杏MAP导航

Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuchukua fursa hii kuwapongeza kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi hiki, hususan kwa kuwekeza zaidi katika majiundo kwa vijana wa kizazi kipya. Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuchukua fursa hii kuwapongeza kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi hiki, hususan kwa kuwekeza zaidi katika majiundo kwa vijana wa kizazi kipya.  (Vatican Media)

Chuo Kikuu cha Kikatoliki Ni Mahali Pa Majiundo, Tafiti Na Shuhuda Za Maisha!

Papa anapenda kuitia shime familia yote ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Taalimungu cha Triveneto kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, daima kwa kuendelea kuwa waaminifu kwa Mapokeo ya kweli ya Mama Kanisa, huku wakijitahhidi kusoma alama za nyakati. Huu ni mwaliko wa kupokea changamoto kwa moyo wa ujasiri, ili kuzifanyia kazi mintarafu kweli za Kiinjili kwa ajili ya kijana wa kizazi kipya.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Ilikuwa ni mwaka 1991, Baraza la Maaskofu Triveneta, Kaskazini mwa Italia lilipobuni mradi wa kuanzisha Kitivo cha Taalimungu Cha Triveneto, mintarafu mageuzi makubwa ya ufundishaji wa Taalimungu nchini Italia na hivyo kuunganisha taasisi mbalimbali za elimu dini, ili kuleta maboresho na ufanisi mkubwa mintarafu: tafiti za kitaalimungu, kwa kukuza na kudumisha majadiliano ya kitamaduni, huduma kwa watu wa Mungu mintarafu mahitaji ya kidini na kijamii kwa mikoa ya: Veneto, Trentino Alto Adige pamoja na Friuli Venezia Giulia. Tarehe 20 Juni 2005 kikafunguliwa rasmi na kuwa na makao yake makuu mjini Padova. Kitivo hiki kwa sasa kina hadhi ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Taalimungu, kinachopania pamoja na mambo mengine kukiandaa kizazi kipya ili kuweza kukabiliana na changamoto za kidini na kimaadili pamoja na kuendelea kujikita katika sayansi ya dini. Chuo hiki kina wanafunzi 1600 wanaohudumiwa na Majaalimu 300. Hawa ni wanafunzi kutoka Romania, Ghana, India, Ufaransa, Togo, Brazili, Pwani ya Pembe, Ukraine, Ecuador, Sri Lanka, Chile, Australia pamoja na Visiwa vya Solomoni. Hizi ni kati ya nchi zenye wanafunzi wengi chuoni hapo! Kumbe, hiki ni Chuo Kikuu kinachotoa Masomo ya Kitaalimungu pamoja na Sayansi ya Dini. Ni Chuo Kikuu kinachowaandaa waalimu wa kufundisha Elimu Katoliki katika shule mbalimbali nchini Italia mintarafu sera na mikakati ya shughuli za kichungaji; Majadiliano ya kidini na kiekumene; Uchapaji, Uandishi wa Habari, Maadili, Sanaa na Utalii.

Kumbukizi ya Miaka 20 ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Triveneto
Kumbukizi ya Miaka 20 ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Triveneto

Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Taalimungu cha Triveneto kwa mwaka 2025 kinaadhimisha kumbukizi ya Miaka 20 tangu kuanzishwa kwake. Kati ya wawezeshaji kwenye kumbukizi hii ni pamoja na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Kardinali Gianfranco Ravasi, Rais Mstaafu wa Baraza la Kipapa la Utamaduni, Prof. Stefano Zamagni, Jaalimu pamoja na wanataalimungu maarufu kama vile Christoph Theobaldi pamoja na Jean Luc Marion. Ni katika muktadha wa kumbukizi ya Miaka Ishirini, tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Taalimungu cha Triveneto, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuchukua fursa hii kuwapongeza kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi hiki, hususan kwa kuwekeza zaidi katika majiundo kwa vijana wa kizazi kipya. Baba Mtakatifu anapenda kuitia shime familia yote ya Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Taalimungu cha Triveneto kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, sehemu mbalimbali za dunia, daima kwa kuendelea kuwa waaminifu kwa Mapokeo ya kweli ya Mama Kanisa, huku wakijitahhidi kusoma alama za nyakati. Huu ni mwaliko wa kupokea changamoto kwa moyo wa ujasiri, ili kuzifanyia kazi mintarafu kweli za Kiinjili kwa ajili ya kijana wa kizazi kipya. Ili kuweza kulifikia lengo hili, Chuo hiki Kikuu kinapaswa kuwa ni mahali pa majiundo ya kitaalimungu sanjari na upembuzi yakinifu wa kitaalimungu unaosimikwa katika ushuhuda wa maisha ya Kikristo kutoka kwa kila mmoja wao.

Kumbukizi ya Miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Triveneto
Kumbukizi ya Miaka 20 tangu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha Triveneto   (ANSA)

Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba majaalimu wataweza kuwasaidia vijana wa kizazi kipya kuweza kukita maisha yao katika haki msingi, mafao ya wengi na uzuri unaopata chimbuko lake kutoka kwa Mungu mwenyewe. Mwishoni Baba Mtakatifu Francisko kwa mara nyingine tena anawashukuru kwa utume huu wa elimu wanaoutekeleza na kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Kikao cha hekima na mwishowe akawatumia baraka zake za kitume.Kwa upande wake Askofu mkuu Francesco Moraglia, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Taalimungu cha Triveneto ambaye pia ni Patriaki wa Jimbo kuu la Venezia katika utangulizi wake katika Siku hii maalum ya “Dies academicus” yaani mwanzo wa Mwaka wa Masomo amekazia umuhimu kwa Jumuiya ya Chuo kikuu kujikita katika ujenzi wa “Sensus ecclesiae” yaani “Maana ya Kanisa” kwa watu wa Mungu kufikiri kwa mapana zaidi, kwa kuhakikisha kwamba, elimu ya dini Katoliki inakuwa ni chemchemi ya matumaini; kwa kuendeleza majadiliano ya kidini na kiekumene; kwa kuthaini tunu msingi za dini mbalimbali; utu, heshima na haki msingi za binadamu; kwa kukuza na kujenga mahusiano na mafungamano kati ya Mungu na mwanadamu na kati yao wenyewe pamoja na kuendelea kupyaisha maisha.

Chuo Kikuu cha Triveneto: Mahali pa majiundo, tafiti na ushuhuda
Chuo Kikuu cha Triveneto: Mahali pa majiundo, tafiti na ushuhuda   (ANSA)

Ni wakati wa kuangalia kwa makini matumizi bora zaidi ya teknolojia ya akili mnemba kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni wakati wa kuragibisha upendo, urafiki wa kijamii, maridhiano na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, kwa kulinda, kutangaza na kushuhudia ukweli. Huu ni mwaliko wa kuachana na tabia ya chuki na uhasama; kwa kukuza uhuru wa kidini na uhuru wa kuabudu. Utu, heshima na haki msingi za binadamu ni mambo msingi ili kukuza na kudumisha Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; kwa kutoa kipaumbele cha pekee kwa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; wajibu na dhamana ya wazazi na walezi katika jamii. Askofu mkuu Francesco Moraglia, amehitimisha hotuba yake kwa kuwatakia wote waangazwe na mwanga wa kitaalimungu, ili Kristo Yesu na Injili yake aweze kuonekana na hivyo watu wa Mungu kuweza kufurahia mambo ya kimungu, furaha inayobubujika kutoka katika maisha ya neema!

Chuo Kikuu cha Kikatoliki
18 Februari 2025, 14:26