambazo kwa kawaida, huondolewa na Kiti cha Kitume pekee, ili upana wa utume wao uonekane wazi. Hawa ni ishara ya huruma ya Baba wa milele kwa watoto wake wanaokimbilia huruma na upendo wake usiokuwa na kikomo! Hawa ni Wamisionari wa huruma kwani wanatumwa na Mama Kanisa kama vyombo vinavyotoa hamasa ya kushinda vikwazo na kuanza maisha mapya ya Ubatizo, daima wakijitahidi kuwa waaminifu, kwa kumkazia macho Kristo Yesu, Kuhani mkuu, wenye rehema na mwaminifu katika mambo ya Mungu. Wamisionari hawa walianza utume wao rasmi, Jumatano ya Majivu, Februari 2016.

Wamisionari wa Huruma ya Mungu ni vyombo na mashuhuda wa huruma
Wamisionari wa Huruma ya Mungu ni vyombo na mashuhuda wa huruma   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume, “Misericordia et misera” “Huruma na haki” aliwathibitisha Wamisionari wa huruma ya Mungu kuendelea na utume wao kama kielelezo hai cha neema ya maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu. Lengo la Baba Mtakatifu ni kuwaondolea waamini vikwazo na vizingiti vilivyokuwa vinawazuia kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu kwa njia ya wongofu wa ndani, toba, msamaha na upatanisho. Mapadre kwa nguvu ya Sakramenti waliyoipokea sasa wameongezewa madaraka ya kuweza hata kusamehe dhambi ya utoaji mimba ambayo hapo awali ilikuwa imeachwa rasmi kwa Askofu na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Lengo ni kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa Kanisa Katoliki. Wamisionari hawa katika maisha na utume wao wanaongozwa na kauli mbiu “Mungu amewafunga wote pamoja katika kuasi ili awarehemu wote” (Rej. Rom. 11: 32) na Rej. Misericordiae vultus 18-19. Msamaha kama chemchemi ya matumaini ndiyo kauli mbiu ambayo imeongoza maadhimisho ya Jubilei ya Wamisionari wa Huruma ya Mungu kuanzia tarehe 28-30 Machi 2025. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa Wamisionari wa Huruma ya Mungu uliosomwa kwa niaba yake na Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Mwenyekiti mwenza, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, Jumamosi tarehe 29 Machi 2025. Baba Mtakatifu Francisko kutoka katika sakafu ya moyo wake, anapenda kuwashukuru na kuwapongeza Wamisionari wa Huruma ya Mungu kwa kuendelea kuwa ni mashuhuda wa ufunuo wa Uso wa Baba mwenye huruma, kielelezo cha upendo usiokuwa na kikomo, anayewaita waja wake kujikita katika toba na wongofu wa ndani, ili kuwapyaisha tena kwa huruma na msamaha.

Wamisionari wa huruma ya Mungu ni mahujaji wa matumaini
Wamisionari wa huruma ya Mungu ni mahujaji wa matumaini   (Vatican Media)

Mwenyezi Mungu hufuta machozi ya waja wake kwa: wongofu na msamaha; na kama wadhambi, kukumbatiwa na mikono ya Mama Kanisa kwa njia ya msamaha na hivyo kuendelea na hija ya matumaini, huku “bondeni kwenye machozi.” Kristo Yesu anawafungulia waja wake njia inayowawezesha kusafiri pamoja huku wakimfuasa kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, chemchemi ya amani. Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime Wamisionari wa Huruma ya Mungu katika maisha na utume wao kama waungamishaji, akiwataka zaidi kuwa wasikivu kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa kusikilizana, tayari kuwakaribisha wadhambi wanaokimbilia huruma ya Mungu, tayari kupyaisha maisha yao ya kiroho na hivyo kumrudia Mwenyezi Mungu. Huruma ya Mungu ni chemchemi ya mabadiliko ya toba na wongofu wa ndani; Msamaha wa Mungu ni chanzo cha matumaini mapya yanayowawezesha waamini kumtegemea Mungu katika hali yote. Fumbo la Umwilisho ni kielelezo makini cha uwepo angavu wa Mungu katika maisha yao na kamwe Mungu hawezi kuwatupa. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Francisko anawatakia Wamisionari wa huruma ya Mungu hija yenye kuzaa matunda bora, huku akiwabariki wamisionari wote wa Huruma ya Mungu kwa moyo wake wote, mwishoni akawaweka Wamisionari hawa wote katika ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa huruma, ili aweze kuwaombea.

Wamisionari wa Huruma 2025
30 Machi 2025, 15:59