Rozari Kwa Ajili ya Kumwombea Baba Mtakatifu Francisko: Mahujaji wa Matumaini
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko amesema kwamba, Bikira Maria ni Mama wa matumaini, anayewasaidia waamini kuangalia mbali zaidi, huku wakiwa na matumaini, hususan katika kipindi hiki cha: Vita, Majanga asilia, Athari za Mabadiliko ya Tabianchi, Magonjwa, Njaa na Umaskini. Lakini kwa njia ya imani, matumaini na mapendo, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaweza kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu. Katika hija hii ya matumaini, Baba Mtakatifu anawashauri mahujaji kumsihi Bikira Maria ili aweze kuwaombea kwa Mwanaye mpendwa Kristo Yesu, ujasiri wa kukabiliana na matatizo na changamoto mamboleo. Kanisa linaendelea kujipambanua katika majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi, ili kuamsha dhamiri nyofu miongoni mwa raia, wanasiasa na Wakristo katika ujumla wao. Leo hii, Mama Kanisa anaendelea kujikita katika ujenzi wa Kanisa la Kisinodi na Kimisionari; na Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo. Matukio yote haya ni fursa kwa watu wa Mungu kuweza kukutana na hatimaye, kuambata huruma na upendo wa Mungu, tayari kupambana na changamoto za umaskini wa: elimu, ajira, makazi na mmong’onyoko wa tunu msingi za kimaadili na utu wema. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu kujielekeza zaidi katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaosimikwa katika: haki na amani; Ukweli na uzima; Utakatifu na neema tayari kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini kwa wale waliovunjika na kupondeka moyo. Baba Mtakatifu katika hotuba yake kwenye Kongamano la Jimbo kuu la Roma lililofanyika hivi karibuni alijikita zaidi katika ukosefu wa usawa na mifumo mipya ya umaskini unaoendelea kujitokeza; wito kwa watu wa Mungu ni kuwatangazia maskini Habari Njema ya Wokovu, kwa sababu maskini ni sehemu ya vinasaba na Sakramenti ya Kanisa; wanapaswa kupewa kipaumbele katika maisha na utume wa Kanisa sanjari na kujenga mshikamano wa upendo unaojikita katika majadiliano, tayari kupandikiza mbegu ya matumaini kwa watu waliovunjika na kupondeka moyo.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, takwimu na shuhuda zinaonesha kwamba bado kunakosekana usawa na kwamba, mifumo mipya ya umaskini inaendelea kuwapekenya watu wa Mungu. Kuna watu wanaoishi katika hali na mazingira magumu, kiasi hata cha kukosa makazi maalum na matokeo yake wanaishi barabarani. Kuna vijana ambao wanashindwa kupata ajira na makazi; kuna wazee na wagonjwa wanaoelemewa na upweke hasi. Kuna kundi kubwa la vijana walioathirika kutokana na matumizi haramu ya dawa za kulevya na ulevi wa kupindukia, kiasi kwamba, idadi ya waathirika wa magonjwa ya afya ya akili inaendelea kuongezeka maradufu. Kuna wagonjwa ambao hawana bima ya afya na hivyo hawawezi kupata tiba mahali popote pale. Kumbe, hawa si idadi bali ni ndugu na jamaa wanaoteseka na kunyanyasika kutokana na mifumo mbalimbali ya umaskini mamboleo. Hawa ni sehemu ya Madonda Matakatifu ya Kristo Yesu, mwaliko kwa waamini kuyaangalia na kuyatafakari kwa kina. Kumbe, huu ni wito na mwaliko kwa waamini kujizatiti katika kuwatangazia maskini Habari Njema ya Wokovu, kwa sababu hawa ni sehemu muhimu sana ya Mwili wa Kristo na ni kama Sakramenti inayoonekana kwa macho matupu! Hawa wanapaswa kuhudumiwa kwa moyo wa ukarimu na upendo; watambue kwamba, Kristo Yesu anawapenda upeo! Utu, heshima na haki zao msingi ni mambo yanayopaswa kulindwa na kuendelezwa.
Baba Mtakatifu alitumia fursa hii, kuwashukuru na kuwapongeza watu mbalimbali wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwa hali na mali. Huduma hii inapaswa kuwa ni wajibu shirikishi kwa watu wote. Kwa upande wa Mama Kanisa, anaitwa na kutumwa, ili kuhakikisha kwamba, maskini wanapewa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wake, ili kuwaonjesha huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka. Kanisa linapenda kuwahakikishia maskini ukarimu, huruma na upendo wa Mungu kwao.Baba Mtakatifu anawaalika watu wa Mungu Jimbo kuu la Roma kuangalia tena mtindo wao wa maisha; kwa kujenga mtandao wa mshikamano ili utu, heshima na haki msingi za binadamu zipewe kipaumbele cha kwanza na hivyo kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangiko ya jirani. Huu ni mchakato wa majadiliano katika ukweli na uwazi na taasisi mbalimbali, tayari kupyaisha mafungamano ya kijamii yanayowahusisha na kuwashirikisha watu wote wa Mungu. Huu ni wakati wa kufikiri na kutenda, kwani maneno matupu hayavunji mfupa! Kuna haja ya kukazia tena na tena malezi na majiundo juu ya Mafundisho Jamii ya Kanisa, ili Injili iweze kumwilishwa katika medani mbalimbali za maisha, ili hatimaye, waamini waweze kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani na udugu wa kibinadamu. Huu ni ujenzi wa mtandao wa mshikamano wa kijamii, ili kujenga na kudumisha umoja.
Mafundisho Jamii ya Kanisa yanapata chimbuko lake mintarafu kanuni na muundo wa elimu fahamu, taalimungu, hususan taalimungu maadili ambayo ni dira na mwongozo wa maisha ya watu. Mafundisho haya yanachota amana na utajiri wake kutoka katika Maandiko Matakatifu na Mapokeo ya Kanisa na imani thabiti ambayo inamwilisha Neno la Mungu katika matendo, kielelezo cha imani tendaji. Mambo msingi katika mchakato wa kudumisha haki msingi za binadamu: Amani katika ukweli, haki, upendo na uhuru. Hizi ni tunu ambazo ni urithi mkubwa kwa binadamu wote kwani zinabubujika kutoka katika asili ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu hivyo zinapaswa kulindwa, kutetewa na kuheshimiwa na wote; kwa kuzingatia kwamba, haki inakwenda sanjari na wajibu; hakuna haki pasi na wajibu. Hii ni haki ya kuishi, kupata huduma bora ya makazi, afya, elimu, kuabudu, uhuru wa dhamiri, uhuru wa kuchagua mfumo wa maisha; haki za kiuchumi na kisiasa pamoja na uhuru wa kwenda unakotaka kwa kuzingatia sheria na kanuni zilizopo. Kanisa Katoliki lina amana na utajiri mkubwa wa Mafundisho Jamii ya Kanisa yanayopata chimbuko lake katika Waraka wa Kichungaji wa Baba Mtakatifu Leo XIII; Mambo Mapya; “Rerum Novarum.” Baba Mtakatifu Francisko anasema, kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, waamini wanapaswa kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini, huruma na mapendo kama walivyokuwa akina Don Di Liegro, aliyekuwa Mkurugenzi wa Caritas Roma. Lakini pia kuna umati mkubwa wa watu wa Mungu wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini na watu wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huu ni mwaliko kwa waamini kuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya matumaini, dhamana na wajibu wa mshikamano wa kijamii. Watu wa Mungu wathubutu kuwa ni vyombo vya huruma na upendo wa Mungu, ili kuendelea kuwa waaminifu katika imani na watendaji katika upendo.
Kardinali Giovanni Battista Re, Dekano wa Baraza la Makardinali Jumatano tarehe 26 Februari 2025 Usiku, ameongoza watu wa Mungu kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko ambaye kwa sasa anasumbuliwa na ugonjwa wa mkamba (Bronchitis) uliopelekea kulazwa tangu Ijumaa tarehe 14 Februari 2025 kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli iliyoko mjini Roma. Ibada hii imehudhuriwa na Makardinali wanaoishi mjini Roma, wafanyakazi wa Sekretarieti kuu ya Vatican na watu wa Mungu katika ujumla wao! Watu wa Mungu wametafakari mafumbo ya maisha na utume wa Kristo Yesu, kwa kujikita katika Matendo ya furaha Ili kwa maombezi ya Bikira Maria, waamini wajionee uwepo angavu wa upendo wa Kristo Yesu Mfufuka na ukaribu kutoka katika Jumuiya ya waamini. Ibada hii imeongozwa na “Sura ya Bikira Maria Mama wa Kanisa” ili kutafakari mafumbo ya utukufu katika maisha na utume wa Kristo Yesu. Lengo la Sala hii ya Rozari Takatifu ni kumwombea Baba Mtakatifu ili aweze kupona haraka na hatimaye, kurejea tena kwenye maisha na utume wake. Huu ni mwendelezo wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, pamoja na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko, Ibada zinazofanywa sehemu mbalimbali za dunia. Waamini wanakumbushwa kwamba, wao ni mahujaji wa matumaini na kwamba, Bikira Maria ni chemchemi ya matumaini. Waamini walikusanyika jioni hiyo kusali Rozari Takatifu sanjari na kutafakari mafumbo ya maisha na utume wa Kristo Yesu kwa macho ya Bikira Maria, Mama wa matumaini.
Kanisa zima linasali kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko afya njema, ili kwamba, Bikira Maria, Mama wa Kanisa amsaidie na kumwombea wakati huu anapokabiliana na changamoto ya afya. Wamini wametafakari mafumbo ya uutukufu, kwa kuwa na uhakika kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ndiye tumaini la Wakristo.Na habari zaidi kutoka kwa Dr Matteo Bruno, Msemaji mkuu wa Vatican zinaonesha kwamba, hali ya afya ya Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha Saa 24 zilizopita inaendelea kuimarika taratibu na kwamba vipimo mbalimbali vinaonesha matumaini ingawa tatizo la figo kushindwa kufanya kazi yake barabara ni jambo ambalo bado linawatia wasiwasi madaktari wake ingwa kwa sasa limetoweka. Baba Mtakatifu anaendelea kupumua kwa kutumia mirija. Jopo la Madaktari wanaomtibu Baba Mtakatifu Francisko linasema, hali yake ya afya bado inaendelea kuwa tete. Jumatatu jioni, tarehe 25 Februari 2025 Baba Mtakatifu alifanyiwa kipimo cha “CT Scan” kifuani ili kufuatilia ugonjwa wa mkamba unaomsumbua na kwamba, kipimo kinaonesha bado kuna uvimbe kwenye mapafu. Baba Mtakatifu asubuhi tarehe 27 Februari 2025 baada ya kupokea Ekaristi Takatifu aliendelea kufanya kazi ndogo ndogo hospitalini hapo! Taarifa ya Alhamisi 27 Februari 2025 inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko amepata usingizi mwanana na kwa sasa anaendelea na mapumziko.