Papa Francisko:Huduma ya silaha iheshimu utakatifu wa maisha na uumbaji!
Na Angella Rwezaula – Vatican.
Mara baada ya Misa Takatifu, Dominika tarehe 9 Februari 2025, kabla ya Sala ya Malaika wa Bwana, Baba Mtakatifu alisema kuwa “Kabla ya kuhitimisha maadhimisho haya, ninapenda kuwasalimu nyote mliofanikisha hija hii ya Jubilei ya Jeshi, Polisi na Usalama. Ninawashukuru mamlaka mashuhuri za kiraia kwa uwepo wao na, kwa utumishi wao wa kichungaji, Maafisa wa kijeshi na Mapadre.
Ninatoa salamu zangu kwa wanajeshi wote wa ulimwengu, na ningependa kukumbuka mafundisho ya Kanisa katika suala hili. Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican unasema: “Wale ambao katika huduma ya nchi yao wanatekeleza taaluma yao katika safu za jeshi, wanapaswa pia kujiona kuwa watumishi wa usalama na uhuru wa watu wao” (Gaudium et spes, 79).”
Kwa kuongezea “Huduma hii ya silaha lazima itekelezwe katika ulinzi halali tu, na kamwe isiweke mamlaka juu ya mataifa mengine, kila mara ikizingatiwa mikataba ya kimataifa kuhusu migogoro na, zaidi ya yote, kwa heshima takatifu ya maisha na uumbaji.”
Papa kwa njia hiyo aliongeza kusema kuwa “ na tusali kwa ajili ya amani, katika Ukraine inayoteswa, katika Palestina, katika Israeli na katika Mashariki ya Kati, katika Myanmar, Kivu na katika Sudan. Silaha zinyamaze kila mahali na kilio cha wananchi kisikike, wakiomba amani! Tunakabidhi maombi yetu kwa maombezi ya Bikira Maria, Malkia wa Amani.”
Aliendelea Papa Francisko na sala ya Malaika wa Bwana: “Angelus Domini…”