杏MAP导航

Tafuta

2024.05.04 MISSIONARI CONSOLATA - MAROCCO - ALEX ZAPPALA'

Ujumbe wa Siku ya 99 ya Kimisionari 2025:Wamisionari wa Matumaini kati ya Watu wote!

“Wamisionari wa matumaini kati ya Watu wote”ndiyo kauli mbiu inayoongoza Ujumbe wa Baba Mtakatifu kwa ajili ya Siku ya 99 ya Kimisionari Ulimwenguni kwa 2025 uliochapishwa tarehe 6 Februari 2025.Ujumbe huo umegawanyika katika vipengele vitatu:"Katika nyayo za Kristo tumaini letu,"Wakristo,wabebaji na wajenzi wa matumaini kati ya watu wote"hatimaye"Kupyaisha utume wa matumaini."

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 6 Februari 2025, amechapisha Ujumbe wa Siku ya 99 ya Kimisionari Ulimwenguni inayotarajiwa kuadhimishwa mwezi Oktoba ijayo. Ujumbe unajikita katika mandhari ya Jubilei ya mwaka Mtakatifu ambao tayari ulianza tangu mkesha wa Noeli. Ufuatao ni ujumbe kamili wa Papa Francisko.

Kaka na dada wapendwa !

Katika Siku ya Utume wa Kimisinoari Ulimwenguni katika Mwaka wa Jubilei 2025, ujumbe mkuu ambao ni matumaini(taz.Spes Non Confundit, 1), nimechagua kauli mbiu: “Wamisionari wa Matumaini Kati ya Watu Wote.” Inawakumbusha Wakristo binafsi na Kanisa zima, jumuiya ya wabatizwa, juu ya wito wetu wa kimsingi wa kuwa, katika nyayo za Kristo, wajumbe na wajenzi wa matumaini. Ninatumaini kwamba itakuwa kwa kila mtu wakati wa neema pamoja na Mungu mwaminifu ambaye ametuzaa upya katika Kristo mfufuka “kwa tumaini lililo hai” (rej. 1 Pet 1:3-4). Hapa, ningependa kutaja baadhi ya vipengele vinavyohusika vya utambulisho wetu wa kimisionari wa Kikristo, ili tuweze kujiachia kuongozwa na Roho wa Mungu na kuwaka kwa bidii takatifu kwa ajili ya msimu mpya wa uinjilishaji katika Kanisa, ambao unatumwa kufufua matumaini katika ulimwengu ambao vivuli vya giza vinatanda (taz. Fratelli Tutti, 9-55).

1. Katika nyayo za Kristo tumaini letu

Kuadhimisha Jubilei ya Kawaida ya Milenia ya Tatu baada ya Mwaka Mtakatifu wa 2000, tunaweka mtazamo wa  Kristo, kitovu cha historia, "yeye jana na leo na hata milele" (Ebr 13:8). Katika sinagogi la Nazareti, Yesu alitangaza kwamba Maandiko yalitimizwa katika “leo” ya kuwapo kwake katika historia. Hivyo alidhihirisha kwamba yeye ndiye aliyetumwa na Baba kwa upako wa Roho Mtakatifu kutangaza Habari Njema ya Ufalme wa Mungu na kuzindua “mwaka wa neema ya Bwana” kwa wanadamu wote (rej. Lk 4:16-21). Katika fumbo la leo hii ambayo itadumu hadi mwisho wa dunia, Kristo ndiye utimilifu wa wokovu kwa wote, na kwa namna ya pekee kwa wale ambao tumaini lao pekee ni Mungu. Katika maisha yake ya kidunia, “alizunguka huko na huko akitenda mema na kuponya wote” kutoka kwa waovu na yule Mwovu (rej. Mdo. 10:38), akirudisha tumaini katika Mungu kwa wenye uhitaji na watu. Alipitia udhaifu wetu wote wa kibinadamu, isipokuwa ule wa dhambi, hata nyakati zile ngumu ambazo zingeweza kusababisha kukata tamaa, kama katika uchungu katika bustani ya Gethsemane na msalabani.

Yesu alitoa kila kitu kwa Mungu Baba, kwa utiifu akitumaini mpango wake wa kuokoa wanadamu, mpango wa amani kwa ajili ya wakati ujao uliojaa tumaini (rej. Yer 29:11). Kwa hiyo akawa Mmisionari wa kimungu wa matumaini, kielelezo kikuu cha wale wote katika karne zote ambao wanatekeleza utume wao wenyewe waliopewa na Mungu, hata katikati ya majaribu makali. Kupitia wanafunzi wake, waliotumwa kwa watu wote na kuandamana naye kwa fumbo, Bwana Yesu anaendelea na huduma yake ya matumaini kwa wanadamu. Bado anawainamia wale wote walio maskini, wanaoteseka, waliokata tamaa na waliokandamizwa, na kuwapaka “kwenye majeraha yao mafuta ya  faraja na divai ya matumaini”(Dibaji “Yesu Msamaria Mwema”).Kwa utiifu kwa Bwana na Mwalimu wake, na katika roho ile ile ya huduma, Kanisa, jumuiya ya wanafunzi wamisionari wa Kristo, linarefusha utume huo, likitoa maisha yake kwa ajili ya wote katikati ya mataifa.

Huku likikabiliwa na mateso, dhiki na matatizo, pamoja na kutokamilika kwake na kushindwa kwake kutokana na udhaifu wa washiriki wake, Kanisa daima linasukumwa na upendo wa Kristo kudumu katika muungano naye,  katika safari yake ya umisionari na kusikia, kama yeye na pamoja naye, ombi la wanadamu wanaoteseka na, kwa hakika, kuteseka kwa kila kiumbe kinachongojea ukombozi wa uhakika. Hili ndilo Kanisa ambalo Bwana daima na milele analiita kufuata nyayo zake: “si Kanisa tulivu, bali ni Kanisa la kimisionari linalotembea na Bwana wake katika mitaa ya ulimwengu”(Homilia katika Misa ya Kuhitimisha Mkutano Mkuu wa Kawaida wa Sinodi ya Maaskofu, 27 Oktoba 2024). Na sisi pia tujisikie kuvutiwa kuzifuata nyayo za Bwana Yesu ili tuwe, pamoja naye na ndani yake, ishara na wajumbe wa tumaini kwa wote, katika kila mahali na hali ambayo Mungu ametujalia kuishi. Na wote waliobatizwa, wakiwa wanafunzi wamisionari wa Kristo, wafanye tumaini lake litangazwe katika kila pembe ya dunia!

2. Wakristo, wabebaji na wajenzi wa matumaini kati ya watu wote

Katika kumfuata Kristo Bwana, Wakristo wanaalikwa kukabidhi Habari Njema kwa kushiriki hali halisi za maisha ya wale wanaokutana nao, na hivyo kuwa wabebaji na wajenzi wa matumaini. Hakika, “furaha na matumaini, huzuni na mahangaiko ya watu wa wakati wetu, hasa wale walio maskini au wanaoteseka, ni furaha na matumaini, huzuni na mahangaiko ya wafuasi wa Kristo pia. Hakuna kitu ambacho ni cha kibinadamu kiukweli kinachoshindwa kupata mwangwi katika mioyo yao”(Gaudium et Spes 1). Tamko hili adhimu la Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican unaodhihirisha hisia na mtindo wa Jumuiya za Kikristo katika kila zama, linaendelea kuwatia moyo washiriki wao na kuwasaidia kutembea na ndugu zao duniani.

Hapa ninawafikiria hasa wale ambao ni wamisionari (ad gentes) wa watu. Kufuatia mwito wa Bwana, wamekwenda kwa mataifa mengine ili kujulisha upendo wa Mungu katika Kristo. Kwa hili, ninawashukuru kwa moyo wote! Maisha yenu ni itikio la wazi kwa amri ya Kristo mfufuka, ambaye aliwatuma wanafunzi wake kuinjilisha mataifa yote (rej. Mt 28:18-20). Kwa njia hii, ninyi ni ishara za wito wa ulimwenguni pote kwa waliobatizwa kuwa, kwa uwezo wa Roho na juhudi za kila siku, wamisionari kati ya watu wote na mashuhuda wa tumaini kuu tulilopewa na Bwana Yesu. Upeo wa tumaini hili unapita mambo yanayopita ya ulimwengu huu na kufungua uhalisi huo wa kimungu ambao tunashiriki hata sasa. Hakika, kama Mtakatifu Paulo VI alivyoona, wokovu katika Kristo, ambao Kanisa hutoa kwa wote kama zawadi ya huruma ya Mungu, sio tu “kutopatana, kukidhi mahitaji ya kimwili au hata ya kiroho… kushikwa kabisa na tamaa za kimwili, matumaini, mambo, na mapambano. Badala yake, inavuka mipaka yote hiyo ili kufikia utimilifu katika ushirika na Mmoja Mkamilifu, ambaye ni Mungu. Ni wokovu unaovuka mipaka na wa kieskatologia, ambao kwa hakika una mwanzo wake katika maisha haya, lakini unatimizwa katika umilele” (Evangelii Nuntiandi, 27).

Kwa kuchochewa na tumaini hili kuu, jumuiya za Kikristo zinaweza kuwa vielelezo vya ubinadamu mpya katika ulimwengu ambao, katika maeneo "iliyoendelea" zaidi, unaonesha dalili kubwa za mgogoro wa kibinadamu: hali iliyoenea ya kuchanganyikiwa, upweke na kutojali mahitaji ya wazee, na kusitasita kufanya jitihada za kuwasaidia jirani zetu wenye shida. Katika mataifa yaliyoendelea zaidi kiteknolojia, "ukaribu" unatoweka: sote tumeunganishwa, lakini hatuhusiani. Kuzingatia ufanisi na kushikamana na vitu vya kimwili na matamanio kunatufanya tujijali na tushindwe kujitolea.  Injili, yenye uzoefu katika maisha ya jumuiya, inaweza kuturudisha katika ubinadamu mzima, wenye afya na uliokombolewa. Kwa sababu hii, kwa mara nyingine tena ninawaalika Ninyi nyote kutekeleza kazi zilizotajwa katika Hati ya Maelekezo ya  Jubile (Kifungu 7-15), tukiwa makini hasa kwa walio maskini na dhaifu zaidi, wagonjwa, wazee na wale waliotengwa na jamii ya kupenda mali na watumiaji hovyo. Na kufanya hivyo kwa "mtindo" wa Mungu: kwa ukaribu, huruma na upole, kukuza uhusiano wa kibinafsi na kaka na dada zetu katika hali zao maalum (taz. Evangelii Gaudium, 127-128). Mara nyingi wao ndiyo wanaotufundisha jinsi ya kuishi kwa matumaini.

Kupitia mawasiliano ya kibinafsi, pia tutawasilisha upendo wa moyo wa huruma wa Bwana. Tutakuja kutambua kwamba “moyo wa Kristo... ndiyo kiini hasa cha mahubiri ya awali ya Injili” (Dilexit Nos, 32). Kwa kuchota kutoka katika chanzo hiki, tunaweza kutoa kwa urahisi tumaini tulilopokea kutoka kwa Mungu (rej. 1 Pet 1:21) na kuwaletea wengine faraja ile ile ambayo tumefarijiwa nayo na Mungu (taz. 2Kor 1:3-4). Katika moyo wa kibinadamu na wa kimungu wa Yesu, Mungu anataka kuzungumza na moyo wa kila mwanamume na mwanamke, akituvuta sote kwa upendo wake.  “Tumetumwa kuendeleza utume huu: kuwa ishara za moyo wa Kristo na upendo wa Baba, tukikumbatia dunia nzima” (Hotuba kwa Washiriki wa Mkutano Mkuu wa Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa, 3 Juni 2023).

3. Kupyaisha utume wa matumaini

Kwa kukabiliwa na uharaka wa utume wa matumaini leo hii wanafunzi wa Kristo wanaitwa kwanza kugundua jinsi ya kuwa “mafundi” wa matumaini na warejeshaji wa ubinadamu ambao mara nyingi hukengeushwa na kukosa furaha. Kwa ajili hiyo, tunahitaji kufanywa upya katika hali ya kiroho ya Pasaka inayopatikana katika kila adhimisho la Ekaristi na hasa wakati wa Utatu wa Pasaka, kitovu na kilele cha mwaka wa kiliturujia. Tumebatizwa katika kifo cha ukombozi na ufufuko wa Kristo, katika Pasaka ya Bwana ambayo inaashiria majira ya milele ya historia. Kwa hiyo, sisi ni "watu wa majira ya kuchipua", tukiwa na matumaini ya kushirikishwa na wote, kwa kuwa katika Kristo "tunaamini na kujua kwamba kifo na chuki sio neno la mwisho" linalotamkwa juu ya kuwepo kwa mwanadamu (taz. Katekesi, 23 Agosti 2017). Kutokana na mafumbo ya Pasaka, yanayotolewa katika adhimisho la kiliturujia na katika sakramenti, daima tunachota nguvu za Roho Mtakatifu ili kufanya kazi kwa bidii, ari na subira katika nyanja pana ya uinjilishaji duniani.

“Kristo, aliyefufuka na kutukuzwa, ndiye chemchemi ya tumaini letu, na hatatunyimwa msaada tunaohitaji kutekeleza utume ambao ametukabidhi” (Evangelii Gaudium, 275). Ndani yake, tunaishi na kutoa ushuhuda kwa tumaini hilo takatifu ambalo ni “zawadi kutoka kwa Mungu na kazi kwa Wakristo” ( Hope is a Light in the Night, Vatican City 2024, 7). Wamisionari wa matumaini ni wanaume na wanawake wa sala, kwani “mtu anayetumaini ni mtu anayesali”, kwa maneno ya Mhashamu Kadinali François-Xavier Van Thuan ambaye  mwenyewe alidumishwa katika tumaini katika kipindi kirefu cha kifungo chake kutokana na nguvu alizopata kutokana na sala ya uaminifu na Ekaristi (taz. The Road of Hope, Boston, 2001, 963). Tusisahau kwamba maombi ndiyo shughuli ya msingi ya kimisionari na wakati huo huo “nguvu ya kwanza ya tumaini” (Katekesi, 20 Mei 2020).Kwa hiyo Tupyaishe utume wa matumaini, tukianzia kwenye maombi, hasa maombi yanayoegemezwa katika neno la Mungu na hasa Zaburi, ule wimbo mkuu wa sala ambao mtunzi wake ni Roho Mtakatifu (taz. Katekesi, 19 Juni 2024).  Zaburi hutufundisha kuwa na tumaini katikati ya dhiki, kutambua ishara za tumaini karibu nasi, na kuwa na hamu ya mara kwa mara ya "mmisionari" kwamba Mungu atukuzwe na watu wote (taz. Zab 41:12; 67:4). Kwa kusali, tunaweka cheche hai ya tumaini inayowashwa na Mungu ndani yetu, ili iweze kuwa moto mkubwa, unaowaangazia na kuwapa joto kila mtu anayetuzunguka, pia kwa vitendo na ishara zile thabiti ambazo sala yenyewe huchochea.

Kwa kuhitimisha, uinjilishaji daima ni mchakato wa kijumuiya, kama vile tumaini la Kikristo lenyewe (taz. Benedict XVI, Spe Salvi, 14). Mchakato huo hauishii kwa mahubiri ya awali ya Injili na Ubatizo, bali unaendelea na ujenzi wa jumuiya za Kikristo kwa kuandamana na kila mmoja wa wabatizwa katika njia ya Injili. Katika jamii ya kisasa, ushirika katika Kanisa kamwe haupatikani mara moja kwa wote. Ndiyo maana shughuli ya umisionari ya kukabidhi na kuchagiza imani iliyokomaa katika Kristo ni "mfano kwa shughuli zote za Kanisa" (Evangelii Gaudium, 15), kazi inayohitaji ushirika wa sala na matendo. Hapa ningesisitiza kwa mara nyingine tena umuhimu wa Sinodi hii ya kimisionari ya Kanisa, pamoja na huduma inayotolewa na Mashirika ya Kimisionari ya Kipapa katika kukuza wajibu wa kimisionari wa waliobatizwa na kusaidia Makanisa Maalum.

Ninawasihi ninyi nyote, watoto, vijana, watu wazima na wazee, kushiriki kikamilifu katika utume wa pamoja wa uinjilishaji wa Kanisa kwa ushuhuda wenu wa maisha na sala, kwa sadaka zenu na kwa ukarimu wenu. Asante kwa hili! Wapendwa dada na kaka, tumrudie Maria, Mama wa Yesu Kristo, tumaini letu. Kwake tunakabidhi maombi yetu kwa ajili ya Jubilei hii na kwa miaka ijayo: “Nuru ya tumaini la Kikristo na imuangazie kila mwanamume na mwanamke, kama ujumbe wa upendo wa Mungu unaoelekezwa kwa wote! Na Kanisa na litoe ushuhuda wa uaminifu kwa ujumbe huu katika kila sehemu ya ulimwengu!” (Hati ya  Spes Non Confundit, 6).

Ndiyo Ujumbe wa Baba Mtakatifu  Francisko uliotiwa sahini Roma katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yohane huko Leterano tarehe 25 Januari 2025 katika Siku kuu ya Uongofu wa Mtakatifu Paulo Mtume wa  Watu.

Ujumbe wa Siku ya 99 ya Kimisionari Ulimwenguni 2025.
06 Februari 2025, 13:02