杏MAP导航

Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru watu wote wa Mungu wanaoendelea kusali, kumwombea na kumwandikia ujumbe wa matumaini wakati huu anapoendelea na matibabu kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli. Baba Mtakatifu Francisko anawashukuru watu wote wa Mungu wanaoendelea kusali, kumwombea na kumwandikia ujumbe wa matumaini wakati huu anapoendelea na matibabu kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli.  (ANSA)

Afya ya Baba Mtakatifu Francisko Na Jubilei ya Mashemasi 21-22 Februari 2025

Baba Mtakatifu kwa sasa anasumbuliwa na ugonjwa wa mkamba uliopelekea kulazwa tangu Ijumaa tarehe 14 Februari 2025. Ameendelea kupokea Ekaristi Takatifu, kujisomea magazeti na nyaraka mbalimbali. Baba Mtakatifu anawashukuru watu wote wa Mungu wanaoendelea kumwombea na kumwandikia ujumbe wa matumaini wakati huu anapoendelea na matibabu kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli. Anawakumbuka na kuwaombea wote kwa wema!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Taarifa kutoka Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli, iliyoko Mjini Roma Nchini Italia inaonesha kwamba, afya ya Baba Mtakatifu Francisko inaendelea kuimarika zaidi na anapata mapumziko ya kutosha, lakini madaktari wanamtaka apumzike zaidi. Baba Mtakatifu kwa sasa anasumbuliwa na ugonjwa wa mkamba (Bronchitis) uliopelekea kulazwa tangu Ijumaa tarehe 14 Februari 2025 na kwamba, hadi sasa anaendelea na matibabu. Ameendelea kupokea Ekaristi Takatifu, kujisomea magazeti na nyaraka mbalimbali. Baba Mtakatifu anawashukuru watu wote wa Mungu wanaoendelea kusali, kumwombea na kumwandikia ujumbe wa matumaini wakati huu anapoendelea na matibabu kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli. Anawakumbuka na kuwaombea wote kwa wema na ukarimu wao! Kutokana na Baba Mtakatifu Francisko kulazwa hospitalini, kumbe, Katekesi yake Siku ya Jumatano kuhusu Jubilei ya Mwaka 2025 ya Ukristo: Yesu Kristo Tumaini Letu, imefutwa. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu amemteuwa Askofu mkuu Salvatore Rino Fisichella, Mwenyekiti mwenza, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya Mashemasi, Dominika tarehe 23 Februari 2025 kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, kuanzia majira ya Saa 3: 00 kwa Saa za Ulaya, sawa na Saa 5:00 kwa Saa za Afrika Mashariki na Kati. Maadhimisho ya Jubilei ya Mashemasi ni kuanzia tarehe 21 hadi tarehe 22 Februari 2025. Itakumbukwa kwamba, kuna makundi mawili ya Mashemasi ndani ya Kanisa.

Kuna makundi mawili ya ushemasi: Ushemasi wa mpito na wakudumu
Kuna makundi mawili ya ushemasi: Ushemasi wa mpito na wakudumu

Kuna Mashemasi wa mpito kuelekea Daraja Takatifu la Upadre na kuna Mashemasi wa kudumu ambao wengi wao ni watu wa familia, lakini wanajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa kadiri ya Sheria za Kanisa, lakini zaidi huduma ya upendo inayomwilishwa katika matendo ya huruma kiroho na kimwili.Huduma ya Sakramenti ya Daraja Takatifu tangu mwanzo, imegawanyika katika sehemu kuu tatu: Uaskofu ambao ni utimilifu wa Sakramenti ya Daraja; Upadre na Ushemasi. Kumbe, Mashemasi ni wasaidizi wakuu wa Maaskofu na Mapadre. Mashemasi hushiriki kwa namna ya pekee utume na neema ya Kristo Yesu kwa kupewa chapa isiyofutika na hufananishwa na Kristo aliyejifanya “Shemasi” yaani mtumishi wa wote. Mashemasi ni wahudumu wakuu wakati wa maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa, hasa wakati wa Ibada ya Misa Takatifu. Mashemasi wanaweza kusimamia na kubariki Ndoa Takatifu. Ni wahudumu wa Neno kwa kutangaza, kuhubiri na kulishuhudia katika huduma mbali mbali za upendo. Dhana ya Mashemasi wa kudumu, ambao kimsingi wanapewa Ushemasi wa huduma kadiri ya mafundisho ya Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Barani Afrika ni wachache sana, lakini kazi ya huduma kwa kiasi kikubwa inatekelezwa na Makatekista. Baba Mtakatifu Benedikto XVI katika Waraka wake wa kitume, Dhamana ya Afrika, “Africae munus” ameweka mkazo juu ya umuhimu wa Mashemasi wa kudumu kama sehemu ya kuendeleza mchakato wa kimisionari.

Mashemasi ni wahudumu wa Neno na Sakramenti za Kanisa
Mashemasi ni wahudumu wa Neno na Sakramenti za Kanisa

Mashemasi wa kudumu wanapaswa kujivunia kazi yao njema wanayoitekeleza kwa nguvu ya kimaadili kwa kuheshimu tunu ya uaminifu, ukweli, furaha na mafao ya wengi. Mashemasi katika ujumla wao wanahimizwa kutoa huduma ya pekee kwa wagonjwa wa kiakili na kimwili; maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii na kwamba, upendo na huruma ya Kristo Yesu iwafikie na kuwaambata wote! Kwa nama ya pekee, Mashemasi wanapoadhimisha Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Maaskofu wanahimizwa kuwapatia majiundo makini ya awali na endelevu Mashemasi wao, ili wawe kweli ni mfano bora wa kuigwa kama ilivyokuwa kwa Mashemasi watakatifu Stefano, Mtakatifu Laurenti, Mtakatifu Vincenti pamoja na mashemasi wengi ambao wamekuwa ni mashuhuda wa imani, matumani na mapendo. Daima watafute kumtambua na kukutana na Kristo Yesu katika Fumbo la Ekaristi Takatifu na katika huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Huduma ya Altare na upendo kwa maskini iwe ni chachu ya utakatifu wa maisha. Mashemasi kwa hakika ni wahudumu wa Injili ya huruma, mapendo na matumaini.

Afya ya Papa Francisko
18 Februari 2025, 14:02