Askofu Ni Mwalimu, Kuhani na Mchungaji Mwema!
Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.
Uaskofu ni utimilifu wa Daraja Takatifu ya Upadre, ambamo Askofu aliyewekwa wakfu anapewa dhamana ya: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Askofu ni kielelezo cha ukuhani mkuu, kilele cha huduma takatifu. Maaskofu kwa namna iliyo ya juu kabisa, hushika nafasi ya Kristo Yesu mwenyewe, aliye mwalimu, mchungaji na kuhani na kwamba, Maaskofu wanatenda kazi yao katika nafsi yake. Kwa njia ya Roho Mtakatifu, Maaskofu wanafanywa walimu kweli na halisi wa imani, makuhani na wachungaji. Maaskofu wamewekwa wakfu ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, kama ilivyokuwa kwa Mitume wa Kristo Yesu sanjari na kuendeleza kazi ya ukombozi iliyoanzishwa na Kristo, Kuhani mkuu na wa milele. Kristo kwa njia ya Maaskofu, anaendelea kutangaza Habari Njema na kuwatakatifuza waja wake kwa njia ya Sakramenti za imani, kiasi hata cha kuliwezesha Kanisa kupata watoto wapya wanaozaliwa kwa Maji na Roho Mtakatifu. Kristo Yesu anaendelea kuliongoza Kanisa lake kwa busara na hekima, kazi inayopaswa kutekelezwa na Maaskofu wanapowaongoza watu wa Mungu katika hija ya maisha yao hapa duniani, ili hatimaye, waweze kufikia furaha ya maisha ya uzima wa milele. Maaskofu wanatakiwa kuonesha nidhamu na heshima kubwa kwa Daraja waliyoipokea kama wagawaji wa Mafumbo ya Mungu, mashuhuda wa Injili ya Kristo na Mitume wa Roho Mtakatifu anayetakatifuza, mwaliko kwa waamini kuwasikiliza Maaskofu wao kwa dhati kabisa kama ushuhuda wa kumsikiliza Kristo mwenyewe!
Maaskofu wanakumbushwa kwamba, wameteuliwa kutoka miongoni mwa watu wa Mungu na hivyo kuwekwa wakfu kwa ajili ya mambo ya Mungu. Hili si Daraja kwa ajili ya kujitafutia mali na malimwengu yake, wala si jukwaa la kisiasa, bali Uaskofu ni kwa ajili ya huduma na kwamba, wanapaswa kukikimbia kishawishi cha kutaka kuwa Wafalme na watawala. Maaskofu watangaze Neno la Mungu; wawaonye watu na kufundisha kwa ari na moyo mkuu tunu msingi za Kiinjili. Kwa njia ya sala na sadaka yao, wawatakatifuze watu wa Mungu ili hatimaye, waweze kupata utimilifu wa utakatifu katika Kristo Yesu. Dhamana ya kwanza ya Askofu ni kusali, kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kumbe, ni wajibu wa Maaskofu kuhakikisha kwamba, wanasali daima kama sehemu ya utekelezaji wa wito wao. Wamekabidhiwa na Mama Kanisa dhamana ya kuwa ni walinzi na waadhimishaji wa Mafumbo ya Kanisa; wakuu wa familia ya Mungu, changamoto na mwaliko wa kumfuasa Kristo Yesu, Mchungaji mwema anayewafahamu Kondoo wake kwa majina na wao wanamtambua kiasi kwamba, akawa tayari kuyamimina maisha yake kwa ajili yao! Maaskofu wanapaswa kuwapenda na kuwathamini watu wao kwa dhati, lakini zaidi waoneshe umoja na mshikamano na wakleri, wadau wakuu katika utume wao kama Maaskofu. Wakleri wawe na fursa ya kuweza kukutana na kuzungumza na Maaskofu wao bila mizengwe mizengwe. Maaskofu wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii; watu wanaohitaji kuonjeshwa huruma pamoja na kupewa msaada wanaohitaji. Maaskofu wajitahidi kushirikiana na kushikamana na waamini walei katika maisha na utume wao; kwa kuwasikiliza na kuwathamini. Waoneshe ari na moyo wa majadiliano ya kiekumene na kidini; kwa kujali na kuguswa na mahangaiko ya Makanisa mengine yanayohitaji pia msaada wa hali na mali.
Baba Mtakatifu Francisko daima anawataka Maaskofu kukesha na kusali katika upendo kama mashuhuda wa Fumbo la Utatu Mtakatifu, ambao wamewekwa wakfu ili kuwa waalimu, makuhani na wachungaji. Roho Mtakatifu awasaidie Maaskofu kudhibiti udhaifu wao wa kibinadamu kwa kuambata huruma na neema ya Mungu! Ni katika muktadha huu, Kardinali José Tolentino Calaça de Mendonça, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu, tarehe 14 Februari 2025 katika Ibada ya Misa Takatifu alimweka wakfu Monsinyo Carlo Maria Polvani, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu kuwa Askofu mkuu, katika Ibada ya Misa Takatifu iliyoadhimishwa kwenye Kanisa la “San Damaso Papa” Jimbo kuu la Roma. Katika mahubiri yake, Kardinali José Tolentino Calaça de Mendonça, amemtaka Askofu mkuu Polvani kutambua udogo na unyonge wake mbele ya Mwenyezi Mungu, lakini atambue kwamba, “Kwa hiyo nakubali kwa radhi udhaifu, dharau, taabu, udhalimu na mateso, kwa ajili ya Kristo; maana ninapokuwa dhaifu, ndipo ninapokuwa na nguvu.” 2Kor 12:10. Hii ni changamoto ya kuendelea kujibidiisha katika maboresho ya maisha ya kiroho na kitume.
Kwa upande wake Askofu mkuu Carlo Maria Polvani, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu amegusia changamoto mamboleo katika maisha na utume wa Kipadre na kwamba, ili kuweza kukabiliana na changamoto hizi zote, Mapadre hawana budi kujikita katika: Sala, Neno, Sakramenti na Matendo ya huruma, ili kujipatia neema na baraka zitakazowawezesha kupambana na changamoto hizi. Amewaalika watu wa Mungu katika ujumla wake, kuwasindikiza Mapadre kwa sala na sadaka zao, huku wakiwasaidia kuweza kuishi vyema wito na utume wao. Itakumbukwa kwamba, Askofu mkuu Carlo Maria Polvani, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu alizaliwa tarehe 28 Julai 1968, huko Milano. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 14 Februari 1998, Sikukuu ya Mtakatifu Valentino, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Tarehe 26 Julai 2019, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Afisa wa Baraza la Kipapa la Utamaduni. Tarehe 12 Januari 2025, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa ni Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu na hivyo kumpandisha hadhi na kuwa ni Askofu mkuu. Tarehe 14 Februari 2025 akawekwa wakfu kuwa ni Askofu mkuu.