Rozari Takatifu Kwa Ajili ya Kumwombea Papa Francisko: Umuhimu Wa Sala
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican
Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro anakazia umuhimu wa waamini kushikamana na Kristo Yesu, ili waweze kuzaa matunda yanayokusudiwa yaani toba na wongofu wa ndani; ushuhuda wa imani tendaji inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya waamini. Kushikamana na Yesu kunafumbatwa katika maisha ya sala, huduma makini kwa wagonjwa na maskini pamoja na kukimbilia huruma na upendo wake unaobubujika kutoka katika Sakramenti ya Upatanisho. Sala haitaweza kuzaa matunda, ikiwa kama mwamini hajaungana kikamilifu na Kristo Yesu.Waamini wakikaa ndani ya Yesu na kuyashika maneno yake, wataweza kuwa kweli ni mfano bora wa kuigwa na jamii inayowazunguka. Kardinali Giovanni Battista Re katika tafakari yake kuhusu maadhimisho ya Jubilei ya miaka 100 tangu Bikira Maria alipowatokea Watoto wa Fatima: Francis, Yacinta Marto na Lucia dos Santos, tarehe 13 Mei 1917 na kujitambulisha kuwa ni Bikira Maria wa Rozari Takatifu aliwakabidhi watoto hawa ujumbe wa matumaini kwa binadamu wote, akiwataka wajizatiti katika kupambana na ubaya, kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kushuhudia imani kwa Kristo na Kanisa lake. Ikumbukwe kwamba, matukio ya Bikira Maria kuwatokea watu mbali mbali si sehemu ya ufunuo wa imani ya Kanisa kama inavyofundishwa katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa!
Matukio haya yanachukuliwa kuwa ni ufunuo binafsi wa Mama wa Mungu kwa baadhi ya watu. Kanisa limekuwa makini sana kuhusu matukio kama haya, lakini pia pale ambapo limejiridhisha, limeruhusu waamini kufanya Ibada na hija kwa Bikira Maria kama ilivyo kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Fatima, huko Ureno, yakabahatika kutembelewa na Mapapa wanne katika kipindi cha zaidi ya miaka 100 iliyopita! Matukio haya ni muhimu kwani yanawasaidia waamini kutambua utashi na mpango wa Mungu katika maisha yao! Daima wanahamasishwa kumpenda Mwenyezi Mungu na kuishi vyema Ukristo wao kwa kuzingatia Amri kumi za Mungu ambazo ni kanuni msingi za maisha, maadili na utu wema.Kardinali Giovanni Battista Re anasema, ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima unaweza kufupishwa kwa maneno makuu matatu: Sala, Toba na Wongofu wa ndani! Sala ni majadiliano ya kina kati ya mwamini na Muumba wake; majadiliano yanayomwongoza mwamini kuelekea katika maisha ya uzima wa milele. Waamini wanachangamotishwa na Mama Kanisa kutubu na kumwongokea Mwenyezi Mungu kwa kuwa na mwelekeo mpya katika maisha yao. Bikira Maria wa Fatima anawaalika waamini kuchuchumilia utakatifu na kuendelea kusali kwa ajili ya toba na wongofu wa ndani; kwa kujiweka wakfu kwa Moyo wake usiokuwa na doa! Bikira Maria anawaalika waamini kusali Rozari Takatifu ili kuombea amani duniani! Hii ni changamoto endelevu hata kwa watu wanaoishi katika ulimwengu mamboleo!
Ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima unafumbatwa kwa kiasi kikubwa katika Injili, kiasi kwamba, Fatima inakuwa ni shule ya imani na ushuhuda wa maisha ya Kikristo, na Bikira Maria ndiye Mwalimu wake mkuu! Anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa na imani kwa Kristo Yesu na kamwe wasikatishwe tamaa na Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia; majanga katika maisha ya watu; tawala za kifashisti na kikomunisti, tawala ambazo zimedhalilisha haki msingi, utu na heshima ya binadamu; kiasi hata cha kutaka kumng’oa Mungu katika maisha na vipaumbele vya waamini. Kilio cha waamini kilikuwa ni kumwomba Mwenyezi Mungu asimame mwenyewe na kujitetea! Ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima ulijikita zaidi katika Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia na Vita Kuu ya Pili ya Dunia; vita ambavyo vimesababisha madhara makubwa kwa maisha ya watu sehemu mbali mbali za dunia. Siri zote za Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima zikafunuliwa hadharani kunako Mwaka 2000 kwa kuonesha madhara makubwa yaliyosababishwa na Urusi kwa wakati ule kwa kupandikiza “ndago” za Ukanimungu; dhuluma, nyanyaso na mauaji ya kikatili dhidi ya Wakristo! Katika kipindi hiki cha utawala wa giza na chuki dhidi ya imani ya Kikristo, hapa kukaibuka makundi ya Wakristo waliosimama imara kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Jeuri ya maisha yao ya kiroho!
Mtakatifu Yohane Paulo II, kunako tarehe 13 Mei 1981 akiwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican akapigwa risasi katika jaribio la kutaka kumuua na kumfutilia mbali kutoka katika uso wa dunia! Lakini akasalimika na kwamba, huu ni muujiza wa pekee kabisa aliotendewa na Bikira Maria wa Fatima. Akaamuru hata ile Siri ya Tatu ya Fatima iwekwe hadharani! Ni siri ambayo ilionesha kwamba kulikuwa na mapambano makubwa dhidi ya Kanisa. Mtakatifu Yohane Paulo II akachukua risasi iliyotoka mwilini mwake na kuiweka kwenye taji ya nyota kumi na mbili zinazopamba kichwa cha Bikira Maria wa Fatima. Tarehe 25 Machi 1984 Mtakatifu Yohane Paulo II akauweka ulimwengu na kwa namna ya pekee kabisa, Urusi chini ya ulinzi na tunza ya Moyo Safi wa Bikira Maria. Kardinali Giovanni Battista Re anasema, Ujumbe wa Bikira Maria kwa Watoto wa Fatima ni endelevu hata kwa watu wa nyakati hizi kwani unafumbatwa katika Injili ya Kristo na Kanisa lake; Unahimiza Ibada kwa Bikira Maria, Toba, Wongofu wa ndani, Utakatifu wa maisha na umuhimu wa kusali Rozari Takatifu ili kuombea amani duniani. Waamini watambue daima kwamba, hata katika shida na mahangaiko yao, Mwenyezi Mungu daima yuko pamoja nao hadi utimilifu wa dahali! Bikira Maria anataka kuwaachia watoto wake, ujumbe wa matumaini, wokovu, amani na kwamba, Mwenyezi Mungu apewe kipaumbele cha kwanza katika maisha ya mwanadamu!
Kardinali Baldassare Reina, maarufu kama “Baldo”, Makamu Askofu wa Jimbo kuu la Roma, Alhamisi tarehe 27 Februari 2025 Usiku, ameongoza watu wa Mungu kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko ambaye kwa sasa anasumbuliwa na ugonjwa wa mkamba (Bronchitis) uliopelekea kulazwa tangu Ijumaa tarehe 14 Februari 2025 kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli iliyoko mjini Roma. Ibada hii imehudhuriwa na Makardinali wanaoishi mjini Roma, wafanyakazi wa Sekretarieti kuu ya Vatican na watu wa Mungu katika ujumla wao! Watu wa Mungu wametafakari mafumbo ya maisha na utume wa Kristo Yesu, kwa kujikita katika Matendo ya Mwanga Ili kwa maombezi ya Bikira Maria, waamini wajionee uwepo angavu wa upendo wa Kristo Yesu Mfufuka na ukaribu kutoka katika Jumuiya ya waamini. Ibada hii imeongozwa na “Sura ya Bikira Maria Mama wa Kanisa” ili kutafakari mafumbo ya Mwanga katika maisha na utume wa Kristo Yesu. Lengo la Sala hii ya Rozari Takatifu ni kumwombea Baba Mtakatifu ili aweze kupona haraka na hatimaye, kurejea tena kwenye maisha na utume wake. Huu ni mwendelezo wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, pamoja na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko, Ibada zinazofanywa sehemu mbalimbali za dunia.
Waamini wanakumbushwa kwamba, wao ni mahujaji wa matumaini na kwamba, Bikira Maria ni chemchemi ya matumaini. Waamini walikusanyika jioni hiyo kusali Rozari Takatifu sanjari na kutafakari mafumbo ya maisha na utume wa Kristo Yesu kwa macho ya Bikira Maria, Mama wa matumaini. Na habari zaidi kutoka kwa Dr Matteo Bruno, Msemaji mkuu wa Vatican zinaonesha kwamba, hali ya afya ya Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha Saa 24 zilizopita inaendelea kuimarika zaidi. Anaendelea na tiba ya Oksijeni na “ventimask.” Alhamisi tarehe 27 Februari 2025 amefanya mazoezi ya viungo katika mfumo wa hewa, amepumzika na wakati wa alasiri, alipata nafasi ya kusali na kutafakari, akapokea Ekaristi Takatifu na baadaye akazama kidogo katika shughuli ndogo ndogo hospitalini hapo. Taarifa ya Ijumaa tarehe 28 Februari 2025 inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko amepata usingizi mwanana na kwa sasa anaendelea na mapumziko.