Jubilei ya Watu wa Kujitolea: Mahujaji wa Upendo na Matumaini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mafundisho Jamii ya Kanisa yanasema kwamba, wema na huruma ambavyo vinasukuma matendo ya Mungu na kuleta uwezo wa kuyaelewa vinakuwa karibu sana na mwanadamu, hadi kuchukua sura ya mwanadamu Yesu, ambaye ni Neno aliyejifanya mwili. Katika Injili ya Mtakatifu Luka, Yesu anaeleza huduma yake ya kimasiha kwa maneno ya Nabii Isaya ambayo yanakumbusha maana ya kinabii ya Jubilei: "Roho wa Bwana yu juu yangu, kwa maana amenitia mafuta kuwahubiri maskini habari njema. Amenituma kuwatangazia wafungwa kufunguliwa kwao, na vipofu kupata kuona tena, kuwaacha huru waliosetwa, na kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa" (Lk 4:18-19; taz. Isa 61:1-2). Kwa hiyo, Kristo Yesu anajiweka, katika mstari wa mbele wa utimilifu, siyo tu kwa sababu yeye hutimiza yaliyoahidiwa na kutazamiwa na Israeli, lakini pia, kwa undani zaidi, kwa sababu katika yeye tendo kuu katika historia ya Mungu na watu linatimizwa. Yeye hutangaza: "Aliyeniona mimi amemwona Baba" (Yn 14:9). Yaani, Kristo Yesu ni ufunuo wazi na halisi wa jinsi Mungu anavyotenda kwa ajili ya watu wake. Kwa kutafakari juu ya majitoleo na wingi wa zawadi ya Mungu Baba katika Mwana, ambayo KristoYesu alifundisha na kuishuhudia kwa kutoa uhai wake kwa ajili ya ukombozi wa binadamu, Mwinjili Yohane anapata maana yake halisi na matokeo yake muhimu zaidi. "Wapenzi, ikiwa Mungu alitupenda sisi hivi, imetupasa na sisi kupendana. Hakuna mtu aliyemwona Mungu wakati wowote. Tukipendana, Mungu hukaa ndani yetu, na pendo lake limekamilika ndani yetu" (1Yn 4:11-12). Kutendeana upendo kunadaiwa na amri ambayo Kristo Yesu hutaja kama "mpya" na kama "yake": "Mpendane. Kama vile nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo" (Yn 13:34). Amri ya kupendana inaoneesha jinsi ya kuishi katika Kristo Yesu maisha ya Fumbo la Utatu Mtakatifu ndani ya Kanisa lililo Fumbo la Mwili wa Kristo, pia jinsi ya kugeuza historia hadi kwamba, ifikie utimilifu wake katika Yerusalemu ya mbinguni.
Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Watu wa Kujitolea kuanzia tarehe 8 Machi na kilele chake tarehe 9 Machi 2025, Baba Mtakatifu Francisko amemteuwa Kardinali Michael Czerny, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Fungamani ya Binadamu kuwa ni mwakilishi wake katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu itakayoadhimishwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kuanzia saa 4:30 kwa Saa za Ulaya, sawa na Saa 6:30 kwa Saa za Afrika Mashariki na Kati. Jubilei hii inahudhuriwa na watu wa kujitolea zaidi ya 25, 000, kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Hii ni fursa kwa vyama na mashirika mbalimbali ya shughuli za kujitolea kuragibisha shughuli zao. Kujitolea ni kitendo cha mtu au kikundi cha watu kufanya kazi mahali fulani kwa kusudio la kukuza ujuzi au kusaidia jamii bila kutegemea malipo. Hapa mtu anasadaka muda, rasilimali na vipaji vyake kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kazi ya kujitolea ni muhimu sana hata kwa mhusika kwani hujiongezea ufahamu, ujuzi na kukuza mahusiano, uzoefu na mafungamano ya kijamii. Wakati mwingine, sadaka na majitoleo ya namna hii ni fursa ya kupata ajira, kwani kwa njia ya majitoleo yake, mtu hujenga tabia ya kujiamini na hivyo kumwezesha kuwa mbobezi katika uwanja wake. Majitoleo haya humwongezea mhusika mtazamo wa kufanya maamuzi na hivyo kuwa ni sehemu ya mchakato wa maendeeo endelevu na fungamani ya binadamu. Kumbe, kuna haja ya kujenga na kudumisha ari na moyo wa watu kujitolea katika huduma kwa Mungu na jirani.
Kujitolea pia, kwa upande mwingine kuna changamoto zake, lakini kwa hakika majitoleo ni amana na hazina kubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Kujitolea ni kutoa sehemu ya muda wako, ujuzi na maarifa uliyonayo na wakati mwingine nguvu zako kufanya kazi ya watu wengine bila kupata malipo ya moja kwa moja. Kazi unayoifanya kwa kujitolea mara nyingi ungeweza kuifanya kwa kudai ujira lakini unaamua kuifanya bure kwani maisha ni zaidi ya fedha. Kujitolea, kwa mantiki hii, ni kuelewa kuwa si lazima ubadilishane ujuzi na muda wako kwa vipande vya fedha. Wakati mwingine mtu anaweza kutoa ujuzi, maarifa na nguvu zake kwa lengo tu la kujisikia furaha ya kutoa mchango wake katika mchakato wa maboresho ya maisha ya wengine ambao katika hali ya kawaida wasingeweza kunufaika na ujuzi huo bila kulipia. Mara nyingi vyuo huwafunza maarifa ya jumla yanayoweza yasioane kabisa na matakwa ya soko la ajira. Hii ni kwa sababu si rahisi vyuo kufanya utafiti wa mara kwa mara kubaini mahitaji ya soko la ajira kwa minajili ya kurekebisha mitaala yao. Katika mazingira kama haya, kujitolea humsaidia mtu kujifunza ujuzi mahususi anaohitaji ili kuajirika kirahisi bila kulazimika kuulipia kwa fedha isipokuwa kwa kutumia nguvu na muda wake. Siku hizi kuna msemo kwamba watu ni mtaji. Ni muhimu kwa jamii kujenga tabia ya kujitolea kwa kuwasaidia wengine kwa kutumia rasilimali muda, karama na mapaji na kwa kufanya hivi, watu wanajiwekea hazina mbinguni, kwani mwanadamu hawezi kubadilisha mambo mengi kwa ujira.