杏MAP导航

Tafuta

Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Wasanii na Wanamichezo, Kardinali José Tolentino Cala?a de Mendon?a, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Dominika 16 Februari 2025 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Wasanii na Wanamichezo, Kardinali José Tolentino Cala?a de Mendon?a, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Dominika 16 Februari 2025 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Jubilei ya Wasanii na Wanamichezo 15-16 Februari 2025: Mashuhuda wa Kinabii

Hawa ni mafundi wa furaha na kile kilicho chema; ni mashuhuda na wajenzi wa imani, matumaini na mapendo. Wasanii ni walimu na kioo cha jamii, licha ya mapungufu yao ya kibinadamu. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Wasanii na Wanamichezo, Kardinali José Tolentino Cala?a de Mendon?a, kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 16 Februari 2025 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama kielelezo cha kufunga maadhimisho ya Jubilei.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika Kanisa Katoliki maadhimisho ya Jubilei ni mwaka wa toba na maondoleo ya dhambi; upatanisho, na wongofu wa ndani unaojikita katika Sakramenti ya Kitubio. Maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo yananogeshwa na kauli mbiu: Mahujaji wa matumaini. Huu ni muda muafaka wa kusoma na kutafakari Neno la Mungu; Kusali na kumwilisha sala hii katika matendo ya huruma kiroho na kimwili, ili kuwaonjesha matumaini wale waliopondeka na kuvunjika moyo! Maadhimisho ya Jubilei kwa wasanii na wanamichezo yamezinduliwa rasmi tarehe 15 Februari na kuhitimishwa kwa Ibada ya Misa Takatifu, Dominika tarehe 16 Februari 2025. Maadhimisho haya ya matumaini ni kipindi cha ushuhuda wa imani, sala, tafakari pamoja na kuonja huruma ya Mungu katika maisha yao kama wasanii na wanamichezo; tayari kujisadaka kwa ajili ya kumwilisha matendo ya huruma: kiroho na kimwili, kielelezo cha imani tendaji, uso wa huruma na upendo wa Mungu.

Kardinali Josè Ameongoza Misa Takatiu kwa niaba ya Papa Francisko
Kardinali Josè Ameongoza Misa Takatiu kwa niaba ya Papa Francisko   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Wasanii na wanamichezo mbalimbali ni chemchemi ya faraja, amani, upendo, mshikamano, urafiki na matumaini kwa watu waliopondeka na kuvunjika moyo. Ni chachu ya majadiliano ya kidini na kiekumene, ingawa pia wanakabiliwa na changamoto kubwa pamoja na ugumu wa maisha. Hawa ni mafundi wa furaha na kile kilicho chema; ni mashuhuda na wajenzi wa imani, matumaini na mapendo. Wasanii ni walimu na kioo cha jamii, licha ya mapungufu yao ya kibinadamu. Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Wasanii na Wanamichezo, Kardinali José Tolentino Calaça de Mendonça, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 16 Februari 2025 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama kielelezo cha kufunga maadhimisho ya Jubilei kwa Wasanii na Wanamichezo yaliyowawezesha wasanii na wanamichezo hawa kupita kwenye Lango la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Zaidi ya washiriki elfu saba kutoka katika nchi sitini, wamehudhuria Jubilei hii, tukio muhimu la maisha ya kiroho na kitamaduni.

Wasanii na wanamichezo ni vyombo na mashuhuda wa Heri za Mlimani
Wasanii na wanamichezo ni vyombo na mashuhuda wa Heri za Mlimani   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Masomo ya dominika ya sita ya kipindi cha Mwaka C wa Kanisa yanayaweka maisha ya mwanadamu kati ya njia mbili: kati ya njia ya kibinadamu na njia ya kimungu, kati ya njia ya wenye haki na njia ya wasio haki; njia ya kidunia na njia ya kiroho. Katika mahibiri yake, Baba Mtakatifu Francisko amekazia kuhusu, Heri za Mlimani, dira na mwongozo wa maisha matakatifu na adili; chemchemi ya furaha ya kweli na amani; kielelezo cha umoja, upendo na mshikamano; sehemu ya mchakato wa kutafuta furaha ya kweli inayopata chimbuko lake kutoka kwa Mwenyezi Mungu, kielelezo ch upendo, umoja na ushuhuda kati ya binadamu na Muumba wake na kati ya binadamu na jirani zake. Rej. Lk 6: 17, 2026. Wasanii na wanamichezo wanao simika maisha yao katika utamaduni wanaalikwa kuwa ni mashuhuda wa dira ya kimapinduzi ya Heri za Mlimani, kwa kuunda uzuri, kufichua ukweli, wema na uzuri uliofichika katika sakafu ya historia ya mwanadamu, kwa kuendelea kuwa ni sauti ya watu wasiokuwa na sauti na hivyo kubadilisha maumivu kuwa ni matumaini. Walimwengu wanashuhudia athari za myumbo wa uchumi na kijamii, mgogoro wa nafsi na maana ya maisha. Jambo la msingi ni waamini kujiuliza ikiwa kweli wao ni mahujaji wa matumaini, au wazururaji; wanalo lengo la maisha, au wamekuwa ni wababaishaji na watu wa kutangatanga.

Jubilei ya Wasanii na Wanamichezo 15-16 Februari 2025
Jubilei ya Wasanii na Wanamichezo 15-16 Februari 2025   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Lengo kuu la msanii ni kumsaidia binadamu asipoteze, mwelekeo na upeo wa matumaini yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya mwanadamu; huu ni moto unaowaka na kuangaza kama Neno la Mungu, kwani sanaa ya kweli daima ni kukutana na fumbo; na hivyo kuwa na uzuri unaopita; kwa uchungu unaotuliza na ukweli wenye wito. Vingenevyo anasema Baba Mtakatifu Francisko wasanii na wanamichezo watakumbana na “Ole.” Dhamiri kuu ya msanii ni kugundua na kufichua ukuu uliofichika, ili kuufanya uonekane kwa macho na mioyo. Msanii anapaswa kuwasaidia wengine kupambanua kati ya mwangwi tofauti wa matukio ya ulimwengu, ili watu waweze kuuthamini mwangwi huu, tayari kuzaa matunda yanayokusudiwa. Rej Zab 1: 3-4.Wasanii na wanamichezo ni walinzi wa uzuri unaojua kukunja madonda ya dunia, kwa kusikiliza na kujibu kilio cha maskini, watu wanaoteseka, waliojeruhiwa, wafungwa, wanaoteseka pamoja na wakimbizi na wahamiaji. Wasanii kwa hakika ni walinzi wa “Heri” za Mlimani na kwamba, hii ni fursa kwa walimwengu kutajirishana kwa kujenga na kudumisha: Madaraja yanayowakutanisha watu katika majadiliano. Ikumbukwe kwamba, sanaa sio anasa, bali ni hitaji la roho lenye kuchukua hatua kwa hatua ukumbusho pamoja na kilio cha binadamu na hivyo kuelimisha kwa matumaini mambo yanayokita uzoefu wake katika maisha ya kawaida, kwa kuzingatia ugumu pamoja na changamoto zake katika ulimwengu mamboleo. Kristo Yesu katika Injili ya Heri na Ole anatangaza: Heri kwa maskini, wenye dhiki, wapole na wale wanaoteswa.

Wasanii na wanamichezo wanatumwa kutangaza Injili ya Heri
Wasanii na wanamichezo wanatumwa kutangaza Injili ya Heri   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Haya ni mapinduzi ya kimtazamo changamoto kwa sanaa kushiriki katika mapinduzi haya. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, ulimwengu unawahitaji wasanii wa kinabii, wasomi wenye ujasiri, wajenzi wa tamaduni mbalimbali. Kumbe, wasanii na wanamichezo wanaitwa kuongozwa na Injili ya Heri, ili kutangaza na kushuhudia ulimwengu mpya. Huu ni mwaliko kwa wasanii na wanamichezo kuwa ni wadadisi wanaohoji na kutafuta, kiasi hata cha kuhatarisha maisha yao. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, sanaa ya kweli inatoa amani ya kutulia. Matumaini kamwe si udanganyifu; uzuri unaoelea katika ombwe. Wasanii na wanamichezo wanakumbushwa kwamba, zawadi ya maisha yao si kwa bahati mbaya, bali ni wito. Hili ni jibu kwa ukarimu, kwa shauku na kwa upendo mkuu.

Jubilei ya Wasanii na Wanamichezo
16 Februari 2025, 15:27