杏MAP导航

Tafuta

Msamaha kama chemchemi ya matumaini ndiyo kauli mbiu ambayo imeongoza maadhimisho ya Jubilei ya Wamisionari wa Huruma ya Mungu kuanzia tarehe 28-30 Machi 2025. Msamaha kama chemchemi ya matumaini ndiyo kauli mbiu ambayo imeongoza maadhimisho ya Jubilei ya Wamisionari wa Huruma ya Mungu kuanzia tarehe 28-30 Machi 2025.   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Kilele cha Jubilei ya Wamisionari wa Huruma ya Mungu 2025: Toba Na Msamaha Wa Kweli

Ni katika muktadha wa huruma ya Mungu; Msamaha kama chemchemi ya matumaini ndiyo kauli mbiu ambayo imeongoza maadhimisho ya Jubilei ya Wamisionari wa Huruma ya Mungu kuanzia tarehe 28-30 Machi 2025 kwa kuhitimishwa na Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu mkuu Salvatore Fisichella, Mwenyekiti mwenza, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu kwenye Kanisa la “Sant’ Andrea della Valle” Jimbo kuu la Roma. Zameni kwenye Mafumbo ya Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anazungumzia kuhusu zawadi na umuhimu wa maungamo kwa kukiri kwamba, mwamini anaweza kuomba huruma ya Mungu moja kwa moja bila kupitia kwa viongozi wa Kanisa waliopewa dhamana na kuwaondolea watu dhambi zao. Lakini, Mama Kanisa kwa busara yake, anataka watoto wake kuonesha moyo wa toba na wongofu wa ndani kwa kumwendea Padre anayemwakilisha Kristo Yesu katika kiti cha maungamo. Hii ndiyo njia sahihi ya kuweza kupata huruma ya Mungu ambayo kimsingi ina mwelekeo pia wa kijamii, tayari kuponya madonda, mipasuko na kinzani za kijamii. Waamini wanakwenda kwenye kiti cha huruma ya Mungu si kwa kutaka kuhukumiwa, bali kukutana na hatimaye, kuambata huruma ya Mungu inayoendelea kuusimamisha ulimwengu. Kutokana na mwelekeo huu, maungamo si kama “mashine ya kufulia nguo” wala “chumba cha mateso na udadisi usiokuwa na mashiko” unaofanywa na baadhi ya waungamishaji, hali ambayo inadhalilisha Sakramenti ya Kitubio. Mapadre watoe mashauri kwa unyenyekevu pasi na kuhukumu, wawe tayari kusamahe kwa moyo wote kwa kutambua kwamba, wao ni vyombo tu vya huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kujitambua kwamba wao ni wadhambi, wanapaswa kutubu na kumwongokea Mungu, ili aweze kuwaonjesha huruma na upendo wake usiokuwa na kifani. Hii ni neema ambayo waamini wanapaswa kuiomba kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa kutambua kwamba, huruma ya Mungu ni kubwa zaidi kuliko hata dhambi zinazotendwa na mwanadamu na kwamba, msamaha wake ni dawa makini dhidi ya dhambi. Mwenyezi Mungu kama ilivyokuwa kwa Baba mwenye huruma daima anawasubiri watoto wake kukimbilia huruma, kwa njia ya toba na wongofu wa ndani. Kitendo cha mwamini kukimbilia kiti cha huruma ya Mungu kinaonesha toba ya ndani, sala inayopaswa kujikita katika unyenyekevu wa moyo badala ya litania ya maneno mengi!

Wamisionari wa huruma ya Mungu ni vyombo na mashuhuda wa huruma.
Wamisionari wa huruma ya Mungu ni vyombo na mashuhuda wa huruma.   (Vatican Media)

Baba Mtakatifu anakaza kusema, hata Khalifa wa Mtakatifu Petro anahitaji kuonja huruma ya Mungu katika maisha yake, kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Petro, pale alipotambua mapungufu yake akaangua kilio! Muungamishaji asiwe ni mtu mwenye kiburi, bali aoneshe unyenyekevu na ukweli wa maisha, kwa kutambua kwamba, hata yeye pia ni mdhambi anahitaji huruma ya Mungu. Muungamishaji ajenge utamaduni wa kusikiliza kwa makini bila kuhukumu, akionesha huruma kama aliyokuwa nayo Baba mwenye huruma kama anavyosimuliwa na Mwinjili Luka, hiki ni kielelezo makini cha huruma ya Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kanisa linalaani dhambi, lakini linamkumbatia mdhambi anayetambua dhambi zake, tayari kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu. Kanisa halina budi kusamehe bila kuchoka kama anavyofundisha Kristo Yesu mwenyewe kwa wafuasi wake. Mwenyezi Mungu yuko radhi kumpokea mwamini anayeonesha moyo wa toba na wongofu wa ndani, tayari kukumbatia na kuambata huruma ya Mungu. Kanisa lipo ili kuwawezesha waamini kukutana na huruma ya Mungu katika maisha yao. Baba Mtakatifu anasema, ili Kanisa liweze kutekeleza dhamana na wajibu wake, halina budi kutoka kwa kutambua kwamba, Kanisa ni kama hospitali kwenye uwanja wa vita, ambako linakutana na majeruhi wanaohitaji kusikilizwa, kueleweka, kusamahewa pamoja na kuonjeshwa upendo. Waamini wakaribishwe kwa heshima na taadhima wanapokimbilia huruma ya Mungu, bila kuwanyanyasa wala kuwakejeri. Huruma ya Mungu si dhana ya kufikirika inayoelea kwenye ombwe anasema Baba Mtakatifu Francisko, bali ni sifa kuu ya Mungu na mafundisho ya Kanisa.

Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella
Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella   (Vatican Media)

Yesu alikuja ulimwenguni ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti kwa kumjalia maisha ya uzima wa milele. Ni mganga wa kweli anayewatafuta wagonjwa na wala si wenye haki ambao hawahitaji kutubu na kumwongokea Mungu. Familia ni shule ya kwanza ya huruma ya Mungu na kwamba hapa wanafamilia wanajifunza kupenda na kupendwa, kusamehe na kusamehewa. Si matarajio yake kuona malango ya magereza yanafunguliwa na wafungwa wote kuachiwa huru hata wale waliotenda makosa makubwa ya jinai. Hapa Baba Mtakatifu anakaza kusema, wafungwa wasaidiwe kutubu, kuongoka na kuanza tena kuandika ukurasa mpya wa maisha yao, wakiwa ni watu wema zaidi kuliko walivyoingia magerezani. Ni katika muktadha wa huruma ya Mungu; Msamaha kama chemchemi ya matumaini ndiyo kauli mbiu ambayo imeongoza maadhimisho ya Jubilei ya Wamisionari wa Huruma ya Mungu kuanzia tarehe 28-30 Machi 2025 kwa kuhitimishwa na Ibada ya Misa Takatifu iliyoongozwa na Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Mwenyekiti mwenza, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu kwenye Kanisa la “Sant’ Andrea della Valle” Jimbo kuu la Roma. Katika mahubiri yake amesema, wahusika wakuu katika Liturujia ya Neno la Mungu, Dominika ya Nne ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka C wa Kanisa ni: Baba mwenye huruma na Mwana mpotevu na Kaka mkubwa, kielelezo cha upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu mdhambi. Watu katika ulimwengu mamboleo wanataka kuwa na uhuru usiokuwa na mipaka, uhuru unaowapeleka watu hawa mbali na uwepo wa Mungu pamoja na Kanisa lake na hivyo kushindwa kuchota upendo kutoka katika chemchemi ya huruma ya Mungu.

Wamisionari wa huruma ya Mungu ni mahujaji wa matumaini
Wamisionari wa huruma ya Mungu ni mahujaji wa matumaini   (Vatican Media)

Kaka mkubwa ni mfano wa waamini wengi. Ni mtu ambaye hakuridhika na ujio wa Mwana mpotevu; ni watu ambao wanabadili huduma yao na uaminifu wa Mungu; ni watu wanaojisahau na kudhani kwamba, sadaka katika huduma inaweza kugeuzwa na kuwa ni silaha dhidi ya Mwenyezi Mungu, kwani mtazamo wa namna hii ni “kichaka cha dhambi.” Huu ni mwaliko kwa waamini kuchuchumilia na kuambata tunu msingi za ukaribu wa Mungu kwa waja wake. “Akamwambia, Mwanangu, wewe u pamoja nami sikuzote, na vyote nilivyo navyo ni vyako.” Lk 15:31. Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, amewaonya Mapadre kutofanya utume wao kwa mazoea, kama kitu kinachorudiwa rudiwa na kwamba, huduma inayotolewa ni matunda ya utendaji wao, kiasi cha kushindwa kufurahi pamoja na Mwenyezi Mungu. Kumbe, ukaribu na ushiriki wa Mafumbo ya Kanisa uwaongoze Mapadre kuzama zaidi katika mawazo ya Baba mwenye huruma, kwa kujikita zaidi katika upendo na uwazi kwa upendo wa Baba wa milele. Mapadre wawe na upeo mpana na matarajio makubwa, kwa wale walio mbali na Kanisa na hawa ambao wanawahudumia kila siku. Huu ni mwaliko wa kupanua nyoyo na akili zao ili kuzama zaidi katika Mafumbo ya Kanisa. Mapadre waige mfano wa Baba mwenye huruma, aliyetoka mbio kwenda kumlaki Mwana mpotevu, aliyetenda makosa, akawa mbali na huruma na upendo wa Baba yake mwenye huruma na kwamba, maisha yake yalikosa dira, mwelekeo na maana. Mapadre wanakumbushwa kwamba, ule ukaribu wa Baba kwa njia ya kumkumbatia Mwana mpotevu, ni kielelezo cha upendo unaofuta na kusahau dhambi; upendo ambao ni chemchemi ya msamaha na chachu ya toba na wongofu wa ndani, tayari kuanza kutembea katika mwanga wa maisha mapya. Huu ni upendo unaozima hasira, wivu, kashfa na kejeri kutoka kwa Mtoto mkubwa, kwa kuonesha moyo wa uvumilivu na utulivu huku akimsihi “Parakalei” akisema: “Mwanangu, wewe u pamoja nami siku zote, na vyote nilivyo navyo ni vyako. Tena, kufanya furaha na shangwe ilipasa, kwa kuwa huyu ndugu yako alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana.” Lk 15: 31-32.

Wamisionari wa Huruma ya Mungu ni vyombo na mashuhuda wa huruma
Wamisionari wa Huruma ya Mungu ni vyombo na mashuhuda wa huruma   (Vatican Media)

Baba Mwenye huruma alikuwa anajitahidi kumfafanulia kijana wake mkubwa kwamba, alikuwa anawathamini wote kama “mboni ya jicho lake.” Wazazi wanafahamu sana changamoto ya malezi na makuzi iliyoko mbele yao. Baba Mwenye huruma anakazia mambo msingi yaliyoko moyoni mwake na wala si utekelezaji wa Amri tu. Hii ni fursa kwa waamini kujichunguza kutoka katika undani wa nyoyo zao kama wanajisikia kufanyiwa sherehe ili wapate kufurahi. Kufanya sherehe ni mchakato wa ujenzi udugu na ujirani mwema, ili kushinda woga na tabia ya kujikatia tamaa, kama sehemu ya kumbukizi ya makosa yalitotendwa huko nyuma katika maisha. Mwenyezi Mungu anasamehe dhambi na kufanya sherehe kwa sababu ya toba na wongofu wa ndani unaotekelezwa na watoto wake. Watoto wote wawili wanapaswa kujitambua kwamba, wao ni ndugu wamoja, wanapaswa kurejea tena nyumbani, ili kuonja na kushuhudia ukuu wa upendo wa Baba kwa kujikita katika upatanisho kamili. Wamisionari wa Huruma ya Mungu wamekumbushwa kwamba, wao ni mashuhuda wa ufunuo wa upendo mkuu wa Mungu na vyombo maalum vya upatanisho kwani wao wanao wajibu wa kuwasaidia waamini kuingia katika undani wa maisha yao, tayari kuchota neema ya toba na wongofu wa ndani, ili kujipatanisha tena na Mungu pamoja na jirani zao. Fumbo la Ekaristi ni chemchemi ya msamaha na upatanisho, ni sherehe na karamu kubwa inayoandaliwa na Baba mwenye huruma na kwamba, msamaha na upatanisho wa kweli unaadhimishwa katika Fumbo la Ekaristi Takatifu, chemchemi ya upendo unaosamehe, kielelezo cha fumbo la imani ya Kanisa.

Kilele cha Jubilei Wamisionari
30 Machi 2025, 15:30