Baba Mtakatifu Francisko: Mahubiri Jumatano ya Majivu 2025
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi cha Kwaresima kwa Mwaka 2025 unanogeshwa na kauli mbiu “Tutembee kwa pamoja katika matumaini.” Kwaresima ni kipindi cha imani na matumaini; toba na wongofu wa ndani, ili kukumbatia na kuambata huruma na upendo wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa mtu mmoja mmoja na kama Jumuiya ya waamini. Kwaresima ni kipindi cha kuimarisha na kuboresha imani, matumaini na mapendo kwa: kufunga na kusali; kwa kufanya toba na malipizi ya dhambi; kwa kushiriki kikamilifu katika Sakramenti za Kanisa; Kwa kusoma, kutafakari na hatimaye, kumwilisha Neno la Mungu katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo makini cha imani tendaji. Lengo ni kujitakasa na kuambata utakatifu wa maisha, ili hatimaye, kushiriki furaha ya Kristo Mfufuka wakati wa Sherehe ya Pasaka ya Bwana, huku waamini wakiwa wamepyaishwa kwa neema ya Roho Mtakatifu. Waamini watambue kwamba, wanaitwa kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao kwa watu wanaowazunguka na wale wote ambao Mwenyezi Mungu anawajalia fursa ya kukutana nao katika hija ya maisha yao, ili waweze kujaliwa mwanga na furaha ya Injili katika maisha. Mateso na kifo cha Kristo Msalabani, kiwe ni kikolezo cha toba na wongofu wa ndani kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa anayesema: “Lakini sikujulikana uso wangu na makanisa ya Uyahudi yaliyokuwa katika Kristo; ila wamesikia tu ya kwamba huyo aliyetuudhi hapo kwanza, sasa anaihubiri imani ile aliyoiharibu zamani. Wakamtukuza Mungu kwa ajili yangu.” Gal 1: 22-24. Waamini wajitahidi kuwa na kumbukumbu hai ya kukutana na Kristo Yesu katika maisha na utume wao. Ni wakati wa kuuvua utu wa kale na kuanza kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka.
Kipindi cha Kwaresima kinasimikwa katika nguzo kuu nne: yaani; Sala, Kufunga, Neno la Mungu na Matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo cha imani tendaji. Ibada ya Jumatano ya Majivu, inawaingiza Wakristo katika Kipindi cha Kwaresima, hija ya imani, matumaini na mapendo inayodumu kwa takribani siku arobaini, za toba na wongofu wa ndani. Ni wakati uliokubalika kwa waamini kumfungulia Mwenyezi Mungu na jirani zao, mioyo ya upendo na huruma. Binadamu kwa kupakwa majivu, anakumbushwa kwamba, yeye ni kiumbe cha Mungu aliyeteolewa kutoka mavumbini na mavumbini atarudi tena! Hapa Mwenyezi Mungu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza na pili ni kumheshimu binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.Majivu ni alama inayomwingiza mwamini katika Fumbo kuu la huruma na upendo wa Mungu katika maisha ya mwanadamu; kwa njia ya mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu. Majivu ni alama ya unyenyekevu, mwanzo mpya na kwamba, hapa duniani mwanadamu ni msafiri na wala hana makazi ya kudumu! Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri ya Jumatano ya Majivu, tarehe 5 Machi 2025, yaliyosomwa kwa niaba yake na Kardinali Angelo De Donatis Mhudumu mkuu wa Baraza la Kipapa la Toba ya Kitume amekazia: Umuhimu wa kumbukumbu ya utambulisho wao, mahujaji wa matumaini kwani Kristo Yesu kwa fumbo la Umwilisho ameshuka katika udongo wa nchi na kwa ufufuko wake amewapandisha wote katika Moyo mtukufu wa Baba yake wa milele.
Jumatano ya Majivu ni mwanzo wa safari ya kuelekea kwenye maadhimisho ya Fumbo la Pasaka, linalogusa udhaifu wa maisha ya mwanadamu na matumaini ya ufufuko wa wafu. Kwa kupakwa majivu, waamini wanafanya kumbukumbu kwamba, wao wameumbwa kutokana na mavumbi na mavumbini watarudi tena. Mavumbi ni kielelezo cha udhaifu wa binadamu unaojikita katika magonjwa, umaskini, matatizo na changamoto mbalimbali zinazoiandama familia ya binadamu.Huu ni udhaifu unaojionesha katika medani mbalimbali za maisha. Kutokana na uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote, katika maisha ya kijamii na kisiasa sanjari na itikadi zinazosigana na utu, heshima na haki msingi za binadamu. Huu ni udhaifu unaojikita katika ukwapuaji na matumizi mabaya ya rasilimali za dunia, vita, kinzani na misigano ya kijamii kati ya watu wa Mataifa. Yote haya ni mavumbi ya sumu yanayoendelea kuchafua mazimngira ya sayari hii, kiasi hata cha watu kushindwa kuishi kwa amani na utulivu, hali inayosababisha kila siku kuzuka kwa wasiwasi na hofu kwa siku za usoni. Majivu ni kielelezo cha kifo, kinacho mfanya mwanadamu kufanya tafakari na kuanza kujikita katika unyenyekevu, kwa kujitoa na kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengine. Majivu ni kielezo cha dhambi na mauti, lakini Kristo Yesu ameibuka mshindi kwa njia ya utukufu na maisha ya uzima wa milele.
Kwaresima ni kipindi cha kupyaisha matumaini, ili kuinua vichwa kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, ili kuwakirimia waja wake utukufu na maisha ya uzima wa milele na hivyo kuwapatanisha na Baba wa milele kama anavyosema Mtakatifu Paulo Mtume, “Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye.” 2Kor 5:21. Baba Mtakatifu Francisko anasema haya ndiyo matumaini yaliyojichimbia kwenye majivu, kielelezo cha udhaifu wa binadamu, na hofu mbele ya kifo, ni matumaini yanayohuisha majivu yaliyoko mbele ya waamini. Udhaifu wa binadamu na uzoefu wa kifo ni mambo yanayowazamisha watu katika huzuni na upweke hasi, kiasi cha kufikiria ufupi wa maisha wakisema: “Maisha yetu ni mafupi yenye masumbufu, wala hakuna dawa ya kuponya iwapo binadamu aujia mwisho wake, wala hajajulikana mtu awezaye kufungua ahera. Tumezaliwa kwa bahati tu, hatimaye tutakuwa kana kwamba hatukupata kuwapo kamwe. Mradi pumzi ya puani mwetu ni moshi, hata na akili ni cheche iliyowashwa kwa kupiga moyo wetu, ikizimika, mwili utageuka majivu.” Hek 2:1-3.
Kumbe, tumaini la Fumbo la Pasaka huwaunga mkono watu katika udhaifu wao, kwa kuwahakikishia msamaha wa Mungu, huku wakiwa wamefunikwa na majivu ya dhambi, huwafungulia ungamo la furaha ya maisha: “Lakini mimi najua ya kuwa Mteteaji wangu yu hai, Na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi.” Ayu 19:25. Mwanadamu ni mavumbi yenye thamani kubwa machozi pa Mungu, kwa sababu aliumbwa na Mungu na wala hakumpangia kufa. Majivu ambayo waamini wamepakwa ni ukumbusho wa tumaini la Pasaka ya Kristo Yesu, changamoto na mwaliko wa toba na wongofu wa ndani ili kumrudia tena Mungu kwa miyo yao yote, kwa kumweka kuwa ni kiini cha maisha yao, Kristo Yesu aliyefufuka kwa wafu. Waamini wajifunze kutoa sadaka, ishara ya tumaini na kwamba, wanahitaji kuonana na Mungu, mwisho wa safari yao ya maisha hapa duniani; kwa kutambua kwamba, kweli wanayo njaa ya upendo na ya uwepo angavu wa Mungu katika maisha yao; Mungu anayeweza kuwashibisha na hivyo kuwaboreshea tumaini la maisha. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Kristo Yesu amezaliwa katika majivu ya ulimwengu, kwa sababu historia ya dunia ni historia ya mbinguni; Mungu na mwanadamu wameunganishwa kwenye hatima moja. Kristo Yesu atafagia majivu ya kifo milele, ili kuwang’arisha waja wake, huku wakiwa na tumaini hili nyoyoni mwao, waamini wanahimizwa kuanza kutembea, ili hatimaye, waweze kujipatanisha na Mungu.