杏MAP导航

Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru watu wote wa Mungu wanaojisadaka na kumwombea afya njema. Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru watu wote wa Mungu wanaojisadaka na kumwombea afya njema.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Papa Francisko Anawashukuru Wote Wanaomwombea Afya Njema

Kabla ya kuanza Rozari, Alhamisi tarehe 6 Machi 2025 Baba Mtakatifu Francisko kutoka katika sakafu ya mtima wake, amewashukuru waamini na watu wote wenye mapenzi mema, waliokuwa wamekusanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu afya njema na kwamba, alikuwa anawasindikiza kutoka Hospitalini Gemelli. Amewaombea baraka kutoka kwa Mwenyezi Mung una pia ulinzi na tunza ya Bikira Maria.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Alhamisi tarehe 6 Machi 2025 majira ya usiku, Kardinali Ángel Fernández Artime, S.D.B., Mwenyekiti mwenza wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume, amewaongoza watu wa Mungu kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko ambaye kwa sasa amelazwa kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli iliyoko mjini Roma, tangu tarehe 14 Februari 2025. Kabla ya kuanza sala ya Rozari, Alhamisi tarehe 6 Machi 2025 Baba Mtakatifu Francisko kutoka katika sakafu ya mtima wake, amewashukuru waamini na watu wote wenye mapenzi mema, waliokuwa wamekusanyika kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu afya njema na kwamba, alikuwa anawasindikiza kutoka Hospitalini Gemelli. Amewaombea baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu na pia ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Ujumbe huu kwa njia ya sauti, umewatia moyo wa matumaini, waamini wanaoendelea kufuatilia hali ya afya ya Baba Mtakatifu Francisko. Taarifa rasmi kutoka kwa Dr. Matteo Bruno, Msemaji mkuu wa Vatican inaonesha kwamba, hali ya afya ya Baba Mtakatifu Francisko inaendelea kuimarika zaidi kwa kupumua kama kawaida pamoja na kuendelea na mazoezi ya kupumua kwa viungo bila mashine. Madaktari wanasema, pamoja na maendeleo haya makubwa, lakini hali ya afya ya Baba Mtakatifu inabaki kuwa ni tete. Ijumaa tarehe 7 Machi 2025, Baba Mtakatifu amefanya mazoezi, amesali na kupokea Ekaristi Takatifu pamoja na kuendelea kufanya kazi ndogo ndogo pamoja na mapumziko.

Imati mkubwa wa watu wa Mungu unamwombea Papa Afya Njema
Imati mkubwa wa watu wa Mungu unamwombea Papa Afya Njema   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Watu wa Mungu, Alhamisi tarehe 6 Machi 2025, kwa mara nyingine tena, walikusanyika kusali kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu kwa Bikira Maria Mama wa Kanisa na Mama wa shauri jema, liyebahatika kustahili kuwa ni Mama wa Mkombozi, kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. Katika maisha na utume wake, alijitahidi kutafuta na kuambata mapenzi ya Mungu katika maisha yake, akikuza rehema na kuendelea kushikamana na Kristo Yesu kwa karibu zaidi. Huyu ndiye Mama wa Kanisa; kimbilio na salama ya waamini.Kanisa linasadiki na kufundisha kuhusu Roho Mtakatifu, Bwana mleta uzima; atokaye kwa Baba na Mwana. Anayeabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana: aliyenena kwa vinywa vya Manabii. Roho Mtakatifu anatenda pamoja na Baba na Mwana kama inavyojidhihirisha katika kazi ya uumbaji. Roho Mtakatifu anatawala, anatakatifuza na kuhuisha viumbe vyote. Roho Mtakatifu ameendelea kutenda kazi katika historia ya ukombozi wa mwanadamu unaofumbata Roho wa Kristo katika utimilifu wa nyakati. Kwa namna ya pekee kabisa, Roho Mtakatifu anaonekana katika Fumbo la Umwilisho, kwa kumwandaa Bikira Maria kuwa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili. Mtakatifu Paulo katika Waraka wake wa kwanza kwa Wakorintho: 12:24 anaelezea kuhusu Karama za Roho Mtakatifu kwamba, kuna tofauti za karama, huduma na kutenda kazi, bali Roho ni yeye yule. Hapa kuna umoja na utofauti, kielelezo kwamba, Roho Mtakatifu ndiye anayeunganisha mambo kwa pamoja. Na kwa njia hii, Kanisa liliweza kuzaliwa. Kuna tofauti kubwa kati ya watu, lakini wote wanaunganishwa chini ya kifungo cha Roho Mtakatifu.

Roho Mtakatifu ni Bwana Mleta Uzima atokaye kwa Baba na Mwana.
Roho Mtakatifu ni Bwana Mleta Uzima atokaye kwa Baba na Mwana.

Baba Mtakatifu katika ujumbe wake kwa wakurugenzi wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa kwa mwaka 2020 alikazia: Umuhimu wa kuwashirikisha watu wa Mungu furaha ya Injili, kama mashuhuda wa zawadi ya imani. Wawe ni watu wenye mvuto kutokana na uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Mihimili ya uinjilishaji iwe ni kielelezo cha shukrani na sadaka inayosimikwa katika fadhila ya unyenyekevu. Wasaidie kurahisisha mambo na wala wasiyagumishe hata kidogo, daima wakijitahidi kuwa karibu na maisha ya waamini wanaowainjilisha kadiri ya hali na mazingira yao pamoja na kuzingatia ufahamu wa watu wa Mungu “Sensus fidei”. Wajitahidi kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.Kardinali Raniero Cantalamessa mhubiri mstaafu wa nyumba ya kipapa anasema: “Hawezi mtu kusema Yesu ni Bwana, isipokuwa katika Roho Mtakatifu”. (Rej. 1 Kor. 12: 3) Imani kwa Kristo Yesu inawezekana tu kwa njia ya Roho Mtakatifu na kwamba, kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, Mkristo anashirikishwa kwa karibu sana Fumbo la Utatu Mtakatifu. Ndiyo maana mahubiri ya Kwaresima kwa mwaka 2017 yalijikita zaidi katika Roho Mtakatifu “anayeabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana” Roho Mtakatifu ni sehemu ya mpango mzima wa Mungu katika ukombozi wa mwanadamu. Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, vyombo vya habari ndivyo vinavyotoa vipaumbele vya kushughulikiwa na mwanadamu katika ustawi na maendeleo yake. Kwa Kanisa, Roho Mtakatifu ndiye mleta uzima, atokaye kwa Baba na Mwana. Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walitoa dira na mwelekeo mpya katika maisha na utume wa Kanisa kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa Roho Mtakatifu anayeishi na kutenda kazi ndani ya Kanisa la Kristo.

Kardinali Raniero Cantalamessa
Kardinali Raniero Cantalamessa

Mwaka 2017, Chama cha Kitume cha Uhamsho wa Kikatoliki kiliadhimisha kumbukumbu ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwake. Hiki ni chama ambacho kimewagusa na kuwaunganisha mamilioni ya Wakatoliki sehemu mbalimbali za dunia. Kardinali Cantalamessa anakaza kusema, tafakari zake zinapenda kuonesha nafasi na dhamana ya Roho Mtakatifu katika maisha na utume wa Kanisa; maana ya maisha na hatima ya maisha ya binadamu mintarafu Fumbo la Pasaka yaani mateso, kifo na ufufuko wa Kristo. Roho Mtakatifu ndiye anayezima kiu cha maswali na udadisi wa binadamu kutoka katika undani wa maisha yake. Roho Mtakatifu anawasaidia waamini kuufahamu ukweli wote yaani: Yesu Kristo aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu, kiini cha imani ya Kanisa. Hii ni changamoto kwa waamini kutambua nafasi ya Roho Mtakatifu katika maisha, ili kuweza kumpatia kipaumbele cha kwanza. Roho Mtakatifu ni nguzo thabiti kwa wale wanaomwamini na kumtumaini katika maisha yao.Kardinali Cantalamessa katika mahojiano maalum na Gazeti la L’Osservatore Romano anasema, Roho Mtakatifu yuko daima katika maisha na utume wa Kanisa kama  Nafsi ya Tatu katika Fumbo la Utatu Mtakatifu, ndiye anayeabudiwa na kutukuzwa pamoja na Baba na Mwana. Roho Mtakatifu ni mfariji na wakili; ni Roho wa Kristo, Roho wa Bwana anayetambulika kama: Maji, Mpako, Moto, Wingu na nuru, Muhuri wa Baba wa milele, Mkono na kwamba, Roho Mtakatifu ni kidole cha Mungu na hua, alama ya amani, utulivu na utakaso. Waamini wanapewa changamoto na Mama Kanisa ya kumwalika daima Roho Mtakatifu katika maisha yao ya kila siku, ili awasaidie katika kufikiri, kutenda na kupenda zaidi. Roho Mtakatifu ni chemchemi ya upendo halisi anayeweza kunyeeshea pakavu pa maisha ya mwanadamu!

Shukrani za Papa
07 Machi 2025, 16:50