杏MAP导航

Tafuta

Baba mwenye huruma, Mwana mpotevu na Kaka mkubwa, kielelezo cha upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu mdhambi. Baba mwenye huruma, Mwana mpotevu na Kaka mkubwa, kielelezo cha upendo na huruma ya Mungu kwa binadamu mdhambi.   (Vatican Media)

Injili ya Baba Mwenye Huruma Kwa Watoto Wake Wote! Toba, Wongofu na Msamaha Wa Kweli

Kipindi hiki cha Kwaresima sanjari na Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo, ni muda wa kujikita katika uponyaji. Baba Mtakatifu Francisko anasema hata yeye anapitia katika changamoto za afya kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuwashukuru na kuwaombea wote wanaoendelea kumwombea ili apone haraka. Kwa mfano wa Kristo Yesu, waamini nao pia wawe ni vyombo na mashuhuda wa uponyaji kwa jirani zao kwa neno na tendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Liturujia ya Neno la Mungu na hasa Injili ya Dominika ya IV ya Kipindi cha Kwaresima Mwaka C wa Kanisa inabeba ujumbe wa furaha ya Baba mwenye huruma anayewapenda, kuwajali na kuwasubiri watoto wake ili waweze kutubu na kumwongokea, tayari kuanza kutembea katika mwanga mpya wa maisha. Dominika ya IV ya Kipindi cha Kwaresima pia huitwa "Domenica Laetare" au “dominika ya furaha” hii ni furaha ya toba na wongofu wa ndani tayari kumrudia Mwenyezi Mungu. Ni furaha, utulivu na amani ya ndani, baada ya mwamini kujipatanisha na nafsi yake, Mwenyezi Mungu, jirani pamoja na mazingira nyumba ya wote. Rej. Lk 15:1-3; 11-32. Sehemu hii ya Injili kwa wengi inajulikana kama “Injili ya Mwana Mpotevu.” Lakini inapaswa kuitwa “Injili ya Baba Mwenye Huruma” kwani ndiye mhusika mkuu anayewangojea watoto wake wawili, waweze kutubu na kurejea tena nyumbani, ili aweze kuwafanyia sherehe. Baba Mwenye huruma ni kielelezo cha Mungu Baba Mwenyezi anayesamehe daima, ambaye yuko tayari kuwapokea na kuwafanyia watoto wake sherehe, hata kama wametenda dhambi kubwa kiasi gani. Jambo la msingi ni: toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata njia ya maisha mapya. Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu, unaowatafuta wale wote waliopotea. Mifano yote mitatu katika Injili ya Luka15:1-32, inaonesha mapungufu katika maisha ya mwanadamu: Mchungaji amempoteza kondoo, mwanamke amepoteza shilingi na Baba mwenye huruma amempoteza Mwana, ingawa alikuwa na mwanae mkubwa, lakini akapiga moyo konde na kuendelea kumsubiri. Hiki ni kielelezo cha mtu anayependa kwa dhati, kwani hataki hata mara moja chochote kile kipotee. Baba Mtakatifu anasema huruma ya Mungu ndiyo mahangaiko ya upendo wake kwa binadamu dhaifu na mdhambi. Huruma hii inamsumbua na “kumnyima usingizi” kiasi cha kuacha yote na kuanza kumtafuta binadamu dhaifu na mdhambi, ili akimpata aweze kumbeba na kumweka mabegani mwake, kielelezo cha Baba mwenye huruma na mapendo thabiti, au Mama anayeteseka kwa kukosekana kwa mtoto wake mpendwa.

Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma ya Mungu
Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma ya Mungu   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Baba Mtakatifu Francisko, katika tafakari yake wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, Dominika tarehe 30 Machi 2025 anasema, Mwinjili Luka, Dominika ya IV ya Kipindi cha Kwaresima anawaonesha Mafarisayo na Waandishi wakimnung’unikia Kristo Yesu kwa kuwakaribisha wadhambi pamoja na kula nao. Kristo Yesu anawatolea mfano wa Baba Mwenye huruma, Mwana mpotevu na Mtoto mkubwa, “Mwana mtiifu aliyebaki nyumbani mwa Baba.” Mwana mpotevu aliondoka nyumbani, lakini akaja kuishia katika umaskini, alipotafakari sana moyoni mwake akajuta makosa yake, na kuamua kurejea tena nyumbani, alipofika, Baba mwenye huruma akampokea kwa shangwe kubwa, lakini yule Mtoto mkubwa, “Mwana mtiifu” akasusia sherehe hiyo na hivyo kumlazimu Baba mwenye huruma kutoka nje kwenda kumtafuta Mwanaye mpendwa ili aweze kushiriki katika furaha ya Baba wa milele. Kristo Yesu ni ufunuo wa moyo wa Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, anayependa kuganga na hatimaye kuponya majerana ya waja wake ili waweze kupendana na kuthaminiana kama ndugu wamoja. Kipindi hiki cha Kwaresima sanjari na Maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2025 ya Ukristo, ni muda wa kujikita katika uponyaji. Baba Mtakatifu anasema hata yeye anapitia katika changamoto za afya kiroho na kimwili. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii, kuwashukuru na kuwaombea wote wanaoendelea kumkumbuka na kumwombea ili apone haraka. Kwa mfano wa Kristo Yesu, waamini nao pia wawe ni vyombo na mashuhuda wa uponyaji kwa jirani zao, kwa njia ya neno lao sayansi, upendo na sala zao. Udhaifu na magonjwa anasema Baba Mtakatifu ni mambo yanayofanana sehemu mbalimbali za dunia na kwamba, Wakristo ni ndugu katika wokovu ambao unapata chimbuko lake kutoka kwa Kristo Yesu.

Salam za rambirambi kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko
Salam za rambirambi kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko   (ANSA)

Baba Mtakatifu Francisko ameendelea kujiaminisha katika huruma ya Mungu, anawaomba waamini kuungana pamoja naye kwa ajili ya kuombea amani nchini Ukraine, Palestine, Israel, Lebabon, DRC na Myanmar ambayo inaendelea kuteseka kutokana na tetemeko la ardhi lililotokea Ijumaa tarehe 28 Machi 2025 na kusababisha watu zaidi ya 1,600 kupoteza maisha na kwamba, idadi hii inaweza kuongezeka maradufu. Watu zaidi ya milioni 20 hawana makazi maalum, chakula, maji na makazi. Baba Mtakatifu Francisko anasema, anafuatilia kwa hofu na wasiwasi mwingi kuhusu hali tete ilivyo nchini Sudan. Baba Mtakatifu anatoa rai kwa viongozi wote wanaohusika kujibidiisha katika ujenzi wa amani, ambayo ni matunda ya majadiliano katika ukweli na haki, ili kupunguza mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu Sudan, ili hatimaye, kujenga mustakabali wa haki, amani na utulivu. Nchini Sudan vita inaendelea kusababisha vifo vya watu wasiokuwa na hatia, rai kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko ni kwa wahusika kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maisha ya ndugu zao na hivyo kuanza tena kwa haraka kwa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kupata suluhu ya kudumu ya mgogoro huu. Baba Mtakatifu anaisihi Jumuiya ya Kimataifa kuongeza juhudi katika kukakabiliana na janga hili la kutosha katika maisha ya watu wa Mungu huko nchini Sudan. Mwishoni mwa ujumbe wake, Baba Mtakatifu Francisko anapongeza juhudi za kuweka mipaka kati ya Tajikistan na Kyrgystan, mfano bora wa majadiliano ya kidiplomasia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Huu ni mfano bora wa kuigwa na kwamba, nchi hizi mbili ziendelee kujikita katika njia hii. Bikira Maria Mama wa huruma, aisaidie Familia ya binadamu kupatanishwa kwa amani.

Baba Mwenye Huruma 2025
30 Machi 2025, 15:00