杏MAP导航

Tafuta

Ibada hii imeongozwa na sura ya Bikira Maria Mama wa Kanisa: Matendo ya uchungu. Ibada hii imeongozwa na sura ya Bikira Maria Mama wa Kanisa: Matendo ya uchungu.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Rozari Takatifu Kwa Ajili ya Kumwombea Papa Francisko: Mafumbo ya Uchungu

Lengo la Sala hii ni kumwombea Baba Mtakatifu Francisko ili aweze kupona haraka na hatimaye, kurejea tena kwenye maisha na utume wake. Huu ni mwendelezo wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, pamoja na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko, Ibada zinazofanywa sehemu mbalimbali za dunia. Jumatatu Baba Mtakatifu mefanyiwa kipimo cha "CT Scan", Amepokea Ekaristi na Kufanya kazi ndogo ndogo hapo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema nguvu ya kuinjilisha ya matendo ya kiibada ya waamini wengi ni njia muafaka inayojenga na kudumisha vifungo vya urafiki na udugu wa kibinadamu kati ya watu wa Mungu na hivyo kukua na kuimarishana, kama sehemu ya uinjilishaji. Matendo haya ya kiibada huwawezesha waamini kuona jinsi ambavyo imani ikishapokelewa, hujumuishwa katika utamaduni na daima kurithishwa na kwamba, hii ni nguvu ya kimisionari na kielelezo cha maisha ya kitaalimungu yanayorutubishwa kwa kazi ya Roho Mtakatifu aliyemiminwa ndani ya roho zao Rej. Rum 5:5. Bikira Maria ni wakili mwaminifu anayeingilia kati na kuleta ufumbuzi wa kudumu kama ilivyokuwa kwenye Harusi ya Kana ya Galilaya. Baba Mtakatifu anasema, Bikira Maria ni Mama anayewaelekeza waamini kujenga na kudumisha urafiki wa kijamii kati ya watu wa Mataifa, ili waweze kumfuasa na kuonana na Uso wa Kristo Yesu, tayari kujikita katika njia ya amani, utu wema, usikivu na majadiliano yanayosimikwa katika uvumilifu na imani. Bikira Maria anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumwilisha ndani mwao udugu wa kibinadamu, tayari kujenga ulimwengu mpya unaowawezesha watu wote kujisikia kuwa ni ndugu wamoja, wanaoheshimiana na kuthaminiana; katika ulimwengu ambamo haki na amani vinang’ara na kushamiri. Bikira Maria: Nyota ya Uinjilishaji mpya na Mama wa uinjilishaji awashike mkono na kuwasaidia kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, utume na zawadi wanayopaswa kuitekeleza.

Watu wengi wameitikia mwaliko wa kusali Rozari kwa ajili ya Papa Francisko
Watu wengi wameitikia mwaliko wa kusali Rozari kwa ajili ya Papa Francisko   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Ili kuwa Wakristo kweli, waamini hawana budi kuwa na Ibada kwa Bikira Maria, kwa kutambua mambo msingi yanayounganisha maisha ya Bikira Maria na Kristo Yesu. Kwa kusali Rozari Takatifu, Injili ya Kristo inaendelea kutangazwa na kumwilishwa katika maisha, watu, familia na katika ulimwengu mzima! Baba Mtakatifu anawaalika waamini kufanya hija pamoja na Bikira Maria, Mwalimu mkuu katika maisha ya kiroho, aliyethubutu kumfuasa Kristo katika Njia ya Msalaba, akabarikiwa kwa kuwa aliamini! Anawaonya waamini kutomkimbilia Bikira Maria kwa kutaka awafanyie miujiza ya “chapuchapu”, kwani Bikira Maria wa Injili anayeheshimiwa na Kanisa ni yule anayeangalia mambo msingi, anayewaombea watoto wake huruma ya Mungu ili hatimaye, kukutana na Hakimu mwenye haki, yaani Mwana kondoo wa Mungu aliyechinjwa kwa ajili ya ukombozi wa mwanadamu!

Waamini wanaalikwa kukimbilia huruma na upendo wa Mungu
Waamini wanaalikwa kukimbilia huruma na upendo wa Mungu   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Mwenyezi Mungu ni mwingi wa huruma na mapendo anasema Baba Mtakatifu, mwaliko kwa waamini kukimbilia upendo na huruma ya Mungu badala ya kuogopa hukumu yake kwa kutambua kwamba, huruma ya Mungu kamwe haiwezi kuondoa haki! Yesu aliteswa na kufa Msalabani ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la utumwa wa dhambi na mauti. Kwa njia ya imani inayowaunganisha katika Msalaba wa Kristo, wamekombolea na hivyo kuwekwa huru, kumbe hakuna sababu ya kuwa na woga, bali kukimbilia na kuambata upendo wake. Bikira Maria ni kielelezo cha mapinduzi ya wema na upendo wa Mungu kwa binadamu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Bikira Maria anaonesha kwamba unyenyekevu na upole si fadhila ya wanyonge bali ni fadhila ya watu wenye nguvu ambao hawana sababu ya kuwatendea wengine ubaya ili kuonekana kuwa ni watu wa maana sana. Mwingiliano wa haki na upole, wa taamuli na kujali mahitaji ya wengine ndiyo inayolifanya Kanisa limtazame Bikira Maria kama mfano bora wa uinjilishaji.

Bikira Maria Mama wa Kanisa awe ni faraja kwa wote wanaoteseka
Bikira Maria Mama wa Kanisa awe ni faraja kwa wote wanaoteseka   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Baba Mtakatifu Francisko anawaalika waamini wote kuiga mfano wa Bikira Maria, ili waweze kuwa ni alama na Sakramenti ya upendo na huruma ya Mungu anayesamehe yote! Kwa kushikamana na Bikira Maria, wote wanaweza kuimba upendo na huruma ya Mungu kwani ni huruma ambayo amewakirimia watakatifu na watu wake waaminifu imeweza kuwafikia wengine wote. Kwa njia ya kiburi cha binadamu na uchu wa malimwengu, binadamu ameshindwa kutimiza hamu ya moyo wake! Njia pekee ya kuweza kuinuka tena ni kwa njia ya Bikira Maria kumshika mkono na kumfunika kwa joho ili kumweka pembeni wa Moyo wake usiokuwa na doa! Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, Mwenyekiti Mwenza wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, Jumanne tarehe 25 Februari 2025 ameongoza watu wa Mungu kusali Rozari Takatifu kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko ambaye kwa sasa anasumbuliwa na ugonjwa wa mkamba (Bronchitis) uliopelekea kulazwa tangu Ijumaa tarehe 14 Februari 2025 kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli iliyoko mjini Roma.

Bikira Maria ni kielelezo cha imani na fadhila
Bikira Maria ni kielelezo cha imani na fadhila   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Ibada hii imehudhuriwa na Makardinali wanaoishi mjini Roma, wafanyakazi wa Sekretarieti kuu ya Vatican na watu wa Mungu katika ujumla wao! Watu wa Mungu wametafakari mafumbo ya maisha na utume wa Kristo Yesu, kwa kujikita katika Matendo ya Uchungu. Ili kwa maombezi ya Bikira Maria, waamini wajionee uwepo angavu wa upendo wa Kristo Yesu Mfufuka na ukaribu kutoka katika Jumuiya ya waamini. Ibada hii imeongozwa na “Sura ya Bikira Maria Mama wa Kanisa” ili kutafakari mafumbo ya uchungu katika maisha na utume wa Kristo Yesu. Lengo la Sala hii ya Rozari Takatifu ni kumwombea Baba Mtakatifu ili aweze kupona haraka na hatimaye, kurejea tena kwenye maisha na utume wake. Huu ni mwendelezo wa maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, pamoja na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu kwa ajili ya kumwombea Baba Mtakatifu Francisko, Ibada zinazofanywa sehemu mbalimbali za dunia.

Baba Mtakatifu Francisko ana ibada kubwa kwa Bikira Maria
Baba Mtakatifu Francisko ana ibada kubwa kwa Bikira Maria   (Vatican Media)

Na habari zaidi kutoka kwa Dr Matteo Bruno, Msemaji mkuu wa Vatican zinaonesha kwamba, hali ya afya ya Baba Mtakatifu Francisko inaendelea kuimarika taratibu na kwamba vipimo mbalimbali vinaonesha matumaini ingawa tatizo la figo kushindwa kufanya kazi yake barabara ni jambo linalowatia wasiwasi madaktari. Baba Mtakatifu anaendelea kupumua kwa kutumia mirija. Jopo la Madaktari wanaomtibu Baba Mtakatifu Francisko linasema, hali yake ya afya bado inaendelea kuwa tete. Jumatatu jioni, tarehe 25 Februari 2025 Baba Mtakatifu amefanyiwa kipimo cha “CT Scan” ili kufuatilia ugonjwa wa mkamba unaomsumbua. Baba Mtakatifu asubuhi baada ya kupokea Ekaristi Takatifu aliendelea kufanya kazi ndogo ndogo hospitalini hapo! Taarifa ya Jumatano tarehe 26 Februari 2025 inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu Frabcisko amepata usingizi mwanana na kwa sasa anaendelea na mapumziko.

Matendo ya Uchungu
26 Februari 2025, 08:00