杏MAP导航

Tafuta

Papa,Katekesi ya Jubilei 2025:Kutumaini ni kubadilika.Maria Magdala!

Katika katekesi ya Pili kuhusu Jubilei 2025,Baba Mtakatifu Francisko amesisitiza juu ya mabadiliko kwa mtazamo wa ndoto ya Mungu na kwamba mabadiliko ya mwelekeo yanazaliwa kutokana na kukutana na Yesu Kristo.Kwa kumtazama Yeye tunaingia katika ndoto ya Mungu na katika matumaini.Papa amefafanua juu ya Mfano wa Maria Mgdalena kama mtume wa mitume.

Na Angella Rwezaula – Vatican.

Katika mzunguko wa Katekesi kama sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo ambayo Papa Francisko alianzisha tarehe 11 Januari 2025 yenye kauli mbiu hiyo hiyo ya "Mahujajii wa Matumaini," tarehe 1 Februari 2025, katekesi yake kwa waamini na mahujaji waliokusanyika katika Ukumbi wa Paulo VI imejikita na mada: “Kutumaini ni kubadilika: Maria Magdalena.” Awali ya yote ilisomwa Injili ya Yohane kifungi kisemacho:  “Alipokwisha kusema hayo, (Maria Magdalena) akageuka akamwona Yesu pale, lakini hakujua ya kuwa ni Yesu. Yesu akamwambia, “Mwanamke, kwa nini unalia? Unamtafuta nani?” Akafikiri ni mtunza bustani, akamwambia, “Bwana, ikiwa umemchukua, niambie ulipomweka, nami nitamchukua.” Yesu akamwambia, "Maria!" Akageuka, akamwambia kwa Kiebrania, Rabbouni, maana yake, Mwalimu(Yh 20,14-16).

Papa akisalimia waamini na mahujaji
Papa akisalimia waamini na mahujaji   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Baba Mtakatifu Francisko  bada ya Injili alianza kusema kuwa: “Ndugu wapendwa kaka na dada, Jubilei kwa ajili ya watu na kwa Dunia ni mwanzo mpya; ni wakati ambapo kila kitu lazima kifikiriwe upya ndani ya ndoto ya Mungu. Na tunajua kwamba neno "uongofu" linaonesha mabadiliko ya mwelekeo. Kila kitu kinaweza kuonekana, hatimaye, kutoka katika mtazamo mwingine, na hivyo hatua zetu pia huenda kuelekea malengo mapya. Hivi ndivyo tumaini, ambalo halikatishi tamaa, hutokea.” Baba Mtakatifu Francisko amekazia kusema kuwa “Biblia inaeleza jambo hilo kwa njia nyingi. Na kwetu sisi pia, uzoefu wa imani umechochewa na kukutana na watu ambao wameweza kubadilika katika maisha na wakaingia katika ndoto za Mungu. Kwa maana ingawa kuna maovu mengi ulimwenguni, tunaweza kutofautisha ni nani aliye tofauti: ukuu wao, ambao mara nyingi hupatana na udogo, hutushinda.”

Katika Injili, sura ya Maria Magdalena inasimama juu ya wengine wote kwa hili. Yesu alimponya kwa huruma (rej. Lk 8:2), naye akabadilika: kwa njia hiyo Papa amesisitiza kuwa “kaka na dada huruma hubadilisha moyo, na kwa upande wa Maria Magdalena, huruma hiyo ilimleta katika ndoto za Mungu na kutoa kusudi jipya kwa ajili ya safari yake. Injili ya Yohane inasimulia juu ya kukutana kwake na Yesu Mfufuka kwa njia inayotufanya tufikiri. Inarudiwa mara kadhaa kwamba Maria aligeuka. Mwinjili anachagua maneno yake vizuri! Kwa machozi, Maria anatazama kwanza ndani ya kaburi, kisha anageuka: Aliyefufuka hayuko upande wa kifo, bali yuko upande wa maisha. Anaweza kudhaniwa kuwa mmoja wa watu tunaokutana nao kila siku. Kisha, anaposikia jina lake likitajwa, Injili inasema tena Maria anageuka. Na hivi ndivyo tumaini lake linakua na kwa muda huo analiona kaburi, lakini sio kama hapo awali. Anaweza kukausha machozi yake, kwa sababu amesikia jina lake mwenyewe: Mwalimu pekee ndiye anayetamka kwa njia hii.”

Waamini na mahujaji
Waamini na mahujaji   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Baba Mtakatifu Francisko alisema: “Ulimwengu wa zamani bado unaonekana kuwapo, lakini haupo tena. Tunapohisi kwamba Roho Mtakatifu anatenda ndani ya mioyo yetu, na tunahisi kwamba Bwana anatuita kwa jina, je, tunajua jinsi ya kutofautisha sauti ya Bwana?”  Kwa njia hiyo Msisitizo wa Papa ni kwamba, kutoka kwa Maria Magdalena, ambaye utamaduni unamwita "mtume wa mitume", tunajifunza matumaini. Mtu huingia katika ulimwengu mpya kwa kubadilika zaidi ya mara moja. Safari yetu ni mwaliko wa mara kwa mara wa kubadili mtazamo. Yule Mfufuka anatupeleka katika ulimwengu Wake, hatua kwa hatua, kwa sharti kwamba hatudai kujua kila kitu tayari. Hebu tujiulize leo: Je, ninajua jinsi ya kugeuka ili kuona mambo kwa njia tofauti, kwa mtazamo tofauti? Je, nina hamu ya uongofu? Kujiamini kupita kiasi na kuwa na kiburi hutuzuia kumtambua Yesu Mfufuka.

Papa akisalimia mahujaji
Papa akisalimia mahujaji   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Hata tunapolia na kukata tamaa, tunampa kisogo. Badala ya kutazama katika giza la zamani, ndani ya utupu wa kaburi, kutoka kwa Maria Magdalena tunajifunza kugeuka kuelekea maisha. Hapo Bwana wetu anatungoja. Hapo jina letu linatajwa. Kwa maana katika maisha halisi kuna nafasi kwa ajili yetu, na daima na kila mahali. Kuna nafsi  kwako, kwangu, na kwa kila mtu.” Papa aliongeza kusema kuwa  “Hakuna mtu anayeweza kuichukua, kwa sababu imekuwa ikikusudiwa sisi kila wakati. Ni mbaya, kama wasemavyo katika lugha ya kawaida, ni mbaya kuacha kiti tupu ukisema kuwa hapa ni nafasi yangu, je usipokwenda...”. Kila mtu anaweza kusema: Nina nafasi, mimi ni mtume! Kwa njia hyo Papa amewashauri mahujaji na waamini kufikiria juu ya hilo kwamba je mahali pangu ni wapi? Je, ni utume gani ambao Bwana anatupatia? Wazo hili na litusaidie kuwa na mtazamo wa ujasiri maishani.” Alihitimisha Papa Francisko.

Katekesi ya Papa Jumamosi 1 Februari 2025

 

01 Februari 2025, 13:54