Papa amemteua Sr.Raffaella kuwa Rais wa Tume ya Kipapa ya Mji wa Vatican na Gavana wa Mji wa Vatican!
Vatican News.
Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi tarehe 15 Februari 2025, amemteua Sista Raffaella Petrini kuwa Rais mpya wa Tume ya Kipapa ya Mji wa Vatican na Gavana wa Mji wa Vatican.
Taarifa hiyo iliyotolewa na Ofisi ya Wanahabari mjini Vatican ambapo ilifahamisha kuwa uteuzi huo utaanza tangu tarehe 1 Machi 2025.
Sista Petrini, ni Mtawa wa Shirika la Masista Wafransiskani wa Ekaristi, na ambaye amekuwa akihudumu kama Katibu Mkuu wa mji wa Vatican, tangu mwaka 2021.
Kwa uteuzi huo, anakuwa mwanamke wa kwanza kushika nafasi ya juu kabisa ya uongozi ndani ya muundo wa utawala wa Vatican.
Katika nafasi yake mpya, atasimamia utawala wa Mji wa Vatican, huku pia akisimamia shughuli na sera zake za kila siku kadiri ya maagizo ya mji wa Vatican. Gavana anawajibika kwa nyanja mbalimbali za utawala wa Jiji la Vatican, ikiwa ni pamoja na usalama, miundombinu, na urithi wa kiutamaduni.
Mtangulizi wa nafasi hiyo ya Sr Petrini, ni Kardinali Fernando Vérgez Alzaga, L.C., ambaye amehudumu kama Gavana wa Mji wa Vatican tangu 2021.