Papa na wakunga wa Calabria:kuongeza taaluma,usikivu wa kibinadamu na sala!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko tarehe 6 febbraio 2025 alikutana katika Nyumba ya Mtakatifu Marta mjini Vatican na ujumbe kutoka Catanzaro, Cosenza, Crotone na Vibo Valentia. Katika Ujumbe wake aliowakabidhi wajisomee, Papa anaonesha furaha sana kuwakaribisha, wakunga, madaktari wa magonjwa ya wanawake na wahudumu wa afya kutoka Calabria. Taaluma yao ni nzuri, wito na wimbo wa maisha, muhimu zaidi katika wakati huu wa kihistoria. Kiukweli, nchini Italia, na katika nchi nyingine pia, shauku ya umama na ubaba inaonekana imepotea; wanaonekana kuwa chanzo cha matatizo na usumbufu, badala ya kuwa ni ufunguzi wa upeo mpya wa ubunifu na furaha. Papa amebainisha hata hivyo katika hilo kuwa: “tunajua inategemea sana muktadha wa kijamii na kiutamaduni.” Kwa sababu hiyo, wao kama shirika la kitaaluma, wamejipa lengo la kiprogramu: kubadilisha mwelekeo wa kushuka kwa viwango vya kuzaliwa. Papa anawapongeza kuwa wamefanya vizuri! Na kwa hivyo alipenda kutafakari nao juu ya sehemu tatu zinazokamilishana na zinazotegemeana za maisha yao na utume wao: taaluma, usikivu wa kibinadamu na, kwa wale wanaoamini, sala.
Kwanza: taaluma. Uboreshaji unaoendelea wa ujuzi siyo sehemu ya kanuni zao za maadili tu, bali pia njia ya utakatifu wa walei. Umahiri ndiyo zana ambayo wanaweza kutumia vyema upendo waliyokabidhiwa, kwa kusindikizana wale mama wa baadaye na katika kushughulika na hali ngumu na uchungu. Katika matukio haya yote, kuwepo kwa wataalamu waliofunzwa kunatoa utulivu na, katika hali mbaya zaidi, kunaweza kuokoa maisha.
Pili: unyeti wa kibinadamu. Katika wakati muhimu maishani kama vile kuzaliwa kwa mwana au binti, mtu anaweza kuhisi hatari, udhaifu, na kwa hivyo wanahitaji ukaribu, huruma, joto. Katika hali kama hizo, ni vizuri sana kuwa na watu nyeti na maridadi wa karibunao. Kwa hiyo Papa alipendekeza kwamba wakuze, pamoja na uwezo wa kitaaluma, “hisia kubwa ya ubinadamu, ambayo inathibitisha katika nafsi za wazazi shauku na furaha ya maisha mapya, yaliyochanuliwa kutoka katika upendo wao." (Makatifu Yohane Paulo II, Hotuba kwa wakunga, tarehe 26 Januari 1980) na inachangia "kuhakikisha mtoto anazaliwa mwenye afya na furaha."
Jambo la tatu: sala. Baba Mtakatifu anabainisha kuwa “hii dawa iliyofichika lakini yenye ufanisi ambayo wale wanaoamini wanayo, kwa sababu inaponya roho. Wakati mwingine itawezekana kushiriki na wagonjwa; katika hali nyingine, inaweza kutolewa kwa Mungu kwa busara na unyenyekevu, katika moyo wa mtu, kuheshimu imani na njia ya wote. Hata hivyo, maombi yatasaidia daima kuimarisha huo“ushirikiano wa kupendeza kati ya wazazi, asili na Mungu, ambamo mwanadamu mpya anakuja kuonekana katika sura na mfano wa Muumba”, kama Papa Pio XII alivyosema (Hotuba kwa Umoja wa Wakunga wa Kikatoliki Italia, 29 Oktoba 1951). Kwa hiyo Papa anawatia moyo wajisikie wajibu kwa akina mama, baba na watoto ambao Mungu ameweka katika njia zao, kuwaombea pia, hasa katika Misa Takatifu, katika Kuabudu Ekaristi na katika sala rahisi ya kila siku. Papa amewashukuru tena kwa mema yote wanayofanya kila siku! Waendelea kutekeleza utume wao kwa ari na ukarimu. Anawabariki wote kwa kazi zao na familia zao. Anawaombea na tafadhali nao wasisahau kumuombe pia.