杏MAP导航

Tafuta

Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 10 Januari 2025 amekutana na kuzungumza na Waragibishaji wa Mradi wa Ecoles de Vies” unaokita mizizi yake katika Injili na Mafundishi Jamii ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 10 Januari 2025 amekutana na kuzungumza na Waragibishaji wa Mradi wa Ecoles de Vies” unaokita mizizi yake katika Injili na Mafundishi Jamii ya Kanisa.  (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Umuhimu wa Elimu Shirikishi: Utu, Heshima na Haki Msingi za Binadamu

Papa Francisko, Ijumaa tarehe 10 Januari 2025 amekutana na kuzungumza na Waragibishaji wa Mradi wa Ecoles de Vies” unaokita mizizi yake katika Injili na Mafundishi Jamii ya Kanisa, unaotoa kipaumbele kwa walemavu, wanaopaswa kutambuliwa kuwa ni watu wenye utu, heshima na haki zao msingi na kwamba, maisha ya kila mtu yanapaswa kulindwa na kuheshimiwa, kwa sababu ni zawadi kutoka kwa Mungu; zawadi inayopaswa kupokelewa kwa upendo na heshima.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa “Global Compact on Education” ni mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji zinazotekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko, ili kujenga mfumo wa elimu unaojikita katika msingi wa elimu fungamanishi. Lengo ni kuwasaidia vijana kujizatiti zaidi katika elimu fungamanishi inayowataka vijana wa kizazi kipya kuwa wasikivu, wajenzi wa haki, amani, umoja na udugu wa kibinadamu katika usawa! Baba Mtakatifu anakazia mfumo wa elimu itakayosaidia pia kuleta Mfumo Mpya wa Uchumi Duniani unaojikita katika wongofu wa kiikolojia kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kimsingi mchakato wa mabadiliko katika mfumo wa elimu duniani unapaswa kuwahusisha watu wote ili kuunda “kijiji cha elimu”, mahali ambapo watu wote, kadiri ya dhamana zao, wanashiriki wajibu wa kuunda mtandao ambao ni wazi katika ujenzi wa mafungamano ya kibinadamu, kwani kila mtu anakuwa na wajibu wa kuchangia katika mchakato wa maboresho ya elimu.

Elimu inayokita mizizi yake katika utu, heshima na haki msingi
Elimu inayokita mizizi yake katika utu, heshima na haki msingi   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Huu ni mwaliko kwa jamii kujenga utamaduni wa usikivu kwa vijana wa kizazi kipya; wadumishe: mshikamano wa udugu wa kibinadamu, ukarimu na mafungamano ya kijamii yanayowawezesha kukutana na vijana wengine kutoka sehemu mbalimbali za dunia. Ni katika muktadha huu wa elimu, Baba Mtakatifu Francisko, Ijumaa tarehe 10 Januari 2025 amekutana na kuzungumza na Waragibishaji wa Mradi wa Ecoles de Vies” unaokita mizizi yake katika Injili na Mafundisho Jamii ya Kanisa, unaotoa kipaumbele cha pekee kwa walemavu, wanaopaswa kutambuliwa kuwa ni watu wenye utu, heshima na haki zao msingi na kwamba, maisha ya kila mtu yanapaswa kulindwa na kuheshimiwa, kwa sababu ni zawadi kubwa kutoka kwa Mungu; zawadi inayopaswa kupokelewa kwa upendo na heshima. Kristo Yesu katika maisha na utume wake, alizungukwa daima na wagonjwa, watu waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii, akawagusa, akazungumza nao; akawaganga na kuwaponya magonjwa yao. Kwa njia hii, Kristo Yesu akajenga na kudumisha mahusiano mazito na wagonjwa pamoja na wale wote waliokuwa wakisukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii.

Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa: Mageuzi makubwa ya elimu
Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa: Mageuzi makubwa ya elimu   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Ni katika mantiki hii, Kristo Yesu akaleta mang’amuzi na mwono mpya juu ya wagonjwa na walemavu. Baba Mtakatifu Francisko anasema, kwa kumwilisha tunu msingi hizi wanashiriki katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa ambalo linatoka kuwaendea wagonjwa; hili ni Kanisa ambalo ni karimu, tayari kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na watu wote, lakini zaidi kwa kuendelea kujikita katika kuwaganga na kuwahudumia waliovunjika na kupondeka moyo; kuwafariji wale wote wanaoteseka, tayari kuwasimamisha wale walioteleza na kuanguka. Vijana katika ujana wao, licha ya mapungufu na ukomo wa uwezo wao, lakini ni watu wenye uwezo mkubwa, changamoto na mwaliko wa kushirikiana na vijana hawa wa kizazi kipya daima. Lengo ni kuwapokea na kuwatengenezea mazingira yatakayowawezesha kutekeleza ndoto zao sanjari na kuwashirikisha matumaini. Kumbe, dhamana kubwa na wajibu wa waragibishaji hawa ni kuwasaidia vijana kugundua kwamba, maisha yao yana maana na kuwa wanao mchango wa pekee kwa ajili ya ujenzi wa jumuiya. Baba Mtakatifu anawapongeza kwa sababu utekelezaji wa mradi huu unakwenda sanjari na Mkataba wa Mfumo Mpya wa Elimu Kimataifa “Global Compact on Education”, unaopania pamoja na mambo mengine kujenga na kudumisha sera za elimu shirikishi, inayowawezesha watu wa Mungu kutoka katika dunia ya tatu kuwa na huruma sanjari na ujenzi wa udugu wa kibinadamu; ili kukua na kukomaa kiutu mintarafu tunu msingi za Injili.

Mchakato wa mabadiliko katika mfumo wa elimu mpya duniani
Mchakato wa mabadiliko katika mfumo wa elimu mpya duniani   (VATICAN MEDIA Divisione Foto)

Katika maadhimisho ya Mwaka wa Jubilei ya Miaka 2025 ya Ukristo, Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu, heshima, ustawi na maendeleo ya kiutu na kiroho, ili hatimaye, kujenga jamii inayosimikwa katika haki na mshikamano. Lengo ni kuwarejeshea tena watu wenye ulemavu nafasi yao katika jumuiya inayosimikwa katika furaha na udugu; kwa kuwafungulia fursa za maendeleo mapya ya elimu, ambayo vijana wa kizazi kipya wana shauku nayo. Mwishoni mwa hotuba yake, Baba Mtakatifu Francisko amewaweka wajumbe hawa chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa matumaini na mwalimu wa Mtoto Yesu, ili aweze kuwasindikiza na kuwalinda. Mwishoni kabisa amewapatia baraka zake za kitume na pia ziwaendee wale wanao wahudumia, familia zao pamoja na wafadhili wa mradi huo.

Elimu Shirikishi
10 Januari 2025, 15:10