Kumbukizi Ya Miaka 12 Tangu Papa Francisko Achaguliwe Kuliongoza Kanisa Katoliki
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Ni katika maadhimisho ya Sherehe ya Mtakatifu Yosefu, Mume wake Bikira Maria, tarehe 19 Machi 2013, Baba Mtakatifu Francisko aliposimikwa rasmi kuwa Khalifa wa Mtakatifu Petro wa 266 kwa kuchagua jina la Mtakatifu Francisko wa Assisi. Vipaumbele vyake tangu wakati huo ni: Maskini, Amani, Mazingira na sasa ni Udugu wa kibinadamu unaofumbatwa katika diplomasia ya huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka kwa waja wake wote sanjari na ujenzi wa Kanisa la Kisinodi. Maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii ni amana na utajiri wa Kanisa; wao ndio walengwa wakuu wa Habari Njema ya Wokovu. Hawa ni maskini wa hali na mali; wanaotumbukizwa katika biashara ya binadamu na viungo vyake; wanaodhalilishwa na kunyanyaswa utu, heshima na haki zao msingi kama watu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani, utawala bora, ushirikiano na mshikamano katika kukabiliana na changamoto mamboleo kwamba ni mambo yanayopaswa kupewa kipaumbele cha pekee. Baba Mtakatifu Francisko anajikita kwenye siasa safi kwa ajili ya huduma kwa jamii, maendeleo, ustawi na mafao ya wengi; utu, haki msingi za binadamu na umuhimu wa kufanya mageuzi makubwa kwenye Umoja wa Mataifa ili kweli uweze kuwa ni kielelezo cha “familia ya Mataifa.” Watu wa Mungu hawana budi kujikita zaidi katika mchakato wa majadiliano na urafiki ili kujenga sanaa ya watu kukutana.
Baba Mtakatifu anapembua kuhusu makutano yaliyopyaishwa ili kujenga misingi ya haki na amani; msamaha kwa kuondokana na “dhana ya vita ya haki na halali” ambayo kwa sasa imepitwa na wakati kama ilivyo pia kwa adhabu ya kifo kwani inakwenda kinyume cha haki msingi za binadamu, utakatifu na zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Baba Mtakatifu anapinga kwa nguvu zote utamaduni wa kifo! Dini na udugu wa kibinadamu ni chanda na pete; hapa mkazo ni umuhimu wa dini kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu na kwamba, Kanisa litaendelea kujizatiti katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu kwa kuzingatia kanuni msingi za Kiinjili, utu, heshima na haki msingi za binadamu. Ni katika muktadha wa kumbukizi ya Miaka Kumi na Miwili, tangu Baba Mtakatifu Francisko alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, lakini kwa sasa amelazwa kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli iliyoko mjini Roma tangu Ijumaa tarehe 14 Februari 2025; sauti yake ni dhaifu inayojikita katika mamlaka fundishi ya udhaifu wa mwili. Baba Mtakatifu amelazwa hospitalini hapo kwa takribani mwezi mmoja. Habari zinazokuja kutoka hospitalini hapo kuhusu matibabu ya Baba Mtakatifu zinatia moyo na kwamba, inatumainiwa kuwa Baba Mtakatifu hivi punde ataweza kuruhusiwa kuondoka hospitalini na kurejea tena mjini Vatican kuendelea na utume wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu.
Hii ni sehemu ya tahariri ya Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano, wakati huu, Baba Mtakatifu Francisko anapoadhimisha miaka kumi na miwili, tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki. Changamoto ya ugonjwa na hatimaye kulazwa kwake ni kumbukumbu ya pekee kabisa katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Huu ni mwaka ambayo umeshuhudia hija ndefu za kitume zilizofanywa na Baba Mtakatifu Francisko nchini Indonesia, Papua New Guinea, Timor ya Mashariki pamoja na Singapore. Baba Mtakatifu alihitimisha Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yaliyokuwa yakinogeshwa na kauli mbiu “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Lengo kuu la Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ni kuliwezesha Kanisa kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza na kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wake. Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu daima yanapania pamoja na mambo mengine: kujenga na kudumisha urika wa Maaskofu, tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha.
Leo hii, Baba Mtakatifu Francisko, Khalifa wa Mtakatifu Petro amelazwa kati ya wagonjwa, anateseka, lakini anaendelea kuombea amani, huku akisindikizwa na umati wa watu wa Mungu wanaoendelea kumwombe afya njema. Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha miaka kumi na miwili ya maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, daima amekuwa akihitimisha: Katekesi, Mikutano na Sala ya Malaika wa Bwana kwa kusema, “tafadhali msisahau kuniombea.” Leo hii anaombewa na umati mkubwa wa waamini na watu wenye mapenzi mema wanaomwombea kama kielelezo chao cha upendo na mshikamano wao na Baba Mtakatifu. Kuna tofauti kubwa kati ya Askofu wa Roma na Mkurugenzi wa Mashirika ya Kimataifa. Henri De Lubac “aliona uovu mbaya zaidi ambao Kanisa linaweza kujikuta limetumbukia humo, kwa “kuamini kwamba, lina nuru yake” kwa kutegemea nguvu zake; sera na mikakati yake lenyewe pamoja na ufanisi wake na hivyo kuacha kuwa ni Fumbo la Mwezi “Mysterium lunae” linaloakisi nguvu za Kristo Yesu, kwa kuishi na kufanya kazi kwa nguvu na uweza wa Kristo Yesu kwani anasema, “Mimi ni mzabibu, ninyi ni matawi. Akaaye ndani yangu, nami ndani yake, huyo huzaa sana; maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya jambo lolote.” Yn 15:5.
Haya ni maneno yanayowaongoza waamini pamoja na watu wenye mapenzi mema, kuendelea kuangalia kwa imani na matumaini yale yanayojiri kwenye ghorofa ya kumi, ambako Baba Mtakatifu Francisko amelazwa. Mama Kanisa anamshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu kwa mafundisho na ushuhuda wa udhaifu wa mwili na sauti dhaifu na tete inayoendelea kusali kwa ajili ya amani duniani na wala si vita; majadiliano katika ukweli na uwazi na wala si uonevu; huruma na upendo na wala si tabia ya kutojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Kanisa linamtakia heri na baraka Baba Mtakatifu anapofanya kumbukizi ya Miaka 12 tangu alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, kwa hakika watu wa Mungu wanayo hamu ya kuendelea kuisikiliza sauti yake, ndivyo Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano anavyohitimisha tahariri yake kuhusu kumbukizi ya Miaka 12 tangu Baba Mtakatifu Francisko alipochaguliwa kuliongoza Kanisa Katoliki, tarehe 13 Machi 2013.