Barua ya Papa Francisko Kwa Luciano Fontana: Umuhimu Wa Amani: Vita Ni Upuuzi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Mtakatifu Yohane XXIII katika Wosia wake wa Kitume, “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” anasema amani inasimikwa katika: ukweli, haki, upendo na uhuru. Kumbe, kuna haja ya kukuza na kudumisha utamaduni wa kuheshimu: utu, heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu sanjari na haki msingi za binadamu na kwamba, kila mtu anapaswa kuwajibika, ili kujenga na kuimarisha mafungamano ya kijamii na mahusiano pamoja na Mwenyezi Mungu. Ni katika muktadha wa kulinda na kudumisha amani duniani, Baba Mtakatifu Francisko katika barua aliyomwandikia Luciano Fontana, Mkurugenzi mkuu wa Gazeti la Corriere della Sera linalochapishwa nchini Italia, kama sehemu ya majibu yake kwa ukarimu aliomwonesha wa kumtakia matashi mema wakati huu anapoendelea na tiba kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli iliyoko mjini Roma tangu Ijumaa tarehe 14 Februari 2025, anamwomba, kutoa kipaumbele cha kwanza katika kurasa za gazeti lake umuhimu wa kulinda na kudumisha amani duniani kwani vita ni upuuzi mtupu na kwamba, umefika wakati wa kupokonya silaha duniani ili kudumisha amani.
Udhaifu wa kibinadamu una uwezo wa kumweka mwanadamu katika uwazi kwa kile kinachoendelea, kinachopita, kile kinachomfanya mwanadamu kuishi na kile kinachompoka uhai wake. Labda hii ndiyo sababu inayopelekea baadhi ya watu kukataa mipaka ya ubinadamu na hivyo, kujiepusha na watu dhaifu na wale waliojeruhiwa. Kwa sababu watu hawa wana uwezo wa kuhoji mwelekeo unaochaguliwa na viongozi, kama watu binafsi na kama jumuiya. Baba Mtakatifu anapenda kumhimiza Luciano Fontana, Mkurugenzi mkuu wa Gazeti la Corriere della Sera pamoja na wale wanaojisadaka kwa kazi ya akili kwa kutoa taarifa kupitia vyombo vya mawasiliano ya jamii, yanayowaunganisha walimwengu kiasi cha kujisikia kuwa kama “Kijiji” kujikita katika ukweli unaojenga mazingira ya binadamu. Waandishi wa habari wanaweza kuunganisha au kuwagawa watu; kutumikia ukweli au kuupuuzia.
Baba Mtakatifu anakaza kusema, umefika wakati wa kuwapokonya watu silaha za maneno, ili kuponya silaha za akili, ili hatimaye, kuweza kuipokonya dunia silaha zinazosababisha majanga makubwa katika maisha ya mwanadamu. Kuna haja ya kufanya tafakari ya kina kwa utulivu na katika hisia za utata. Vita inasababisha uharibifu mkubwa wa jamii, bila kutoa suluhisho kwa migogoro na kinzani zinazomwandama mwanadamu. Diplomasia na Mashirika ya Kimataifa yanahitaji anasema Baba Mtakatifu Francisko maisha mapya na uaminifu na kwamba, dini zinaweza kutumia maisha ya kiroho, ili kuamsha tena ile kiu ya ujenzi wa udugu wa kibinadamu, haki, sanjari na tumaini la amani. Hii ni changamoto inayohitaji sadaka na majitoleo; kwa kufanya kazi, katika ukimya na kwa njia ya maneno. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawaalika wanatasnia ya mawasiliano ya jamii kujisikia wamoja katika juhudi hizi za kujenga na kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watu, kwani hii neema ya mbinguni inayowatia moyo na kuwasindikiza.