Papa Francisko:Maria hakuogopa hukumu bali alisukumwa na upendo wa kusaidia wengine!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Katika mzunguko wa Katekesi kuhusu Jubilei 2025 inayoongozwa na mada ya: Yesu Kristo Matumaini yetu:” Utoto wa Yesu, Jumatano tarehe 5 Februari, kwa waamini na mahujaji waliokusanyika katika Ukumbi wa Paulo VI mjini Vatican, mada ya nne ni “Na heri aliyeamini (Lk 1,45). Ziara ya Maria na wimbo wa Sifa(Magnificat). Kabla ya Katekesi hiyo imesoma Injili ya Luka 1,39-42) isemayo: “Basi, Maria akaondoka siku hizo, akaenda hata nchi ya milimani kwa haraka mpaka mji mmoja wa Yuda. Akaingia nyumbani kwa Zakaria akamwamkia Elisabeti. Ikawa Elisabeti aliposikia kule kuamkia kwake Maria, kitoto kichanga kikaruka ndani ya tumbo lake; Elisabeti akajazwa Roho Mtakatifu; akapaza sauti kwa nguvu akasema, Umebarikiwa wewe katika wanawake, naye mzao wa tumbo lako amebarikiwa.”
Kwa njia hiyo Baba Mtakatifu alimkabidhi usomaji wa katekesi yake kwa Padre Pierluigi Giroli, Mkuu wa Ofisi ya Sekretarieti ya Vatican ambapo Papa alisema: “Nataka kuomba samahani kwa sababu ya baridi na mafua inaniwia vigumu kuzungumza.” Katika andiko la tafakari yake, Papa amejikita kufafanua sura ya Maria kwamba “Leo tunatafakari uzuri wa Yesu Kristo tumaini letu katika fumbo la Ziara. Bikira Maria alimtembelea Mtakatifu Elizabeth; lakini juu ya yote ni Yesu, akiwa tumboni mwa mama yake, ambaye huwatembelea watu wake ( Lk 1:68), kama Zakaria asemavyo katika wimbo wake wa sifa. Baada ya mshangao na kustaajabu kwa yale ambayo Malaika alikuwa amemtangazia, Maria aliinuka na kuanza safari yake, kama wale wote wanaoitwa katika Biblia, kwa sababu "kitendo pekee ambacho mwanadamu anaweza kupatana na Mungu anayejidhihirisha ni kile cha kupatikana bila kikomo" (H.U. von Balthasar, Vocazione, Rome 2002, 29).
Binti huyo mdogo wa Israeli hakuchagua kujikinga na ulimwengu, hakugopa hatari na hukumu za wengine, bali alikwenda nje kukutana na wengine. Unapohisi kupendwa, unapata nguvu inayoweka upendo katika mzunguko; kama mtume Paulo asemavyo, “upendo wa Kristo hutusukuma sisi” (2 Kor 5:14). Maria alihisi msukumo wa upendo na akaenda kumsaidia mwanamke ambaye ni ndugu yake, lakini pia ni mwanamke mzee ambaye alikaribisha, baada ya kusubiri kwa muda mrefu,ujauzito usiyotarajiwa, ambao ni vigumu kukabiliana na umri wake. Lakini Bikira pia alikwenda kwa Elizabeti ili kushirikisha imani yake katika Mungu wa mambo yasiyowezekana na tumaini lake katika utimizo wa ahadi zake.
Mkutano kati ya wanawake hao wawili una matokeo ya kushangaza: sauti ya "mwenye neema nyingi" anayesalimia Elizabeti inachochea unabii katika mtoto ambaye mwanamke mzee hubeba ndani ya tumbo lake na kuamsha ndani yake baraka mbili: "Umebarikiwa wewe katika wanawake, na mzao wa tumbo lako amebarikiwa!" ( Lk 1:42 ). Na pia heri: "Heri yeye aliyeamini kwamba yatatimizwa yale aliyoambiwa na Bwana" (Lk 1, 45). Akiwa amekabiliwa na utambuzi wa utambulisho wa kimasiha wa Mwanawe na utume wake kama mama, Maria hakuwa juu yake mwenyewe bali juu ya Mungu na alitoa sifa iliyojaa imani, matumaini na furaha, wimbo unaovuma kila siku katika Kanisa wakati wa sala ya Masifu ya jioni: Magnificat (Lk 1:46-55).
Sifa hii kwa Mungu anayeokoa, inayobubujika kutoka moyoni mwa mtumishi wake mnyenyekevu, ni ukumbusho mzito unaofupisha na kutimiza maombi ya Israeli. Imefumwa kwa sauti za kibiblia, ishara kwamba Maria hataki kuimba "nje ya sauti" bali kuungana na baba, akiinua huruma yake kwa wanyenyekevu, wale wadogo ambao Yesu katika mahubiri yake atatangaza "heri"(Mt 5: 1-12). Uwepo mkubwa wa sababu za Pasaka pia unaifanya (Magnificat) yaani Sifa, kuwa wimbo wa ukombozi, ambao una kumbukumbu ya ukombozi wa Israeli kutoka Misri. Vitenzi vyote viko katika wakati uliopita, vilivyojaa kumbukumbu ya upendo ambayo huangaza sasa kwa imani na kuangaza wakati ujao kwa matumaini: Maria aliimba juu ya neema ya wakati uliopita lakini ni mwanamke wa sasa ambaye amebeba wakati ujao katika tumbo lake.
Sehemu ya kwanza ya wimbo huu inasifu kitendo cha Mungu katika Maria, kiumbe mdogo ambaye yeye hujifafanua ndani yake mwenyewe kwa watu wa Mungu ambao wanashikamana kikamilifu na agano (Lk 1, 46-50); safu ya pili ni juu ya kazi ya Baba katika udogo wa historia ya watoto wake (Lk 1, 51-55), kupitia maneno matatu muhimu: kumbukumbu ya rehema na ahadi. Bwana, ambaye aliinama juu ya Maria mdogo ili kutimiza "mambo makubwa" ndani yake na kumfanya kuwa mama wa Bwana, alianza kuokoa watu wake kuanzia katika Kutoka, akikumbuka baraka ya ulimwengu wote iliyoahidiwa kwa Ibrahimu (rej. Mwa 12:1-3).
Bwana, Mungu ni mwaminifu milele, amefanya mtiririko usiokatizwa wa upendo wa rehema “kutoka kizazi hata kizazi” (Lk 1,50) juu ya watu waaminifu kwa agano, na sasa anadhihirisha utimilifu wa wokovu katika Mwana wake, aliyetumwa kuwaokoa watu kutoka katika dhambi zao. Kuanzia kwa Ibrahimu hadi kwa Yesu Kristo na jumuiya ya waamini, Pasaka kwa hiyo inaonekana kama kitengo cha kuelewa kila ukombozi unaofuata, hadi ule uliopatikana na Masiha katika utimilifu wa wakati. Kwa njia hiyo Papa ameomba kuwa leo hii tumwombe Bwana neema ya kuweza kusubiri utimilifu wa kila ahadi yake; na kutusaidia kukaribisha uwepo wa Maria katika maisha yetu. Kwa kufuata mfano wake, sote tunaweza kugundua kwamba kila nafsi inayoamini na kutumaini “huchukua mimba na kuzalisha Neno la Mungu”(Mtakafu Ambrose, katika ufafanuzi wa Injili ya Luka 2, 26).