杏MAP导航

Tafuta

Jubilei ya mwaka Mtakatifu 2025, mahujaji wa matumaini. Jubilei ya mwaka Mtakatifu 2025, mahujaji wa matumaini.  (Vatican Media)

Papa Francisko:kama Mamajusi katika njia ya Kristo,tumaini la watu wote

Katekesi ambayo Baba Mtakatifu alipaswa kuifanya tarehe 19 Februari 2025 katika Ukumbi wa Paul VI na ambayo ilifutwa kutokana na kulazwa kwake hospitali ya Gemelli imechapishwa. Katika andiko hilo,kama sehemu ya mzunguko wa katekesi za Jubilei kuhusu:Yesu Kristo tumaini letu,anaendeleza tafakari kuhusu:“watu wenye hekima waliokuja kutoka Mashariki(Mamajusi) ili kumwabudu Mwana wa Mungu,watu wanaojua kutazama zaidi ya wao wenyewe na wanaojua kutazama juu.”

Vatican News

Ofisi ya Vyombo vya Habari vya Vatican imechapisha Katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko iliyotayarishwa kwa ajili ya Katekesi yake ya Jumatano tarehe 19 Februari 2025, na ambayo haikufanyika kutokana na kulazwa kwa Papa katika Hospitali ya A. Gemelli. Tunachapishwa Tafakari hii  kama sehemu ya mzunguko wa Jubilei 2025: "Yesu Kristo tumaini letu. Utoto wa Yesu" na kwa kupendekeza  tafakari ya: "Ziara ya Mamajusi kwa Mfalme aliyezaliwa."

Kaka na dada  katika Injili za utoto wa Yesu kuna kipindi ambacho ni maalum kwa simulizi la Mathayo: ziara ya Mamajusi. Wakiwa wamevutiwa na kuonekana kwa nyota, ambayo katika tamaduni nyingi ni ishara ya kuzaliwa kwa watu wa kipekee, watu wengine wenye busara walitoka Mashariki, bila kujua wanakwenda wapi. Hawa ni Mamajusi, watu ambao si wa watu wa agano. Mara ya mwisho tulizungumza juu ya wachungaji wa Bethlehemu, waliotengwa katika jamii ya Kiyahudi kwa sababu walionekana kuwa "wachafu"; Leo hii tunakutana na jamii nyingine, wageni, ambao wanakuja mara moja kutoa heshima kwa Mwana wa Mungu ambaye aliingia katika historia na ufalme mpya kabisa.

Kwa hiyo Injili zinatuambia waziwazi kwamba maskini na wageni ni miongoni mwa watu wa kwanza kukutana na Mungu aliyefanywa mtoto, Mwokozi wa ulimwengu. Mamajusi wamezingatiwa kama wawakilishi wa jamii zote mbili za mwanzo, zilizotolewa na watoto watatu wa Nuhu, na wa mabara matatu yaliyojulikana zamani: Asia, Afrika na Ulaya, na wa hatua tatu za maisha ya mwanadamu: ujana, ukomavu na uzee. Zaidi ya tafsiri yoyote iwezekanayo, wao ni watu ambao hawatulii tuli lakini, kama waitwao wakuu wa historia ya Biblia, wanahisi mwaliko wa kuhama, kuanza safari. Ni watu ambao wanajua jinsi ya kuangalia zaidi ya wao wenyewe, ambao wanajua jinsi ya kutazama juu. Mvuto wa nyota iliyochomoza angani,  uliwaweka kwenye njia yao hadi nchi ya Yuda, hadi Yerusalemu, ambapo walikutana na Mfalme Herode.

Ujinga wao na tumaini lao la kutaka habari juu ya mfalme mchanga wa Wayahudi wanakutanana werevu wa Herode, ambaye, akifadhaika na woga wa kupoteza kiti chake cha enzi, mara moja alijaribu kuona waziwazi, akiwasiliana na waandishi na kuwaomba wachunguze. Nguvu ya mtawala wa kidunia hivyo inaonesha udhaifu wake wote. Wataalamu wanajua Maandiko na kumwambia mfalme mahali ambapo, kulingana na unabii wa Mika, kiongozi na mchungaji wa watu wa Israeli angezaliwa (Mika 5:1): Bethlehemu uliye ndogo na si Yerusalemu kubwa! Kwa hakika, kama vile Paulo anavyowakumbusha Wakorintho, “Mungu alichagua kile kilicho dhaifu katika dunia ili kuwaaibisha wenye nguvu” (1 Wakor 1:27). Hata hivyo, waandishi, wanaojua hasa mahali ambapo Masiha alizaliwa, walioesha njia kwa wengine lakini wao wenyewe hawakusogea. Kiukweli, haitoshi kujua maandiko ya kinabii ili tuwe katika masafa ya kimungu, bali ni lazima tujiachie tuzame ndani na kuruhusu Neno la Mungu kufufua shauku ya utafiti, ili kuwasha hamu ya kumwona Mungu.

Katika hatua hii Herode, kwa siri, kama wadanganyifu na watu wenye jeuri wafanyavyo, anawauliza Mamajusi wakati hususan,  wa kutokea kwa nyota hiyo na kuwahimiza waendelee na safari yao kisha warudi kumpa habari, ili kwamba yeye pia aweze kwenda na kumwabudu mtoto mchanga. Kwa wale walioshikamana na mamlaka, Yesu si tumaini la kukaribishwa, bali ni tishio la kuondolewa! Mamajusi wanapoondoka, nyota hiyo inatokea tena na kuwaongoza kwa Yesu, ishara kwamba uumbaji na neno la kiunabii huwakilisha neno  ambalo Mungu huzungumza nalo na kujiruhusu kupatikana. Kuonekana kwa nyota hiyo kunaamsha ndani ya watu hao furaha isiyo na kifani, kwa sababu Roho Mtakatifu, ambaye husukuma moyo wa yeyote anayemtafuta Mungu kwa uaminifu, pia humjaza furaha. Baada ya kuingia ndani ya nyumba, Mamajusi walimsujudia Yesu na kumpa zawadi za thamani, zinazostahili mfalme, zinazostahili Mungu. Kwa nini? Je, wanaona nini?

Mwandishi wa kale anaandika: wanaona “mwili mdogo mnyenyekevu ambao Neno ameuchukua; lakini utukufu wa umungu haufichiki kwao. Wanamwona mtoto mchanga; bali wanamwabudu Mungu”(rej. Chromatius wa Aquileia, Ufafanuzi wa Injili ya Mathayo 5,1). Kwa hiyo Mamajusi wanakuwa waamini wa kwanza kati ya wapagani wote, Picha ya Kanisa lililokusanywa kutoka katika kila lugha na taifa. Ndugu wapendwa, na tujiweke pia katika shule ya Mamajusi, ya hawa “mahujaji wa matumaini” ambao, kwa ujasiri mkubwa, walielekeza hatua zao, mioyo yao na mali zao kumwelekea Yeye aliye tumaini si la Israeli tu bali la mataifa yote. Tujifunze kumwabudu Mungu katika udogo wake, katika ufalme wake usiopondeka bali hutufanya kuwa huru na wenye uwezo wa kutumikia kwa heshima. Na tumpe zawadi nzuri zaidi, ili kuonesha imani yetu na upendo wetu.

Katekesi ya Papa
19 Februari 2025, 15:08