Barua ya Baba Mtakatifu Francisko Kwa Maaskofu Katoliki Marekani: Changamoto Ya Wahamiaji
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Baba Mtakatifu Francisko anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi, usalama na matumaini ya maisha. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu kwamba, sera na mikakati hii itaendelea kumwilishwa pia kwenye Makanisa mahalia, ili kuwasaidia watu hawa ambao mara nyingi wanajikuta wakitumbukia katika biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; mifumo mbalimbali ya utumwa mamboleo na nyanyaso mambo ambayo kimsingi yanasigina: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna sababu nyingi zinazowalazimisha watu kuzikimbia au kuzihama nchi zao: Vita, Majanga asilia, Umaskini nk. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Misericordia et misera” yaani “Huruma na amani” anasema, huruma ni kielelezo makini cha upendo wa Mungu unaosamehe, unaoongoa, unaopyaisha na kubadili mwelekeo wa maisha. Ni kielelezo cha ufunuo wa Fumbo la Mungu ambalo ni huruma ya milele, inayowakumbatia na kuwaambata wote pasi na ubaguzi, kiasi cha kuwakirimia maisha mapya, chemchemi ya furaha na matumaini mapya, yanayovunjilia mbali kuta za ubaguzi, ubinafsi na uchoyo ili kutenda wema, kufikiri vyema na kuondoa huzuni moyoni. Huu ni mwaliko kwa waamini kufanya mang’amuzi ya huruma inayowakirimia furaha, hata kama maisha yao bado yanasheheni matatizo na changamoto mbalimbali, ili kuondokana na utamaduni wa huzuni, utupu na upweke unaopelekea msongo wa mawazo kwa watu wengi!
Baba Mtakatifu anasema Wakristo wa Kanisa la Mwanzo walitambulikana kama “wanafunzi wa njia” Rej. Mdo 9:2. Mwamini ni msafiri ambaye anatambua kwamba, kamwe hajafikia lengo na hatima ya safari yake hapa duniani. Kumbe, anapaswa kujifunza kila siku, akijitahidi kumfuasa Kristo Yesu ambaye ni: njia, kweli, na uzima unawaowapeleka kwa Baba wa milele. Rej. Yn 14:6. Baba Mtakatifu anatoa mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kufungua malango yake kwa wakimbizi na wahamiaji, kama ilivyokuwa kwa Msamariamwema aliyethubutu kuokoa maisha ya mtu yule aliyeangukia kati ya wanyang’anyi. Hata leo hii kuna watu wanaohatarisha maisha yao huko jangwani, misituni na kwenye mito, maziwa na bahari. Ni watu wanaoteswa na kunyanyaswa utu, heshima na haki zao msingi, kiasi hata cha kutumbukizwa katika utumwa mamboleo. Mara nyingi hawa ni watu wanaokimbia: majanga asilia, vita pamoja na vitendo vya kigaidi kama inavyojitokeza kwa sasa sehemu mbalimbali za dunia. Kuna watu ambao hawawajali hata kidogo, hiki ni kielelezo cha ubinafsi, uchoyo na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuonesha moyo wa huruma na mapendo kwa sababu huu ndio utambulisho wa Mwenyezi Mungu katika mioyo ya wanadamu. Itakumbukwa kwamba, mtindo wa Mungu unasimikwa katika maneno makuu matatu: Ukaribu, Huruma na Upole na kwamba, hiki ni kielelezo makini cha ushuhuda wa Ukristo uliopelekea yule Msamaria mwema kutangaza na kushuhudia wema na upendo wa Mungu na udugu wa kibinadamu. Huu ni mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kuwa kama Msamaria Mwema kwa kuwasaidia wakimbizi na wahamiaji katika mateso yao.
Ni katika muktadha wa mateso na mahangaiko kwa ajili ya wakimbizi na wahamiaji, Baba Mtakatifu Francisko amewaandikia Maaskofu wa Marekani, Barua, kuonesha mshikamano wake wa dhati na Maaskofu katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji wanaokabiliana na changamoto kubwa kwa wakati huu. Papa Pio wa XII ameelezea kwa ubora zaidi Mafundisho Jamii ya Kanisa kuhusu wakimbizi na wahamiaji, changamoto na mwaliko kwa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za wakimbizi na wahamiaji. Inasikitisha kuona Marekani inatekeleza mkakati wa kuwarejesha makwao kwa nguvu wahamiaji na wakimbizi, changamoto ni kuhakikisha kwamba, utawala wa sheria unazingatiwa, kwa kujikita katika upendo unaojenga na kudumisha udugu wa kibinadamu kwa wote. Huu ni mwaliko kwa watu wa Mungu nchini Marekani kufanya kazi kwa karibu zaidi na wakimbizi pamoja na wahamiaji, kwa kuragibisha haki msingi za binadamu na kuendelea kujenga mshikamano na udugu wa kibinadamu. Maandiko Matakatifu yanasimulia wimbi kubwa la Waisraeli waliolazimika kupelekwa uhamishoni, wakaimarisha imani yao kwa Mwenyezi Mungu anayekuza na kutukuza utu wa kila mtu. Hata Familia Takatifu ya Yesu, Maria na Yosefu ililazimika kwenda uhamishoni nchini Misri, kielelezo cha faraja kwa wahamiaji na mahujaji wa nyakati zote, wanaokimbia nyanyaso na madhulumu; na hivyo kuacha nyuma makazi, familia, ndugu na jamaa na kwenda kuishi ugenini. Hivi ndivyo ilivyokuwa hata kwa Kristo Yesu, anayeendelea kuwafundisha waja wake kutambua utu, heshima na haki msingi za binadamu na kwamba, sera na mikakati ya wakimbizi na wahamiaji haina budi kuzingatia utu, heshima na haki msingi za binadamu.
Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, amekuwa akifuatilia kwa umakini mkubwa sera na mikakati ya kuwarejesha kwa nguvu wakimbizi na wahamiaji wengine wakishutumiwa kwa uhalifu. Ni kweli kwamba, kila taifa linapaswa kujilinda na kuhakikisha usalama wa raia na mali zao. Lakini inasikitisha kuona kwamba, watu waliokimbia umaskini wa kutisha, ukosefu wa uhakika wa usalama; watu walionyonywa, walioteswa na kudhulumiwa; watu walioathirika kutokana na mabadiliko ya tabianchi; watu ambao kwa hakika utu, heshima na haki zao msingi zimesiginwa, wanarejeshwa makwao kwa nguvu. Kimsingi utawala wa sheria unapimwa kwa sheria kuwalinda na kuwatetea maskini na wanyonge katika jamii. Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yanaendelezwa pale ambapo Serikali inaheshimu sheria kwa raia wote. Baba Mtakatifu anasema, sera na mbinu mkakati wa Kanisa Katoliki katika huduma kwa wakimbizi na wahamiaji inajikita katika mambo makuu manne yaani: “Kuwapokea, kuwalinda, kuwaendeleza na kuwahusisha wakimbizi na wahamiaji” katika maisha ya jamii inayowapokea na kuwapatia hifadhi, usalama na matumaini ya maisha.
Sera hii si kikwazo kwa maendeleo ya sheria, taratibu na kanuni bora za uhamiaji kwa kuzingatia ukweli, utu, heshima na haki msingi za binadamu, vinginevyo zoezi kama hili ambalo limeanza vibaya litamalizika vibaya pia. Kama Wakristo, wanaongozwa na upendo, unaosimikwa katika utu, heshima na haki msingi za binadamu; mambo msingi yanayojenga mahusiano na mafungamano ya kijamii. Hii ndiyo sheria ya upendo “Ordo amoris” kama ilivyomwilishwa kwenye mfano wa “Msamaria Mwema.” Rej. Lk 10: 25-37. Huu ni upendo unaojenga na kudumisha udugu wa kibinadamu ambao uko wazi kwa watu wote. Baba Mtakatifu Francisko anatambua changamoto ya Maaskofu Katoliki Marekani kwa kufanya kazi kwa karibu sana na wakimbizi na wahamiaji, kama sehemu msingi ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu sanjari na kuendeleza haki msingi za binadamu. Kwa hakika Mwenyezi Mungu, kwa wakati wake, atawatuza kwa yote wanayotenda kwa ajili ya kuwalinda wakimbizi na wahamiaji. Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu kujizuia kuzama katika ubaguzi na badala yake wazame katika upendo unaokita mizizi yake katika mshikamano na ujenzi wa udugu wa kibinadamu, huku wakiendelea kujenga madaraja yanayowaunganisha watu na hivyo kuendelea kujifunza kujisadaka kwa ajili ya jirani zao kama Kristo Yesu alivyojisadaka kwa ajili ya wokovu wa wengi. Mwishoni mwa Barua yake kwa Maaskofu Katoliki Marekani, Baba Mtakatifu Francisko anawaweka wakimbizi na wahamiaji chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria wa Guadalupe; ili awawezeshe kujikita katika upatanisho, wale wanaoonekana kuwa ni maadui; awasaidie wote ili waweze kukutana tena kama ndugu wamoja, ili kwa pamoja waweze tena kukumbatiana tayari kushiriki katika ujenzi wa jamii ambayo inasimikwa katika nguzo ya udugu wa kibinadamu, jamii shirikishi na inayoheshimu utu wa wote.