Papa Fransisko:Wakristo waungane tena katika kanuni moja ya Imani ya Nikea
Na Angella Rwezaula – vatican.
Katika Hotuba ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Washiriki wa ziara ya Mafunzo ya Vijana Mapadre na Watawa ya Makanisa ya Kiorthodox ya Mashariki tarehe 6 Februari 2025 , alisema: “Jinsi ilivyo vyema na kupendeza wakati ndugu wanaishi pamoja kwa umoja!” (Zab 133:1 ). Kwa maneno haya ya mtunga Zaburi, ndiyo aliyowakaribisha kwa furaha kwa ziara hiyo ya mapadre vijana na watawa wa Makanisa ya Kiarmenia, Kikoptic, Ethiopia, Eritrea, Malankara na Waorthodox wa Mashariki ya Syria. Salamu kwa Askofu Mkuu Khajag Barsamian na kwa Askofu Barnabas El-Soryani, waliowasindikiza. Kupitia kwao alipenda pia, kuwasalimu wakuu wa Makanisa ya Kiorthodox ya Mashariki.
Hiyo ni Ziara ya tano ya Mafunzo kwa mapadre na watawa vijana wa Mashariki iliyoandaliwa na Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Kikristo. Ziara kama hizo za Mapadre wa Kikatoliki zimetayarishwa na Kanisa Katoliki la Armenia la Etchmiadzin na Kanisa la Kiorthodox la Syria la Malankara. Papa aliwashukuru sana kwa ubadilishanaji wa zawadi unaohamasishwa na Tume ya Pamoja ya Kimataifa ya Mazungumzo ya Kitaalimungu kati ya Kanisa Katoliki na Makanisa ya Kiorthodox ya Mashariki, kwa sababu wanawezesha mazungumzo ya upendo kwenda sambamba na mazungumzo ya ukweli.
Ziara yao ina umuhimu wa kipekee mwaka huu, tunapoadhimisha miaka 1700 ya Mtaguso wa Nikea, Baraza la kwanza la kiekumene, lililojitangaza kuwa ni Ishara ya Imani inayoshirikishwa na Wakristo wote. Papa alisema “Ningependa, basi, kutafakari na ninyi juu ya neno hilo, "ishara", ambayo katika maana yake yenye pande tatu, ina maana kubwa ya kiekumene. Katika maana ya kitaalimungu, ishara huweka mkusanyo wa kweli kuu za imani ya Kikristo, ambazo zinakamilishana kwa mapatano. Kwa maana hii, Imani ya Nikea, ambayo inaweka wazi siri ya wokovu wetu kwa njia ya kisanaa, ni ya kielelezo na isiyo na kifani. Ishara hii pia ina umuhimu wa kikanisa. Sio tu kwamba inaunganisha ukweli, pia inaunganisha waamini. Zamani, neno la Kigiriki ishara lilionesha nusu ya hati iliyovunjwa vipande viwili, ili kuwasilishwa kama ishara ya utambulisho. Kwa hivyo ishara hii hutumika kama ishara ya utambulisho na ushirika kati ya waamini.”
Papa Francisko aidha alisema kuwa “Kila mtu ana imani kama "ishara", ambayo hupata umoja wake kamili pamoja na wengine. Tunahitajiana sisi kwa sisi ili tuweze kukiri imani moja. Ndiyo maana Ishara ya Nikea, katika toleo lake la asili, inatumia umbo la wingi, “Tunaamini”. Nikiibeba taswira hii hatua zaidi, ningesema kwamba sisi Wakristo, tungali tumegawanyika, ni kama “vipande” ambavyo lazima turudishe umoja katika kukiri imani moja. Kwa maana tunashikilia Ishara ya imani yetu kama hazina katika vyombo vya udongo (taz. 2Kor 4:7).” Baba Mtakatifu akiendelea alisisitiza kuwa kwa hivyo, tunafikia maana ya tatu ya ishara, umuhimu wake wa kiroho. Hatupaswi kamwe kusahau kwamba Imani ni juu ya sala zote za sifa zinazotuunganisha na Mungu: muungano na Mungu lazima ufanyike kupitia umoja kati yetu Wakristo tunaokiri imani sawa.
Ingawa shetani anagawanyika, ishara inaungana! Ingekuwa jambo zuri kama nini ikiwa, kila wakati tunapokiri Imani, tulihisi kuunganishwa na Wakristo wa mapokeo yote! Utangazaji wa imani yetu sote, kiukweli, unahitaji kabla ya yote tupendane, kama liturujia ya Mashariki inavyotusihi tufanye kabla ya kukariri Imani: “Na tupendane sisi kwa sisi, ili katika umoja wa roho tukiri imani yetu katika Baba, na Mwana, na Roho Mtakatifu.” Ni matumaini ya Papa kwamba uwepo wao utakuwa mfano wa ushirika wetu unaoonekana, tunapodumu katika kutafuta umoja kamili ambao Bwana Yesu alitamani sana (taz. Y 17:21). “Ninawahakikishia maombi yangu kwa kila mmoja wenu na kwa Makanisa yenu, na ninategemea maombi yenu wenyewe kwa ajili yangu na kwa ajili ya huduma yangu. Bwana awabariki na Mama wa Mungu awalinde. Na sasa, ningependekeza kwamba tusali kwa pamoja sala ya Imani ya Nikea, kila mmoja wetu katika lugha yake mwenyewe." Walihitimisha kwa Sali na Papa.