Papa kwa Talitha Kum:Jamii isiwe na sintofahamu ya janga la biashara haramu ya binadamu
Na Angella Rwezaua – Vatican.
Ijumaa tarehe 7 Februari 2025, Baba Mtakatifu Francisko amekutana na Wawakilishi wa Mtandao wa Talitha Kum, katika Nyumba ya Mtakatifu Marta mjini Vatican, katika fursa ya Siku ya XI sala na Tafakari dhidi ya Bishara haramu ya Binadamu, ifanyikayo kila tarehe 8 Februari kila mwaka, sanjari na Kumbukizi ya Mtakatifu Josephine Bakhita, mwathirika wa utumwa. Katika hotuba yake Papa Francisko amekuwa na furaha ya kukutana na kuungana nao ambao kila siku wako katika jitihada dhidi ya Biashara haramu ya watu. Ameshukuru kwa namna ya pekee Mtandao huo wa Kimataifa wa Talitha Kumu kwa huduma yao wanayojikita nayo.
Papa alisema “Tunajikuta katika mkesha wa Siku Kuu ya Mtakatifu Josephine Bakhita, ambaye alikuwa mwathirika wa janga hili lisilosemekana la kijamii. Historia yake inatupatia nguvu, kwa kutuonesha jinsi gani licha ya ukosefu wa haki na mateso yanayopatikana, kwa neema ya Bwana inawezekana kuvunja minyororo, kurudi katika huru na kugeuka kuwa watangazaji wa matumaini kwa wengine walio katika matatizo.” “Biashara mbaya ya binadamu ni tukio la kiulimwengu linalopandikiza mamilioni ya waathriwa na halisimami mbele ya kitu chochote,” alisema Papa na kwamba “ Daima linapata mitindo mipya kwa ajili ya udanganyifu katika jamii zetu, na kila aina ya kona. Mbele ya janga hilo hatuwezi kuwa na sintofahamu na kama wao wafanyavyo, lazima kuunganisha nguvu zetu,sauti zetu na kutoa mwaliko kwa wote wa uwajibikaji, ili kuweza kukomesha mitindo hii ya kihalifu ambayo inapata faida kubwa juu ya ngozi za watu walio katika mazingira hatarishi.
Baba Mtakatifu Francisko amekazia kusema kuwa “Hatuwezi kukubali kwamba dada wengi na kaka wengi wananyonywa kwa namna hiyo ya kuchukiza. Biashara ya miili, unyonyaji wa kingono, hata watoto wa kike na kiume, kazi za suruba ni aibu na ukiukaji mkubwa wa haki msingi za kibinadamu.” Papa Francisko anatambua jinsi mtandao huo wa Talitha Kum walivyo kundi la kimataifa, na baadhi yao wamefika kutoka mbali sana kwa ajili ya Juma hili la sala na Tafakari dhidi ya biashara haramu ya binadamu. Kwa njia hiyo, anawashukuru! Kwa namna ya pekee anawapongea vijana mabalozi dhidi ya biashara haramu ambao kwa ubunifu na nguvu daima wanatafuta mitindo mipya kwa ajili ya kuhamasisha na kuelimisha.
Papa anawatia moyo kila shirika katika mtandao huo, na kwa wote binafsi, ambao wanashiriki na kuendelea kuunganisha nguvu, kwa kuwaweka katikati waathriiwa na wahanga, kuwasikiliza historia zao, kwa kutunza majeraha yao na kuongeza sauti zao. Hiyo ina maana ya kuwa mabalozi wa matumaini; na ni matumaini ya Papa kuwa Jubilei hii, watu wengine wengi wanataweza kufuata mfano wao. Alihitimisha kwa kuwabariki na kwamba anawasindikiza katika sala. Na wao pia wamwombee.