Barua Kuhusu Mchakato wa Usindikizaji, Tathmini na Utekelezaji wa Maazimio ya Sinodi
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini kuliombea Kanisa linaloitwa kutafsiri na hatimaye, kumwilisha mang’amuzi yaliyofanywa katika Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yaliyonogeshwa na kauli mbiu: “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume.” Lengo kuu la Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu ni kuliwezesha Kanisa kuendelea kujizatiti katika ujenzi wa utamaduni wa kuwasikiliza na kuwashirikisha waamini walei katika maisha na utume wake. Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu yanapania pamoja na mambo mengine: kujenga na kudumisha urika wa Maaskofu, tayari kumsikiliza Roho Mtakatifu, Mhimili mkuu wa mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha adili na matakatifu. Baba Mtakatifu anaishukuru Sekretarieti kuu ya Sinodi kwa kuandaa mpango mkakati unaopaswa kutekeleza na Makanisa Mahalia katika kipindi cha Miaka mitatu kuanzia sasa. Mwishoni mwa tafakari yake, Baba Mtakatifu Francisko anawaweka waamini na watu wenye mapenzi mema, chini ya ulinzi na tunza za Bikira Maria, ili awasaidie kuwa ni vyombo na mashuhuda wa mwanga wa amani ya Kristo Yesu. Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu imeyaandikia barua Mabaraza ya Maaskofu Katoliki, kuhusiana na mchakato wa usindikizaji, tathmini na utekelezaji wa maamuzi yaliyotolewa kwenye maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu. Mchakato huu umeridhiwa na Baba Mtakatifu Francisko, tayari kwa utekelezaji wake. Baba Mtakatifu anayataka Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbalimbali za dunia, kuhakikisha kwamba, yanasambaza mchakato huu, ili uweze kuwafikia watu wengi zaidi na kwamba, hitimisho la mchakato huu, utakuwa ni Mkutano wa Kanisa utakaoadhimishwa Mwezi Oktoba 2028, mjini Vatican.
Hatua hii ni kadiri ya Katiba ya Sinodi, ili kuhakikisha kwamba, maamuzi yake yanaingizwa na kumwilishwa katika maisha ya Makanisa mahalia na hatimaye, kwenye Kanisa zima. Lengo ni kuendelea kuimarisha mchakato uliokwisha kufikiwa hadi wakati huu na wala hakuna nia ya kuitisha tena Sinodi nyingine. Hati ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu imegawanyika katika sura tano, ikiwa na utangulizi pamoja na hitimisho lake. Sura ya kwanza inazungumzia kiini cha hulka ya Kisinodi ni wito kutoka kwa Roho Mtakatifu kuhusu wongofu; Pili, wote wakiwa katika Mtumbwi mmoja wanaitwa kuongoka katika mahusiano; Tatu ni kutupa nyavu katika mchakato wa wongofu; Nne ni Mavuno makubwa yanayosimikwa katika kifungo cha wongofu. Sura ya tano: Ni kutumwa, Majiundo ya watu wa Mungu kama Mitume wamisionari na hatimaye ni kuadhimisha sherehe kwa watu wote. Kama sehemu ya utangulizi, Mababa wa Sinodi wanasema, Roho Mtakatifu anaendelea kutenda kazi ndani ya Kanisa, kwa kujenga umoja na ushirika wa watu wa Mungu, hata katika tofauti zao msingi. Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu yanajidhihirisha katika mateso ya watu wa Mungu kutoka sehemu mbalimbali za dunia; watu wenye kiu ya: haki na amani ambayo ni mchakato wa watu wote wa Mungu, kwani Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, “furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati zetu, hasa ya maskini na ya wale wote wanaoteswa, yote ni furaha na matumaini, uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia. Wala hakuna jambo lililo na hali halisi ya kibinadamu lisiloigusa mioyo yao.” Gaudium et spes, 1.
Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu yaligawanyika katika awamu kuu mbili na kwamba, hati hii ni muhtasari wa safari nzima ya Maadhimisho haya iliyowahusisha watu wa Mungu katika ujumla wao kwa kutambua kwamba, kiini cha Sinodi kuanzia mwaka 2021 hadi mwaka 2024 “Kwa Ajili ya Kanisa la Kisinodi: Umoja, Ushiriki na Utume” mwaliko ni kulipyaisha Kanisa kwa kujisadaka katika huduma inayosimikwa katika utume, daima likitafuta njia za kuweza kuwa aminifu na kuendelea kujikita katika Mapokeo hai ya Kanisa, ili kumwilisha Mafundisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kwa: Kwa kusoma alama za nyakati; kutafuta na kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha. Maadhimisho ya Sinodi Awamu ya Pili yalianza kwa mwaliko wa toba na wongofu wa ndani kwa dhambi dhidi ya haki na amani; Utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote; dhambi dhidi ya wazawa, wakimbizi na wahamiaji; watoto na wanawake; maskini na kwa kushindwa kusikiliza kwa makini na ujenzi wa ushirika mambo yanayohitaji toba na wongofu wa ndani, kwa kuadhimisha Sakramenti ya huruma ya Mungu, upendo usiokuwa na mipaka sanjari na ushirika. Kanisa linataka kuwa ni kielelezo cha msamaha na upatanisho kutoka kwa Mungu na mashuhuda wa neema ya Mungu. Sasa Makanisa mahalia yanaalikwa kumwilisha hati hii katika uhalisia wa maisha ya Makanisa mahalia, kwa kuzingatia mchakato wa mang’amuzi na utekelezaji wake mintarafu Sheria na Hati yenyewe; kwa kuzingatia utamaduni na hali halisi ya Kanisa mahalia, katika hali ya utulivu na umoja. Lengo ni kumwilisha matunda ya Maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu kwa Kanisa zima. Ni wakati wa kufanya tathmini ya maamuzi yaliyofikiwa katika ngazi ya Kanisa mahalia sanjari na kufanya mang’amuzi ya maendeleo makubwa yaliyofikiwa kwenye majadiliano ya makundi pamoja na ushauri wa wanasheria wa Kanisa. Utekelezaji huu ni muhimu sana hasa kwa kuwashirikisha wadau wote waliochangia, na hivyo kujikita katika mchakato wa utamaduni wa kusikilizana. Mchakato huu unaundwa na kundi la: Wakleri, Watawa na Waamini walei, huku wakisindikizwa na Askofu mahalia. Kundi hili ni muhimu sana katika mchakato wa kusindikiza maisha na utume wa Kanisa mahalia.
Ni wakati wa kuthamini mchango uliotolewa; kupyaisha mang’amuzi na mitazamo yao na hivyo kuliwezesha Jimbo ambalo limewekeza kwa kiasi kikubwa katika maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu na hatimaye, matunda ya kazi hii, itabidi yawasilishwe kwenye Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu, kwa kuambatanisha kundi la rejea la Jimbo husika. Kundi hili la Sinodi, litaadhimisha Mwaka wa Jubilei kuanzia tarehe 24-26 Oktoba 2025. Lengo ni kuwashukuru na kuwapongeza wajumbe hawa kwa sadaka na majitoleo yao makubwa, sanjari na kuendeleza mchakato wa ujenzi wa Kanisa mahalia na hatima yake ni hapo Mwezi Oktoba 2028: Ziafuatazo ni tarehe maalum kwa ajili ya kufanya tathmini ya mchakato wa maadhimishio ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu. Mwezi Machi 2025 tangazo la kusindikiza mchakato wa maadhimisho ya Kanisa mahalia pamoja na tathmini yake. Mwezi Mei 2025 kutachapishwa Hati ya Utekelezaji wa Sinodi pamoja na washiriki wake. Tarehe 24-26 Oktoba 2025 ni maadhimisho ya Jubilei ya Washiriki wa Sinodi. Muhula wa kwanza wa Mwaka 2027 kunafanyika tathmini ya Kijimbo. Muhula wa Pili wa Mwaka 2027 kunafanyika tathmini katika ngazi ya Mabaraza ya Maaskofu, Kitaifa, Kikanda na Kimataifa. Muhula wa Kwanza mwaka 2028 Mkutano mkuu wa Kimabara ili kufanya tathmini. Mwezi Juni 2028 Kuchapishwa kwa Hati ya Kutendea Kazi, Instrumentum laboris, kwa ajili ya Mkutano wa Kikanisa utakaoadhimishwa Mwezi Oktoba 2028. Na Mwezi Oktoba 2028 ni Maadhimisho ya Mkutano wa Kikanisa, mjini Vatican. Tangu wakati huu, Sekretarieti kuu ya Sinodi za Maaskofu inaendelea kujizatiti katika huduma kwa Makanisa mahalia na kwamba, wahusika wakuu ni Maaskofu mahalia.
Kardinali Mario Grech, Katibu Mkuu wa Sinodi za Maaskofu katika mahojiano maalum aliyoyafanya na Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano anasema, maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu yamegawanyika katika sehemu kuu tatu: Maandalizi, Maadhimisho na Utekelezaji wake; maadhimisho yanayojikita katika toba na wongofu wa ndani, dhamana inayoendelea kutekelezwa na Makanisa mahalia. Mchakato huu unatoa umuhimu wa pekee kwa Makanisa mahalia pamoja na Urika wa Maaskofu kutekeleza dhamana na wajibu wao wa: Kufundisha, Kuongoza na Kuwatakatifuza watu wa Mungu. Huu ni muda muafaka wa kuendeleza utamaduni wa majadiliano na kusikilizana ndani ya Kanisa, kwa kushirikishana karama na zawadi za Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa; tayari kutembea kwa pamoja katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na hatima yake ni maadhimisho ya Mkutano wa Kikanisa hapo Oktoba 2028. Baba Mtakatifu atakuwa tayari kupokea mchango kutoka katika Makanisa mahalia, kwa ajili ya Kanisa zima. Itakumbukwa kwamba, Mwaka 2026 umetengwa maalum kwa ajili maadhimisho ya Sinodi katika ngazi ya: Majimbo, Kitaifa, Kikanda na Kimataifa, kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano, hali ya kusikilizana na kuwajibika kwa pamoja, ili hatimaye, kuweza kuandaa Hati ya Sinodi inayopata chimbuko lake katika utamaduni wa majadiliano. Huu ni mchakato unaotarajiwa kuwa na ushiriki mkubwa wa watu wa Mungu, “Portio populi Dei” tayari kumwilisha tunu msingi za Injili katika uhalisia wa maisha yao.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, Maadhimisho ya Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu “Peregrinantes in spem” yaani “Mahujaji wa matumaini.” Matumaini ya waamini yako katika Msalaba, yaani katika Kristo Yesu, chemchemi ya wokovu wa mwanadamu aliyezaliwa katika Familia Takatifu iliyopata baraka ya kuwa na Mungu yaani Emanueli kati yake. Hata Kanisa la Kristo ni hujaji wa matumaini, kwa kutembea kwa pamoja. Kumbe, tarehe 24-26 Oktoba 2025 ni maadhimisho ya Jubilei ya Washiriki wa Sinodi. Hawa ni watu waliosadaka muda, karama na mapaji yao kwa ajili ya maadhimisho ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu. Hii ni fursa ya kuendelea kukazia maana halisi ya ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari; kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani; tayari kupyaisha maisha na utume wa Kanisa, ili kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa watu waliopondeka na kuvunjika moyo. Kanisa linataka kuwa ni chombo na shuhuda wa wamisionari wa furaha ya Injili. Hati ya Sinodi ya XVI ya Maaskofu, ni kielelezo cha nguvu ya Kinabii; Huu ni mwaliko wa toba, wongofu wa ndani, tayari kuambata utakatifu wa maisha; Umoja na mshikamano wa watu wote wa Mungu. Changamoto ni kuendeleza wongofu wa kichungaji na kimisionari, mwaliko unaotolewa na Baba Mtakatifu Francisko.