Fumbo la Msalaba, Mateso Na Kifo Katika Maisha ya Mwanadamu
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu umefunuliwa kwa njia ya Fumbo la Msalaba, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Ni katika muktadha huu, Msalaba unakuwa ni kitabu cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Katika maisha na utume wa Kanisa, Wakristo wa nyakati mbalimbali wamesoma na kulitafakari Fumbo la Msalaba na hapo wakapata chemchemi ya majibu yaliyozima kiu ya maisha yao ya ndani! Kwa njia ya Roho Mtakatifu, wameweza kutambua msingi wa sayansi ya huruma na upendo wa Mungu, chemchemi ya hekima na busara ya Kikristo, yaani mwanga wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuishi katika mwanga wa Mungu kwa kutambua kwamba, utukufu wa Mungu umetundikwa Msalabani! Kwa Mtakatifu Petro, wanafunzi wengine na hata Wakristo katika ulimwengu mamboleo bado Msalaba unaonekana kuwa ni kashfa ya mwaka. Lakini, kwa Kristo Yesu, kashfa inakuja pale Mkristo anapoukimbia Msalaba, yaani kukimbia na kutofanya mapenzi ya Mungu, utume na kazi ya ukombozi ambayo alitumwa na Baba yake wa mbinguni kuja kutekeleza. Ni kutokana na mazingira haya, Kristo Yesu, akageuka na kumwambia Petro “Nenda nyuma yangu, Shetani! U kikwazo kwangu, maana huyawazi yaliyo ya Mungu, bali ya wanadamu” Rej. Mt. 16: 23. Msalaba ni alama takatifu ya huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu. Ni Sadaka ya Kristo Yesu na kamwe, Msalaba usigeuzwe kuwa ni alama ya mapambo shingoni au kuhusianishwa na imani za kishirikina. Kila mara mwamini anapomtaza Kristo Yesu aliyetundikwa Msalabani, amwone kuwa ni Mtumishi mwaminifu wa Mungu, aliyetekeleza dhamana na utume wake, kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wake unaoleta wokovu, kwa ajili ya maondoleo ya dhambi za binadamu. Matokeo yake, kama kweli waamini wanataka kuwa wafuasi wake, wanapaswa kufuata nyayo zake, kwa kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya upendo kwa Mungu na jirani.
Msalaba wa Kristo ni chombo cha wokovu na utukufu wa Mungu. Badala ya kashfa na utupu, Msalaba unakua ni chombo cha ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu! Ni ishara ya mapendo, neema, sala, msamaha, upatanisho na matumaini. Ni kutokana na maana hii mpya, Mama Kanisa anaona fahari kuu kuutangaza utukufu na kuimba sifa kuu za Msalaba wa Bwana wetu Yesu Kristo. Msalaba unaendelea kumfunza mwamini kwamba, hakuna mapendo kamili yasiyokuwa na mateso na matumaini ya uzima wa milele. Changamoto kwa waamini katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo ni kuuangalia, kuutafakari, kuushangaaa, kuusikiliza, kuuheshimu, kuutukuza na kuuabudu kwa imani, matumaini na mapendo, kwani ni kielelezo ambacho wokovu wa dunia umetundikwa juu yake! Fumbo la Msalaba wa Kristo Yesu yaani: Mateso, kifo na ufufuko wake ni kilele cha ufunuo wa: huruma, upendo, ukuu, utukufu na utakatifu wake, changamoto kwa Wakristo ni kushikamana pamoja na Kristo katika mapambano, ili siku moja waweze kushinda pamoja naye! Huu ndio ujumbe wa matumaini unaofumbatwa kwa namna ya pekee katika Fumbo la Msalaba, mwaliko kwa waamini kumtafakari Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu kuwa ni kiini cha imani ya Kikristo. Fumbo la Msalaba ni alama ya upendo wa Mungu kwa binadamu; kielelezo cha sadaka ya hali ya juu kabisa ya Kristo Yesu dhidi ya ukosefu wa haki msingi za binadamu; ubinafsi, dhuluma na nyanyaso. Msalaba ni alama ya ushindi dhidi ya dhambi na kifo. Msalaba ni kielelezo cha mateso, dhuluma na nyanyaso dhidi ya Wakristo wanaouwawa kikatili kwa kuchomwa moto wangali hai; na wakati mwingine nyanyaso na dhuluma hizi zinatendwa katika hali ya ukimya mkubwa.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Msalaba unatisha, kama ilivyojionesha hata kwa Mitume wa Yesu, waliotaka kukimbia madhulumu ya Nero; Mtume Petro kwa mshangao mkubwa akakutana na Kristo Yesu njiani akielekea mjini Roma ili aweze kusulubishwa mara ya pili; hapo ndipo Mtume Petro alipoishiwa nguvu, akapiga moyo konde na kufuata nyayo za Kristo Yesu, kiasi hata cha kuyamimina maisha yake juu ya Msalaba: miguu juu, kichwa chini, kwa kutambua kwamba, Yesu alikuwa amempenda upeo! Baba Mtakatifu anasema, kwa njia ya Msalaba, Yesu anajiunga na wale wote wanaodhulumiwa na kuteswa; watu ambao hawana tena nguvu ya kupiga kelele; hasa watu wasiokuwa na hatia wala ulinzi madhubuti; familia zinazokabiliana na hali ngumu ya maisha; wale wanaolia na kuomboleza kwa kuondokewa na wapendwa wao katika maisha; wanaowalilia watoto wao waliotumbukia katika matumizi haramu ya dawa za kulevya. Kwa njia ya Fumbo la Msalaba, Yesu anaungana na mamillioni ya watu wanaoteseka kutokana na baa la njaa duniani wakati ambapo kuna sehemu nyingine za dunia wanakula na kusaza! Anajiunga na wale wanaoteswa na kudhulumiwa kutokana na imani, mawazo na rangi ya ngozi yao. Kristo Yesu anaendelea kujiunga na umati mkubwa wa vijana uliopoteza dira, mwelekeo na matumaini ya maisha kutokana na wanasiasa wanaowaongoza kuelemewa mno na uchoyo, ubinafsi, rushwa na ufisadi. Yesu anaendelea kuungana kwa njia ya Fumbo la Msalaba na waamini ambao wamepoteza imani yao kwa Mungu na Kanisa kutokana na kashfa na utepetevu wa imani ulioneshwa na watumishi wa Injili. Yesu anayapokea yote haya kwa mikono miwili na kujitwika mabegani mwake pamoja na Misalaba ya wafuasi wake, tayari kuwaambia, jipeni moyo kwani yuko pamoja nao na kwamba, ameshinda dhambi na mauti na yuko kati yao ili kuweza kuwakirimia matumaini na maisha tele!
Fumbo la Msalaba ni mwaliko kwa kila mwamini kuwa kama: Simoni wa Kirene, aliyemsaidia Kristo Yesu kubeba Msalaba, Mtakatifu Veronica aliyeupangusa Uso wa Yesu, kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria na kwa wanawake wengine watakatifu, waliopiga moyo konde, wakaifuata ile Njia ya Msalaba; “Via Crucis”; Njia ya uchungu “Via Dolorosa” wakiwa wamesheheni upendo na huruma hadi chini ya Msalaba, wakiwa wamesheheni matumaini kwa Kristo Yesu, Mkombozi wa ulimwengu. Tarehe 4 Machi 2025 Usiku, Kardinali Arthur Roche, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Ibada, nidhamu na Sakramenti za Kanisa, amewaongoza watu wa Mungu kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko ambaye kwa sasa anasumbuliwa na ugonjwa wa mkamba (Bronchitis) uliopelekea kulazwa tangu Ijumaa tarehe 14 Februari 2025 kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli iliyoko mjini Roma. Naye Kardinali Marcello Semeraro, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza waamini kuwa wenye heri na watakatifu amewaongoza watu wa Mungu kusali Rozari Takatifu, Jumatano ya Majivu, tarehe 5 Machi 2025. Taarifa rasmi kutoka kwa Dr. Matteo Bruno, Msemaji mkuu wa Vatican inaonesha kwamba, Jumatano ya Majivu, Baba Mtakatifu ameendelea na matibabu pamoja na mazoezi ya kupumua bila mashine, ameshiriki Ibada ya kupakwa majivu na baadaye akapata Ekaristi Takatifu na kuendelea na mapumziko pamoja na kufanya kazi ndogo ndogo hospitalini hapo. Amepata nafasi ya kuzungumza kwa njia ya simu na Padre Gabriel Romanelli, Paroko wa Parokia ya Familia Takatifu, Ukanda wa Gaza. Taarifa ya afya ya Baba Mtakatifu Francisko Alhamisi asubuhi ilionesha kwamba, alipata usingizi mwanana usiku wa kuamkia Alhamisi tarehe 6 Machi 2025 na kwamba, asubuhi ameendelea na mapumziko!