Papa kwa washiriki wa kozi ya kiliturujia:Liturujia inagusa maisha ya watu wa Mungu&inawafunulia asili ya kweli ya kiroho
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Kutoka Hospitali ya Gemelli ambako amelazwa tangu Februari 14 na anaendelea na shughuli zake, Baba Mtakatifu Francisko, aliwatumia ujumbe washiriki wa Kozi ya Kimataifa ya Mafunzo, wahusika wa maadhimisho ya kiliturujia ya kiaskofu iliyofanyika mjini Roma, kuanzia tarehe 24 hadi 28 Februari 2025, kwenye Ukumbi mmojawapo wa Mtakatifu Anselmi na kuwashauri wasidharau furaha na mateso, ndoto na mahangaiko ya watu wa Mungu, kwa sababu wana thamani ya kimafundisho, na kupendekeza kuhamasisha mtindo wa kiliturujia unaoonesha ufuasi wa Yesu huku wakiepuka fahari au kimbele mbele kisicho cha lazima. Liturujia lazima ipate mwili, kukuzwa kwa sababu inaelezea imani ya Kanisa, inagusa maisha ya watu wa Mungu na inawafunulia asili yao ya kweli ya kiroho. Baba Mtakatifu awali ya yote anamsalimu Baba Abate Mkuu na Rais wa Taasisi ya Kiliturujia ya Kipapa, pamoja na maprofesa na wanafunzi waliofuatilia toleo hilo la pili la kozi wanaohusika na maadhimisho ya kiliturujia ya kiaskofu.
Ni furaha yake Papa kutambua kwamba kwa mara nyingine tena wamekubali mwaliko ulio katika Waraka wake wa Kitume “Desiderio desideravi,” kuhusu Majiundo ya Kiliturujia ya Watu wa Mungu, na kwamba wakiendelea “kujifunza Liturujia, si tu kwa mtazamo wa kitaalimungu, bali pia katika muktadha wa hatua ya mazoezi ya maadhimisho. Baba Mtakatifu Francisko anakazia kusema kuwa katika “Mwelekeo huo unagusa maisha ya watu wa Mungu na kuwafunulia asili yao ya kweli ya kiroho (taz Katiba ya Lumen Gentium, 9). Kwa hiyo, “mtu anayehusika na sherehe za kiliturujia si mwalimu wa taalimungu tu; yeye siyo mwandishi ambaye anatumia sheria; yeye si sacristan, ambaye huandaa kile kinachohitajika kwa ajili ya maadhimisho. Yeye ni mwalimu aliyewekwa kwenye huduma ya sala ya jumuiya. Huku akifundisha kwa unyenyekevu sanaa ya kiliturujia, hana budi kuwaongoza wale wote wanaoadhimisha, akiweka alama ya mdundo wa ibada na kuwasindikiza waamini katika tukio la sakramenti.
Kama mwalimu kiongozi, anayepanga kila adhimisho kwa hekima, kwa manufaa ya kusanyiko; anatafsiri katika kanuni za kitaalimungu zinazooneshwa katika vitabu vya kiliturujia katika mazoezi ya sherehe; na kumuunga mkono na kumsaidia Askofu katika nafasi yake kama mhamasishaji na msimamizi wa maisha ya kiliturujia (rej. Caeremoniale Episcoporum, 9). Akisaidiwa hivyo, mchungaji anaweza kuongoza kwa upole jumuiya nzima ya jimbo katika kujitoa kwa Baba, kwa kumwiga Kristo Bwana.” Baba Mtakatifu Francisko kwa washiriki hao, amekazia kufafanua kuwa kila Jimbo linamtazama Askofu na Kanisa Kuu kama kuiga mifano ya kusherehekea. Kwa hivyo Papa amewasihi “kupendekeza na kukuza mtindo wa kiliturujia unaoonesha ufuasi wa Yesu huku ukiepuka fahari au uhusika ukuu(protagonism) usiyo wa lazima. Pia Papa amewaalika, “wafanye huduma yao kwa kwa busara, bila kujivunia matokeo ya utumishi wao. Anawatia moyo kupeleka mitazamo hiyo kwa wahudumu wa madhabahu, wasomaji na waimbaji, kulingana na maneno ya Zaburi 115 yaliyonukuliwa katika Dibaji ya Kanuni ya Wabenediktini isemayo: “Si kwetu, Ee Bwana, si kwetu, bali kwa jina lako ulipe utukufu” (rej. Zab 115, 29-30).Katika kazi zao zote, wasisahau kwamba utunzaji wa liturujia ni huduma ya kwanza kabisa kwa sala, ambayo ni, kukutana na Bwana.
Katika kumtangaza Mtakatifu Teresa wa Avila kuwa Mwalimu wa Kanisa, Mtakatifu Paulo VI alifafanua uzoefu wake wa fumbo kuwa ni upendo ambao unakuwa mwanga na hekima: hekima ya mambo ya kimungu na mambo ya kibinadamu (rej.Homelia ya tarehe 27 Septemba 1970). Mwalimu huyu mkuu wa maisha ya kiroho na awe kielelezo kwao: kwa hakika, kuandaa na kuongoza sherehe za kiliturujia kunamaanisha kuchanganya hekima ya kimungu na hekima ya kibinadamu. Kwanza hupatikana kwa kuomba na kutafakari kwa kina; pili inatokana na kujifunza, kwa jitihada ya kutafakari kwa kina zaidi, na kutokana na uwezo wa kijiweka katika kusikiliza. Ili kuweza kufanikiwa katika kazi hizo, Baba Mtakatifu anawashauri kuwa na mtazamo wao unaowalekeza watu, ambao Askofu ni mchungaji na baba yao: hii itawasaidia kuelewa mahitaji ya waamini, pamoja na mitindo na mbinu za kuhimiza ushiriki wao katika tendo la liturujia. Kwa kuwa kuabudu ni kazi ya kusanyiko zima, kukutana kati ya mafundisho na huduma ya kichungaji si mbinu ya hiari, bali ni kipengele cha msingi cha liturujia, ambacho kinapaswa kumwilishwa kila mara, kukuzwa, kudhihirisha imani ya Kanisa.
Baba Mtakatifu Francisko amekazia kusisitiza kwa njia hiyo kuwa, furaha na mateso, ndoto na mahangaiko ya watu wa Mungu yana thamani ya kihemenetiki ambayo hatuwezi kuipuuza (taz. Ujumbe wa Video kwa Kongamano la Kimataifa la Taalimungu huko U.C.A., Buenos Aires, 1-3 Septemba 2015). Katika suala hilo, Papa Francisko alipeenda kukumbuka kile alichoandika rais wa kwanza wa Taasisi ya Kipapa ya Liturujia, Abate wa Mbenediktini Salvatore Marsili. Ilikuwa ni mwaka 1964: kwa kuona mbali yeye alikuwa akiwaalika kufahamu ujumbe wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, katika nuru ambayo uchungaji wa kweli hauwezekani bila liturujia, kwa sababu liturujia ndiyo kilele ambacho utendaji wote wa Kanisa unaelekea (taz. S. Marsili, Mageuzi ya juu ya kiliturujia jarida la Kiliturujia 1964, kifungu 71-781). Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa kuwaalika kufanya maneno hayo kuwa mtazamo wa kimsingi wa huduma yao na matumaini kwamba kila mmoja wao atakuwa daima na moyoni mwa watu wa Mungu, ambao wanasindikizana nao katika ibada kwa hekima na upendo. Na wasisahau kumuombea.