Taarifa Kuhusu Afya ya Baba Mtakatifu Francisko
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko kwa sasa anasumbuliwa na ugonjwa wa mkamba (Bronchitis) uliopelekea kulazwa tangu Ijumaa tarehe 14 Februari 2025 kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli. Hadi sasa anaendelea vyema na matibabu na kwamba ameendelea kupokea Ekaristi Takatifu, kujisomea magazeti na nyaraka mbalimbali pamoja na kupata kifungua kinywa hali inayomwezesha kutekeleza walau kazi ndogo ndogo akiwa hospitalini hapo. Ijumaa jioni, 21 Februari 2025 Kikosi kazi cha madaktari wanaomtibu Baba Mtakatifu Francisko kutoka Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli kilizungumza na waandishi wa habari, mazungumzo ambayo yaliratibiwa na Dr Matteo Bruno, Msemaji mkuu wa Vatican; juma moja tangu Baba Mtakatifu alazwe hapo. Dalili za ugonjwa wa mkamba zilipoanza kujitokeza, Baba Mtakatifu mwenye umri wa miaka 88 alipatiwa matibabu ya awali kwenye Hosteli ya Mtakatifu Martha iliyoko mjini Vatican, wakisaidiana na madaktari binafsi wa Baba Mtakatifu. Hawa ni Daktari Luigi Carbone, Bwana Massililiano Strappeti pamoja na baadhi ya wauguzi. Ugonjwa wa mkamba ni wa kawaida kwa watu wengi hasa katika kipindi hiki, kiasi kwamba, vituo vya dharura nchini Italia vimefurika. Kumbe, huduma hii kwa Baba Mtakatifu ni jambo la kawaida kwa mtu mwenye umri wa miaka 88 kupatiwa mahali pa faragha kwa matibabu zaidi; matibabu yanayoyotolewa kwa ushirikiano mkubwa wa Kikosi kazi kinachoongozwa na Daktari Sergio Alfieri na kwamba, moyo wake uko safi na kwamba, Baba Mtakatifu amewataka madaktari wanaomuuguza kusema ukweli na kwamba, kile kinachoandikwa na madaktari hawa ni ukweli mtupu!
Ugonjwa huu wa mkamba unaomsumbua Baba Mtakatifu Francisko ni wa muda mrefu unaomfanya awe dhaifu.Baada ya kupimwa na madaktari wa moyo na mabingwa wa magonjwa ya kuambukiza, iliamriwa kwamba, Baba Mtakatifu alazwe kwa ajili ya kupata tiba muafaka. Baba Mtakatifu anajitambua kwamba, kwa sasa ni mgonjwa na mzee mwenye umri wa miaka 88 na kwamba, kuna wakati anapata shida ya kupumua, lakini akili inafanya kazi barabara. Kumbe, Baba Mtakatifu ataendelea kulazwa hospitalini Gemelli hadi pale madaktari watakapokuwa wameridhishwa na hali yake ya usalama. Baba Mtakatifu anaendelea kuonesha ucheshi kwa madaktari wanaomtibu. Dawa annazopewa Baba Mtakatifu zinafanya kazi kwa siku na hata nyingine zinahitaji juma zima ili kuweza kuona matokeo yake. Katika siku za hivi karibuni, kuna wakati Baba Mtakatifu alikosa hewa na hivyo kulazimika kusaidiwa kusoma sehemu ya hotuba zake. Kumbe, madaktari wakalazimika kumwanzishia matibabu maalum kutoka katika Hostel ya Mtakatifu Martha.
Hali ya Baba Mtakatifu inabaki kuwa ni tete, anajitahidi kusali, kujisomea na kufanya kazi ndogo ndogo. Kumbe, ataendelea kubaki hospitalini hapo hadi pale mahitaji ya kulazimika kupewa dawa hospitalini yatakapokoma. Atarejea Vatican, pale tu, hali yake itakapokuwa imetengemaa. Juma moja tangu alipolazwa, hali yake inaendelea kuimarika na kwamba, ameonesha kwamba, ni mgonjwa mtaratibu, mnyenyekevu na wala hana malalamiko hata kidogo. Ni kiongozi ambaye ametoa kipaumbele cha kwanza kwa Kanisa na wakati mwingine, amewaruhusu madaktari kumtibu akiwa kwenye Hosteli ya Mtakatifu Martha. Madaktari wanaweza kushauri, lakini utekelezaji wake ni maaamuzi yake binafsi, lakini anapaswa kuvuka hali hii kwa sasa. Dawa anazotumia Baba Mtakatifu hazijabadilika bali zimeimarishwa tu kadiri ya matokeo ya uchunguzi wanaomfanyia na kwamba afya yake inaendelea kuimarika taratibu taratibu na anaendelea kupumua na kula kama kawaida.
Si busara wala utu kuonesha picha ya Baba Mtakatifu Francisko akiwa amelazwa, lakini pale atakapokuwa tayari, picha zake zitaweza kuoneshwa. Huu ni mwaliko kwa waandishi wa habari kuandika ukweli na wala si “kuanza kupika majungu kama ilivyojitokeza kwa baadhi ya watu kuandika kwamba, walinzi wa Papa wameanza mazoezi ya kifo chake.” Baba Mtakatifu daima amejitahidi kuwa mkweli kwa afya yake, hata alipoanza kutembelea kwenye kiti cha wagonjwa, ameonekana wazi kabisa. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu katika ujana wake aliwahi kufanyiwa upasuaji mkubwa na hivyo kuondolewa pafu moja, hali ambayo imemlazimisha kutumia dawa nyingi ambazo kwa sasa zimemweka kwenye hatari ya kupata ugonjwa wa kisukari. Kikosi kazi cha madaktari wanaomtibu Baba Mtakatifu Francisko kutoka Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli, kiliwashukuru madakari na wauguzi wote wanaoendelea kumhudumia Baba Mtakatifu Francisko hospitalini hapo. Mkutano huu imekuwa pia ni fursa ya kumkumbuka na kumwombea Prof. Giovanni Scambia, mwenye umri wa miaka 65 mfano wa ubora wa utu na ubinadamu, mtaalam wa saratani ya wanawake aliyefariki dunia tarehe 21 Februari 2025 mjini Roma, baada ya kuugua kwa muda mfupi!