杏MAP导航

Tafuta

Afya ya BabaMtakatifu Francisko inaendelea kuimarika. Afya ya BabaMtakatifu Francisko inaendelea kuimarika.   (ANSA)

Afya ya Baba Mtakatifu Francisko Inaendelea Kuimarika: Anawashukuru Wote Kwa Sala

Dominika tarehe 16 Februari 2025, Baba Mtakatifu Francisko ameongoza Sala na tafakari ya Malaika wa Bwana kutoka katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli. Baba Mtakatifu anawashukuru waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaoendelea kumsindikiza kwa sala na kwa kuonesha ukaribu wao katika kipindi hiki alicholazwa hospitalini Gemelli. Baba Mtakatifu ameungana na wasanii pamoja na wanamichezo katika maadhimisho ya Jubilei yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Wasanii na wanamichezo mbalimbali ni chemchemi ya faraja, amani, upendo, mshikamano, urafiki na matumaini kwa watu waliopondeka na kuvunjika moyo. Ni chachu ya majadiliano ya kidini na kiekumene, ingawa pia wanakabiliwa na changamoto kubwa pamoja na ugumu wa maisha. Hawa ni mafundi wa furaha na kile kilicho chema; ni mashuhuda na wajenzi wa imani, matumaini na mapendo. Wasanii ni walimu na kioo cha jamii, licha ya mapungufu yao ya kibinadamu.

Papa Francisko anawashukuru wote wanaosali kwa ajili yake.
Papa Francisko anawashukuru wote wanaosali kwa ajili yake.

Ni katika muktadha wa maadhimisho ya Jubilei ya Wasanii na Wanamichezo, Kardinali José Tolentino Calaça de Mendonça, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Dominika tarehe 16 Februari 2025 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama kielelezo cha kufunga maadhimisho ya Jubilei kwa Wasanii na Wanamichezo yaliyowawezesha wasanii na wanamichezo hawa kupita kwenye Lango la Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Zaidi ya washiriki elfu saba kutoka katika nchi sitini, wamehudhuria Jubilei hii, tukio muhimu la maisha ya kiroho na kitamaduni. Taarifa kutoka Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli, Mjini Roma Nchini Italia inaonesha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko amepata mapumziko ya kutosha na kwamba, hali yake inaendelea kuimarika zaidi, lakini madaktari wanamtaka apumzike zaidi.

Jubilei ya Wasanii na Wanamichezo 15-16 Februari 2025
Jubilei ya Wasanii na Wanamichezo 15-16 Februari 2025   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Dominika tarehe 16 Februari 2025, Baba Mtakatifu Francisko ameongoza Sala na tafakari ya Malaika wa Bwana kutoka katika Hospitali ya Chuo Kikuu cha Agostino Gemelli. Baba Mtakatifu anawashukuru waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanaoendelea kumsindikiza kwa sala na kwa kuonesha ukaribu wao katika kipindi hiki alicholazwa hospitalini Gemelli. Baba Mtakatifu ameungana na wasanii pamoja na wanamichezo katika maadhimisho ya Jubilei yao. Ametumia fursa hii kulishukuru Baraza la Kipapa la Utamaduni na Elimu kwa maandalizi na hatimaye maadhimisho yake, tukio linalokumbushia umuhimu wa sanaa kama lugha inayosambaza uzuri; lugha inayowaunganisha watu wa Mataifa na hivyo kuchangia katika kukuza na kudumisha amani na utulivu, ili hatimaye, kuchamazisha kilio cha vita. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwasalimia na kuwatakia kheri na baraka na kwamba, alitamani sana kuwapo kati yao.

Jubilei ya Wasanii na Wanamichezo 15-16 Februari 2025
Jubilei ya Wasanii na Wanamichezo 15-16 Februari 2025   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko kwa sasa anasumbuliwa na ugonjwa wa mkamba (Bronchitis) uliopelekea kulazwa tangu Ijumaa tarehe 14 Februari 2025. Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwasalimia mahujaji waliofika mjini Roma hasa kutoka Jimbo Katoliki la Parma, wanaofanya hija ya matumaini. Amewaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kusali kwa ajili ya kuombea amani katika nchi zinazokabiliana na vita pamoja na kinzani hasa Ukraine, Palestina, Israeli, Ukanda wa Mashariki, Myanmar, Kivu na Sudan.

Papa: Malaika wa Bwana
16 Februari 2025, 15:02